*Hamann, Keane, McGrath wamvaa
*‘Anaishusha hadhi Man United’
Mjadala wa wachezai kujiangusha makusudi katika eneo la hatari la timu pinzani ili wapate penati umerejea kwa nguvu.
Safari hii kidole kimeelekezwa kwa mchezaji wa Manchester United, Ashley Young.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Dietmar Hamann amemtuhumu Young kwa kujirusha mara kwa mara na kwamba anaishushia hadhi klabu yake.
Young alianguka ndani ya eneo la 18 la Real Sociedad Jumanne hii katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mwamuzi alitoa penati.
Hata hivyo, kwa waliokuwa wakitazama mpira huo, pamoja na wachambuzi wa Uingereza, ilionekana kwamba hakuangushwa bali alijirusha kwani hakuonekana kuguswa wala kusukumwa na mchezaji yeyote.
Hata hivyo, kwa bahati ya Sociedad, penati iliyotolewa na kupigwa na mfungaji hodari, Robin van Persie iligonga mwamba na kurudi uwanjani kisha ikaokolewa na mabeki wa Wahispania hao.
Hamman anasema kwamba Young amekuwa mbaya katika kujirusha hivyo kwamba anamzidi mpachika mabao wa Liverpool, Luis Suarez aliyewahi kukiri kujirusha katika mechi ili timu yake ipate penati.
Young amewahi kupewa kadi ya njano na mwamuzi kwa kujirusha na sasa Hamann anaamini kujirusha kwake kunakuwa tatizo kubwa sana.
Wengine ambao wamemshutumu Young kwa kujirusha ni mchezaji na nahodha wa zamani wa Mashetani Wekundu, Roy Kean na mchambuzi wa masuala ya soka, Ray Wilkins, aliyesema vitendo vya Young vinasikitisha.
Suarez alipata kushambuliwa pia, akatetewa na kocha wake, Brendan Rodgers hadi pale alipokiri mwenyewe kwamba alifanya hivyo kwa ajili ya timu, kisha Rodgers akasema angechukuliwa hatua za kinidhamu ndani kwa ndani. Siku hizi amebadilika.
“Nadhani mnakumbuka yale ya Suarez, lakini Ashley Young ana tabia mbaya zaidi, ni kudanganya kwa waziwazi kabisa kudai penati wakati hujaguswa.
“Kwa hadhi yao, Manchester United hawahitaji mchezaji anayejirusha kama huyo kudanganya ili eti kushinda mechi ya soka,” akalalama Mjerumani huyo Hamann.
Mchezaji mwingine wa zamani wa Manchester United, Paul McGrath alisema Young asipoangalia atamaliza umaarufu wake kwenye soka na kwamba anaweka mfano mbaya kwa vizazi vijavyo.
Katika Ligi Kuu ya England, Gareth Bale amepata kudaiwa kuanguka kirahisi mno, na amepata zaidi ya kadi moja ya njano akiwa na Tottenham lakini bila shaka sasa atajifunza na kuwa na adabu Real Madrid.
Comments
Loading…