in , , ,

Chelsea, Man City chali

Riyad Mahrez akishangilia bao lake la tatu dhidi ya Swansea (hat-trick at Swansea)

*Leicester vinara, Arsenal ushindi

Mzunguko wa 15 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umekuja na matokeo ya aina yake, ambapo waliokuwa wakishikilia usukani, Manchester City wameshushwa chini kwa kuchapwa, mabingwa watetezi Chelsea nao wakachapwa huku Leicester wakirejea kileleni.

Chelsea walilala kwa timu ndogo waliopanda daraja msimu huu, Bournemouth wakati walikuwa wakitarajia kwenda kuchukua ushindi kilaini. Vijana wa Jose Mourinho waliteswa na wakagangamala hadi dakika ya 82 walipozidiwa.

Alikuwa Glenn Murray aliyewaliza Chelsea nyumbani kwao Stamford Bridge na kurejesha upya shinikizo kwa kocha Mourinho kama kweli atabakia kuwa kocha hapo, na baada ya mechi alisema wazi kwamba sasa ana hofu ikiwa watapata hata nafasi ya nne wakati ligi ikimalizika Mei mwakani.

Chelsea walishindwa kujilinda ipasavyo na vijana wa Eddie Howe walishambulia, wakapata kona na kufanikiwa kupata bao muhimu lililowaondoa kwenye eneo la kushuka daraja huku likiwaacha Chelsea pale pale kwenye nafasi ya 14, ukiwa ni msimu mbaya zaidi kwa awamu zote za Mourinho hapo Darajani.

Manager José Mourinho akimuhamasisha nahodha wake Branislav Ivanovic wakati wa mchezo.
Manager José Mourinho akimuhamasisha nahodha wake Branislav Ivanovic wakati wa mchezo.

Hii pia ni mara ya kwanza kwa timu iliyotoka kupanda daraja msimu huo huo kuwafunga Chelsea nyumbani tangu Aprili 2001 walipofanya kitu kama cha Jumamosi hii. wapo pointi 14 nyuma ya wanaoshika nafasi ya nne, Manchester United na wapo pointi 17 nyuma ya vinara Leicester.

Diego Costa, mshambuliaji wa kati aliyetarajiwa kurejea katika kiwango huku akiungwa mkono na kocha wake, alishindwa kung’ara, akagusa mpira mara sita tu kwenye kasha la penati la Chelsea lakini hakuweza kuongezea idadi yake ya mabao manne aliyokwishafunga msimu huu.

Wiki mbili zilizopita ilionekana kwamba Chelsea walikuwa wakianza kurejea kwenye kiwango chao taratibu, baada ya kuwa wamefanikiwa kutoruhusu bao katika mechi tatu mfululizo kwenye michuano yote, lakini kupoteza mechi hii kunazua wasiwasi mpya iwapo wataweza kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Rekodi sasa zinasomeka kwamba Chelsea wamepoteza mechi nane kati ya 15 walizocheza EPL na wapo pointi tatu tu juu ya eneo la kushuka daraja na pengo la pointi zao na vinara wa ligi linaanza kuonekana kubwa na lenye tabu kuziba.

STOKE WAWAVURUGIA MAN CITY

Marko Arnautovic akiwafungia Stoke goli la pili dhidi ya  Manchester City ndani ya  Britannia Stadium.
Marko Arnautovic akiwafungia Stoke goli la pili dhidi ya Manchester City ndani ya Britannia Stadium.

Stoke wameharibu sikukwa waliokuwa vinara wa ligi na wanaoutafuta ubingwa kwa udi na uvumba, Manchester City, kwa kuwachapa mabao mawili ya haraka kipindi cha kwanza kisha kuwabana wasipumue.

Mabao yote mawili yalifungwa na Marko Arnautovic na pia yote yalipikwa na Xherdan Shaqiri, moja likitokana na majalo wakati la pili lilikuwa kwa mpira wa moja kwa moja.

Man City waliocheza bila Sergio Aguero na Yaya Toure ambao ni majeruhi walionekana kukosa mbinu za kurejea mchezoni. Vijana hao wa Manuel Pellegrini hawajashinda katika mechi zao nne za ugenini.

Nafasi chache walizotengeneza ziliishia mikononi mwa kipa Jack Butland, aliyekuwa makini langoni na kuwanyima Kevin de Bruyne na Aleksandar Kolarov mabao yaliyoonekana ya wazi. Kwa matokeo hayo Man City wameshuka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, wakiwa pointi tatu nyuma ya Leicester.

LEICESTER WAREJEA KILELENI

Riyad Mahrez akishangilia bao lake la tatu dhidi ya Swansea (hat-trick at Swansea)
Riyad Mahrez akishangilia bao lake la tatu dhidi ya Swansea (hat-trick at Swansea)

Leicester wameendeleza moto wao, lakini safari hii mwiba si Jamie Vardy, bali Riyad Mahrez aliyefunga mabao matatu kwenye mechi dhidi ya Swansea na kuzidi kumtia matatizoni kocha Garry Monk.

Mahrez alifunga kwa kichwa bao la kwanza dakika ya tano tu kabla ya kutulia akafunga jingine japokuwa wengine waliona kama alikuwa ameotea.

Mchezaji wa Swansea, Ki Sung-yueng alijaribu kumpa raha kocha wake kwa kupiga kichwa akidhani amefunga, lakini kikaparaza mtambaa wa panya mara baada ya mapumziko kabla ya Mahrez kucheka na nyavu kufuatia shambulizi la kushitukiza nyumbani kwa Swansea.

Wakati matokeo yanawarejesha Leicester wanaofundishwa na Claudio Ranieri kileleni waliokuwa wameondolewa na Man City wiki iliyopita, yanawaacha Swansea katika nafasi ya 15, wakiwa wameshinda mechi moja tu kati ya 11 za EPL. Leicester wana pointi 32.

Monk anaweza kufukuzwa kazi, nah hii ilikuwa mechi ya pili wakizomewa nyumbani, ikiwa ni kiashirio kwamba washabiki nao wamechoka, hivyo huenda suluhu ikawa ni kupata kocha mwingine.


ARSENAL WACHANUA KWA SUNDERLAND

Olivier Giroud, kati, akiifungia Arsenal goli la pili dhidi ya  Sunderland katika dimba la  Emirates Stadium
Olivier Giroud, kati, akiifungia Arsenal goli la pili dhidi ya Sunderland katika dimba la Emirates Stadium

Arsenal wamefanikiwa kupata ushindi muhimu wa mabao 3-1 dhidi ya Sunderland waliokuwa wanaanza kuamka chini ya kocha mpya Sam Allardyce.

Mshambuliaji wa kati wa Arsenal, Olivier Giroud alizifungia timu zote mbili bao moja moja, akijifunga kimakosa kabla ya mapumziko kutokana na mpira wa adhabu ndogo waliopewa Sunderland kabla ya kurekebisha makosa yake na kufunga kutoka kwenye eneo hilo hilo baada ya mapumziko.

Kinda Joe Campbell aliyeanzishwa kipindi cha kwanza ndiye alitangulia kufunga bao la kuongoza baada ya kutengewa vyema na kiungo aliye kwenye kiwango cha juu, Mesut Ozil, akikamilisha mfululizo wa pasi saba. Kiungo Aaron Ramsey alifunga bao la tatu baadaye.

Kwa matokeo hayo Arsenal wanashika nafasi ya pili wakati Sunderland wamerejeshwa kwenye eneo la kushuka daraja licha ya kucheza kwa nidhamu, hasa kwenye ulinzi na pia kushambulia kwa akili. Allerdyice anawabadilisha Sunderland kidogo kidogo.

Arsenal wanacheza bila kuwa na Santi Cazorla na Alexis Sanchez, wakashambulia vyema lakini ngome yao ililegalega na itabidi wamshukuru kipa mkongwe, Petr Cech.

MAN UNITED SARE NA WEST HAM

Anthony Martial, katikati,  anajitahidi kuipenya ngome yenye nidhamu ya West Ham ndani ya  Old Trafford
Anthony Martial, katikati, anajitahidi kuipenya ngome yenye nidhamu ya West Ham ndani ya Old Trafford

Manchester United wameangukia nafasi ya nne baada ya kushindwa kufungana na West Ham katika dimba la Old Trafford.

United walikuwa na bahati, kwani nusura wageni wafunge mabao mawili kupitia kwa Mauro Zarate na Winston Reid katika muda mfupi.

Vijana wa Louis van Gaal ambao msimu huu wamefungwa bao moja tu nyumbani wanaonekana kujilinda vyema lakini tatizo linaanzia kwenye kiungo na ushambuliaji, ambapo washabiki wamekuwa wakimlalamikia kocha kwa mfumo wake wanaosema unachusha.

Laiti United wangeshinda, basi wangeshika nafasi ya pili, wakishindwa pia kutumia faida ya mahasimu wao wa Manchester waliopoteza mechi katika mchezo wa mapema mchana.

Hata hivyo inabidi washukuru hata kwa matokeo hayo na kumaliza mechi wakiwa 11 kwani katika kipindi cha kwanza, kiungo Bastian Schweinsteiger alimnyooshea mkono wake mlinzi wa West Ham, Reid, lakini inaelekea mwamuzi, Mark Clattenburg hakuona tukio hilo.

Nahodha Wayne Rooney hakucheza, ambapo amekuwa akiwasikitisha washabiki wanaosema kwamba mchango wake hauonekani kuwa chanya kwa timu. Mfaransa Anthony Martial ndiye alichezeshwa kama mshambuliaji wa kati Jumamosi hii.

Oriol Romeu akifunga goli la kusawazisha kwa Southampton dhidi ya  Aston Villa ndani ya  St Mary’s Stadium.
Oriol Romeu akifunga goli la kusawazisha kwa Southampton dhidi ya Aston Villa ndani ya St Mary’s Stadium.

Hata hivyo hakuonekana tishio, na aligusa mpira mara 46 tu, chache kuliko mchezaji mwingine wa United, ukiacha golikipa. Alionekana kama hapewi mipira na wenzake au labda alishindwa kuifuata inavyotakiwa.

Van Gaal alionekana kusikitishwa na safu yake ya ushambuliaji msimu huu, akisema angekuwa na wachezaji kama Luis Suarez wa Barcelona au Sergio Aguero wa Man City, wangefunga mabao mengi kuliko waliyo nayo sasa.

Katika matokeo mengine, Southampton walikwenda sare ya 1-1 na Aston Villa, Watford wakawapiga Norwich 2-0 huku West Bromwich Albion wakitoshana nguvu na Tottenham Hotspur kwa bao 1-1.

Wakati nafasi sita za juu zinashikwa na Leicester, Arsenal, Man City, Man U, Spurs na West Ham kwa mtiririko huo, nafasi sita za chini kuanzia mkiani wanazo Villa, Newcastle, Sunderland, Bournemouth, Norwich na Swansea. Jumapili hii Newcastle wanawakaribisha Liverpool.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Rushwa ya FIFA inatisha

Tanzania Sports

Liverpool wa Klopp hoi