*Jamaica yatwaa medali zote za mita 200
Usain Bolt ameweka rekodi ya kuwa mtu wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 100 na 200.
Bolt ameshinda mbio hizo wakati taifa lake la Jamaica nalo liking’ara, kwa kutwaa medali zote tatu za dhahabu, fedha na shaba.
Katika fainali iliyofanyika usiku wa Agosti 9, Bolt alikimbia kwa sekunde 19.32; Yohan Blake sekunde 19.44 na Warren Weir sekunde 19.88. Blake na Weir wana umri wa miaka 22.
Katika mbio za mita 100 Agosti 5, ambapo wengi walitarajia Blake ashinde, baada ya kuwapo habari za Bolt kuanguka kiwango, Bolt aliwaonesha kwamba walikosea.
Alikimbia kwa sekunde 9.63, Blake akimfuatia kwa sekunde 9.75 huku Mmarekani Justin Gatlin akitwaa medali ya shaba kwa kuwa wa tatu, akikimbia kwa sekunde 9.79.
Bolt sasa ameifikia rekodi ya dunia iliyowekwa na
Michael Johnson katika michezo ya Atlanta nchini Marekani mwaka 1996.
Kwa ushindi wake, Bolt mwenye umri wa miaka 25 amepata heshima kubwa aliyokuwa akiiwania, baada ya kuweka rekodi ya kushinda mfululizo medali hizo kwenye riadha.
Wakati mamilioni ya watu walishampa heshima kwa kushinda dhahabu mara tatu Beijing na kutetea ubingwa wake wa mbio za mita 100, Bolt alisisitiza lazima kwanza apate dhahabu kwa mbio za mita 200.
Ulikuwa usiku wa furaha kwa wana Jamaica na rafiki zao kwa ujumla, kwa jinsi walivyoitangaza na kuipa sifa nchi yao, huku bendera za Jamaica zikipeperushwa.
Baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 200, Bolt kama kawaida yake alishangilia kwa kufunga mikono kana kwamba anasali, kusujudu ardhini, kunyoosha kidole mbele na juu na kuonesha ishara ya kufyatua mshale kutoka kwenye upinde.
“Hiki ndicho ilikuwa nakitafuta na nimekipata. Najivunia sana hatua hii. Nilikuwa na msimu mbaya lakini nikaja hapa na kufanya nilichotakiwa kufanya.
“Tumekuwa tukijitahidi msimu wote, tulipeana moyo na hata kuweka shinikizo ili tufanikiwe, na sasa tunayo furaha,” alisema akionesha jinsi mambo yalivyokuwa kwenye kambi ya timu ya nchi yao.
Alipoulizwa iwapo angeweza kuweka rekodi ya dunia, kwa maana ya kukimbia katika muda mfupi kuliko ilivyopata kufanywa na yeyote, Bolt alisema:
“Nadhani ingewezekana…lakini naona kwamba sikuwa katika hali nzuri vya kutosha. Nilikuwa nimebanwa, nilihisi maumivu kidogo mgongoni mwangu.
“Nilikuwa najitahidi kurejea kwenye kiwango, lakini niliacha kukimbia maana nilibaini kwamba haingekuwa rekodi ya dunia, ilikuwa vigumu. “Nilijitolea hasa kwa kazi hii, najua london inamaanisha nini kwangu. Nilikuja hapa na nikajitoa kwa kila hali na sasa nafurahi nimefanikiwa. “Sikuweka rekodi ya dunia – kwa kweli ningetaka sana kufanya hivyo kwenye mbio za mita 200 – lakini nimejawa furaha,” akaongeza.
Blake akizungumzia ushindi wao, alisema kwamba Bolt ndiye aliyemtia nguvu na moyo katika msimu wote na kwamba mamb yote yamekuwa yakienda vizuri.
Weir aliyetwaa medali ya shaba naye alikuwa na yake: “Ni heshima kubwa kuja hapa na kufanya kile tulichotumwa nan chi yetu – kuwa kwenye tatu bora hapa. Mapenzi ya London ni mazuri sana.”
Katika mazoezi na mbio za maandalizi, Blake alimshinda Bolt mata kadhaa, ikiwa ni pamoja na nchini Italia.
Wakati fulani katika mbio za Alhamisi hii, Blake alimpita Bolt, lakini haikuwa kwa muda mrefu. Bolt alijiimarisha, kumpita na alipomaliza mbio aliweka kidole mdomoni kama anayemnyamazisha mwenzake.
Comments
Loading…