*Bayern Munich wawachinja Juventus
Wakicheza kwa kujiamini tangu mwanzo, Paris Saint-Germain wamewabana vilivyo Barcelona, na kutoa sare ya mabao 2-2.
Nyota wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic aliyeshindwa kung’ara mapema, alitokea kuwa tishio kipindi cha pili, kwa kufunga bao na kutoa pande la kusawazisha.
Barca walitangulia kufunga kupitia kwa shujaa wao, Lionel Messi katika dakika ya 38, baada ya mabeki kumsahau na kujikuta wamechelewa kumkaba, akiachia mikwaju yake ya kushitukiza na kudhuru.
David Beckham akiwa kwenye kiungo, PSG walisukuma mashambulizi katika mchezo wa kukamiana na kutumia nguvu, ambapo iliwachukua hadi dakika ya 79 Ibrahimovich kusawazisha.
Hata hivyo, Barca walipata penati baada ya golikipa wa PSG, Salavatore Sirigu kumdaka Alexis Sanches badala ya mpira.
Nahodha Xabi hakufanya kosa kuweka mpira kwenye kamba dakika ya 89, hivyo kuongeza shinikizo kwa wenyeji waliokuwa wameamini mechi ingeishia 1-1.
Wakati Barca wakijua watapata ulaini zaidi kwenye mechi ya marudiano Jumanne ijayo, kasi ya PSG iliendelea, na Ibrahimovic alimtilia mpira wa kichwa Mfaransa Blaise Matuidi aliyeachia fataki iliyomshinda kipa Victor Aldes.
Messi alitoka nje kabla ya mechi kumalizika baada ya kuumia, na kuna taarifa kwamba anaweza kukosa mechi ijayo, lakini pia anaweza kukaa nje kwa hadi wiki tatu, kutegemeana na matokeo ya picha atakayopigwa Jumatano hii.
Mlinzi Javier mascherano naye aliumia na kubebwa kutoka uwanjani, hivyo anaweza kukosa mechi ya marudiano katika dimba la Camp Nou, hivyo kuwapa ahueni PSG.
Barcelona walishatwaa kombe la UEFA mara nne wakati PSG walipata kutwaa lile lililokuwa linaitwa The UEFA Cup Winners’ Cup 1996, michuano iliyoanza 1960 na kufutwa 1999.
Katika mechi nyingine, Bayern Munich waliwararua Juventus mabao 2-0, baada ya kucheza mechi dimbani kwao Allianz Arena kwa kujiamini, tofauti na walipochakazwa na Arsenal mechi iliyopita.
Wauaji wake walikuwa David Alaba dakika ya kwanza na Thomas Mueller dakika ya 63.
Bayern wanataka kuweka rekodi ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya tano, baada ya kutawazwa wafalme wa Ulaya 1974, 1975 na 1976, kabla ya kutwaa hili jipya 2001.
Comments
Loading…