Athletic Bilbao wametwaa taji la Super Cup la Hispania, baada ya kuwazidi nguvu Barcelona kwa wastani wa mabao 5-1.
Barcelona walikuwa wamejiandaa kupambana kufa na kupona nyumbani ili kutibu majeraha na kurejesha mabao manne waliyochapwa nyumbani kwa Bilbao majuzi, lakini kocha Luis Enrique na wachezaji wake walimudu bao moja la kufunga na kufungwa pia moja.
Ulikuwa usiku mchungu kwa Barca, hasa Lionel Messi na Luis Suarez walioaminiwa kusaidia timu kupata mabao mengi na ya haraka, lakini mambo yalikwenda vibaya kwao, ikawa neema kwa Bilbao ambao wamepata kombe la kwanza katika miaka 31, lakini wakifurahi zaidi kwa kulipatia Nou Camp.
Kana kwamba mzigo waliokuwa nao hautoshi, waliongezwa kwa mlinzi wao, Gerard Pique kupewa kadi nyekundu baada ya kipindi cha pili kuanza kutokana na mchezo mbaya, na huku Barca wakiwa na bao moja wakijitahidi kupata mengine matatu, walikatwa maini baada ya Aritz Aduriz kufunga la kusawazisha na kufanya uwe mzigo usiobebeka kwa mabingwa hao wa Ulaya na Hispania.
Bilbao nao walionja shubiri ya kadi nyekundu, baada ya mchezaji wao, Kike Sola kupewa kadi nyekundu, lakini washabiki hawakujali kwani walishaanza kushangilia ushindi na ubingwa. Barcelona waliutawala mchezo lakini hawakuweza kuipenya ngome ya Bilbao.
Katika mechi ya mkondo wa kwanza Bilbao waliwalambisha mchanga Barca, ambapo Aduriz alifunga mabao matatu – hat trick na jingine likatiwa kimiani na Mikel San Jose.
Mshamuliaji wa Barcelona anayewaniwa na Manchester United, Pedro, alipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga lakini alishindwa kuzitumia na baada ya kuonekana kupwaya akatolewa nje dakika ya 68.
Kocha Enrique anaingiza timu kwenye michuano ya Ligi Kuu huku akiwa na matatizo kwenye ukuta wa timu, ambapo kwenye mechi ya Jumatatu hii, kipa Marc-Andre ter Stegen alianzishwa benchi, baada ya kuruhusu mabao manane kwenye mechi mbili za mashindano tofauti.