ALIYEKUWA mfadhili mkuu wa Klabu ya Simba, Azim Dewji, ameibuka na kusema kuwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) halipaswi kuwachagulia wanachama wa klabu hiyo kiongozi na kumtaja mgombea aliyeenguliwa, Michael Wambura, hana sifa ya kuiongoza klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini, Dewji, aliitaka TFF iachane na agenda ya ‘siri’ iliyonayo na kuwaacha wanachama wa Simba wachague kiongozi wanayeamini atawafaa na atakayehakikisha heshima ya timu hiyo kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita inarejea.
Dewji alisema kuwa Simba ambayo kwa sasa imepoteza ushindani, inahitaji kupata kiongozi mwenye kuimarisha umoja na malengo ya kuiendeleza klabu hiyo na si vinginevyo.
“Sioni kama Wambura anaweza kuisaidia Simba kwa sababu amesema hataki wafadhili na hakuna klabu iliyopata mafanikio bila wafadhili au kushirikiana na watu wenye fedha,” alisema Dewji.
Alisema pia anashangaa kuona mmoja wa wagombea wa klabu hiyo anaungwa mkono na watani zao Yanga jambo ambalo linampa mashaka kwamba akifanikiwa kuingia madarakani, hali itakuwa mbaya kwa upande wao.
“Niliamua kukaa kimya muda mrefu lakini waswahili wanasema kwa uchungu wa mwanae hata bubu anaweza kuzungumza, nasema hivi apite, asipite, Wana-Simba wanaakili, watachagua mtu makini,” alisema mfadhili huyo wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi.
ATAKA SIMBA IWE KAMPUNI
Mfadhili huyo wa zamani wa Simba amesema kuwa anaushauri uongozi utakaoingia madarakani ufanye mchakato wa kubadili mfumo wa klabu na kuwa kampuni.
Dewji alisema kwamba kufanya hivyo itasaidia kupata fedha za kujiendesha kwa wanachama na watu mbalimbali kujitokeza kununua hisa za klabu.
“Ashanti imekuwa inapanda na kushuka kama homa kwa sababu haina pesa, Azam bila pesa isingekuwa bingwa, TP Mazembe pia isingefanya vizuri, kipimo cha Simba ni Yanga na si Mbeya City wala Azam”, Dewji aliongeza.
Alisema pia kundi la Friends halihusiki kuhujumu timu na kupata matokeo mabaya na kama ni kweli, wapewe nafasi ya kuiongoza klabu ili ushindi uwe unapatikana.
Comments
Loading…