*Yanga, Simba wapigishwa kwata
Ubingwa wa Tanzania unanukia Chamazi kwa Azam ambao Jumapili hii waliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya mnyama Simba Sports Club.
Katika pambano hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kulikuwa na kila aina ya ushindani dimbani na nje lakini Simba walielemewa.
Kituko kilikuwa kwa washabiki wa Yanga kuwashangilia Simba ili kuzuia Azam wasiwaache mbali huku wale wa Yanga wakiwashangilia Simba ili Yanga watwae ubingwa.
Azam walipata mabao yao kupitia kwa John Bocco na Hamisi Mcha wakati Simba walipata la kufutia machozi kupitia kwa Joseph Owino lakini halikusaidia kitu, hata ilifika mahali kipa wao Ivo Mapunda alikuwa akiingia ndani kusaidia mashambulizi.
Kwa matokeo hayo, Azam wamefikisha pointi 53 kwa mechi 23 wakati Yanga wakiwa na pointi 46 kwa mechi 22.
Yanga wenyewe walipoteza pambano lao Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga walipofunga 2-1 na Mgambo JKT. Waliruhusu bai mapema dakika ya kwanza kwa mkwaju wa Fully Maganga ambalo lilimkuta kipa Juma Kaseja kana kwamba alikuwa akifikiria kwingine.
Licha ya kucheza wachezaji 10 kwa dakika 60 baada ya Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi mbili za njano, Mgambo waliwahimili Yanga waliosawazisha bao kwa penati ya Nadir Haroub Canavaro lakini Malimi Busungu kutia kimiani bao la ushindi baadaye.
Watu wengi hawakuamini jinsi Yanga walivyokosa mabao mengi licha ya kushambulia wakati wote, ambapo ajabu ni kwamba yalikuwa yakiokolewa kwenye mstari wa goli, hadi baadhi ya wachambuzi wakadai kamati ya ufundi ya Mgambo imefanya vitu vyake.
Mbeya City walifanikiwa kuwashinda ndugu zao Prisons 1-0 na hivyo kufikisha pointi 45, moja nyuma ya Yanga, lakini mabingwa hao watetezi wana mechi moja mkononi. Bado Mbeya City watakipiga na Azam mjini Mbeya.
Comments
Loading…