*Arsenal wakaribia kumnasa Sanchez
*Pia Debuchy na kipa kinda wa Finland
Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Barcelona na Liverpool juu ya mauzo ya Luis Suarez yanaharakisha Arsenal kumtwaa Alexis Sanchez wa barca.
Baada ya Sanchez kukataa kubadilishwa na Suarez pamoja na kiwango cha fedha ili ajiunge na Liverpool, Barca wanatafuta fedha ili wawalipe Liverpool.
Liverpool inasemekana wamekubali kupokea pauni milioni 63 kwa mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya England (EPL) hivyo Barca wanataka kukusanya fedha ili wamchukue haraka iwezekanavyo.
Manchester United nao wanamtaka Sanchez (25), lakini inaelezwa kwamab Arsenal wapo mbele zaidi katika majadiliano japokuwa hawajafikia bei halisi.
Liverpool wanataka fedha taslimu mapema ili nao wafanye mambo yao, ambapo Barca wanataka pauni milioni 26 kwa Sanchez lakini Arsenal waliweka mezani dau la pauni milioni 19.8.
Mazungumzo zaidi yanaendelea wikiendi hii na ikishindikana Man U wanaweza kumwaga fedha nyingi zaidi japokuwa Sanchez anapenda kucheza Arsenal, maana anataka kuwa London.
Arsenal wanaendelea vyema na mchakato wa kuziba pengo la beki wa kulia, Bacary Sagna aliyekwenda Man City kwani Newcastle wamekubali pauni milioni 7.9 ili wawauzie beki wao Mfaransa, Mathieu Debuchy.
Imeelezwa kwamba Debuchy (28) baada ya Ufaransa kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia Ijumaa nchini Brazil, atatinga London wakati wowote kwa ajili ya vipimo vya afya.
Katika hatua nyingine, Arsenal wamewapiga kumbo Liverpool kwa kusajili golikipa wa kimataifa wa Finland, Hugo Keto kutoka klabu ya HJK Helsinki.
Liverpool walikuwa wakitaka kumsajili Keto (19) lakini tayari Arsenal wamekamilisha mambo kwa kumfanyia vipimo vya afya na kufaulu wiki hii, ambapo amesaini mkataba wa miaka mitatu.
Keto alikuwa shabiki mkubwa wa Liverpool alipokuwa mtoto na msimu uliopita alifanya majaribio klabuni hapo ambapo alicheza mechi kadhaa na timu ya vijana.
Hata hivyo, alitumia muda fulani katika akademia ya Arsenal lakini Liverpool walitarajia angerejea msimu huu na kumsajili kwa ajili ya timu ya vijana, akiwa na urefu wa 6’3″aje kuingia timu ya wakubwa siku zijazo.
Kuna habari zisizothibitishwa kwamba Liverpool wanafikiria kumsajili mshambuliaji wa kati wa AC Milan, Mario Balotelli katika harakati za kuziba pengo la Suarez anayekaribia kuondoka.
Rais wa AC Milan, Silvio Berlusconi alinukuliwa Ijumaa akisema kwamba alikuwa ameshafikia dili kubwa na klabu ya EPL (inadhaniwa ni Arsenal) lakini kutokana na kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Dunia, hakutarajia tena kupata dau kubwa kwa Mtaliano huyo mtukutu.
Comments
Loading…