in , ,

Barcelona fainali Ulaya

*Guardiola asema Messi kama Pele

Barcelona wameingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) licha ya Bayern Munich kupata ushindi wa 3-2 kwenye mechi ya mkondo wa pili.

Barcelona wanaofundishwa na Luis Enrique wanataka kutwaa mataji matatu msimu huu, ambapo wamebakisha mechi moja wajihakikishie ubingwa wa Hispania.

Bayern walipambana kujaribu kugeuza matokeo ya kuchapwa 3-0 kwenye mechi ya kwanza ugenini lakini Barca wakiwa na nyota wa dunia, Lionel Messi, hawakukubali.

Barca wamefika pia fainali ya Kombe la Mfalme nchini mwao wakati katika UCL watakutana na ama mahasimu wao katika La Liga, Real Madrid au Juventus wa Italia.

Safu ya ushambuliaji ya Barca imeonesha nguvu kubwa, kwani katika msimu huu wa 2014/15 wachezaji wake watatu, Messi, Neymar na Luis Suarez wametikisa nyavu mara 114 kati yao.

Hii ni mara ya kwanza tangu 2011 kwa Barcelona kufika fainali ya UCL. Barca waliwachanganya Bayern kwani Wajerumani wanaofundishwa na Pep Guardiola walilenga kutoruhusu hata bao moja.

Wakiwa na deni la mabao matatu, Bayern walifufua matumaini ya washabiki wao waliokuwa wakifuatilia kwa shaka, pale Medhi Benatia alipofunga kwa kichwa mapema.

Hata hivyo, Barca walisawazisha kupitia kwa Neymar wakionesha ushirikiano mzuri na Suarez na Neymar tena akawaadhibu kwa bao la pili.

Robert Lewandowski na Thomas Muller waliendeleza jitihada za Bayern kwa kufunga mabao ambayo hata hivyo hayakuwasaidia zaidi ya kuwafuta machozi tu.

Real Madrid sasa watatakiwa Jumatano hii kugeuza matokeo ya awali ambapo walipigwa na Juventus 2-1 katika mechi ya awali ili waweke hai matumaini ya kutetea ubingwa wao.

Bayern watajilaumu kwa kupoteza nafasi kadhaa na pia kushindwa kuwa na ukuta mzuri kuwazuia Barca mbele ya washabiki waliokuwa na tamaa ya ushindi katika dimba la Allianz Arena.
Guardiola aliyekuwa kocha wa Barcelona kati ya 2008 na 2012 amesema kwamba Messi ni mchezaji mzuri na sasa anamfananisha na gwiji wa soka wa Brazil, Pele.

Messi ndiye aliwaongoza Barca kuwacharaza Bayern kwenye mechi ya awali na Guardiola anasema inakuwa ngumu kumzuia.

“Huyu ndiye mwanasoka bora wa wakati wote. Namfananisha na Pele. Nadhani Barca watatwaa kombe la nne la ubingwa wa Ulaya. Amerejea kwenye kiwango cha juu, yuko pale nilipopata heshima ya kumfundisha,” anasema Guardiola.

Messi amefunga mabao 53 msimu huu katika mashindano yote, akivuka ya msimu wote uliopita yaliyokuwa 44. Guardiola na Messi katika misimu minne waliwezesha timu kutwaa makombe 14.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Paul Pogba habari ya mji

Ulaya ni Barcelona na Juventus