*RATIBA RCL KUPANGWA J’NNE, LIGI KUANZA MEI 12 *
Upangaji ratiba (draw) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike
juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi
hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya
ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka
RCL isogezwe mbele.
Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia
athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja
kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa
wachezaji kwa msimu mpya.
Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari
imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. Mabingwa ambao
wamewasilishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2),
Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es
Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC
(Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe
(Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1),
Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo
ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni
uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa
ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa
wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
Mikoa iliyoshindwa kuwasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa,
Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.
*TAIFA STARS KUANZA COSAFA JULAI 6*
Taifa Stars imepangwa kundi A la michuano ya Kombe la COSAFA ambapo
itacheza mechi yake ya kwanza Julai 6 mwaka huu jijini Lusaka, Zambia dhidi
ya Shelisheli.
Upangaji ratiba (draw) wa mashindano hayo ulifanyika juzi (Mei 3 mwaka huu)
jijini Lusaka ambapo timu nyingine zilizo na Taifa Stars katika kundi hilo
ni Namibia na Mauritius. Kundi la Taifa Stars litachezea mechi zake jijini
Lusaka.
Mechi ya pili ya Taifa Stars katika hatua ya makundi itakuwa Julai 8 mwaka
huu dhidi ya Mauritius. Mechi ya mwisho katika hatua hiyo itakuwa Julai 10
mwaka huu dhidi ya Namibia.
Kundi B lina timu za Kenya (Harambee Stars), Botswana (Zebras), Lesotho na
Swaziland. Hatua itakayofuata baada ya hapo ni ya mtoano (knockout) na kila
kundi litatoa timu moja tu.
Iwapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itafuzu kwa
hatua itakayofuata itacheza Julai 13 mwaka huu na Afrika Kusini (Bafana
Bafana) ambayo pamoja na timu nyingine tano zimekwenda moja kwa moja katika
hatua ya mtoano.
Nyingine zilizokwenda moja kwa moja hatua ya mtoano ni wenyeji Zambia,
Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Malawi ambazo kwenye viwango vya ubora vya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ziko juu ya zile
zilizoanzia hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA
itafanyika Julai 20 mwaka huu.
Timu ya Azam inatarajiwa kurejea nchini kesho (Mei 6 mwaka huu) saa 7
mchana kwa ndege ya Emirates kutoka Morocco ambapo jana (Mei 5 mwaka huu)
ilicheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya
huko.
Azam ilipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1, hivyo kutolewa katika raundi ya
pili ya mashindano hayo. Mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam
timu hizo zilitoka suluhu.
Comments
Loading…