*Watwaa Ngao ya Jamii
Arsenal wameonesha kiwango cha juu katika soka, wakawafyatua Manchester City 3-0 na kutwaa taji la Ngao ya Hisani kwenye mechi nzuri iliyofanyika Uwanja wa Wembley.
Vijana wa Arsene Wenger waliingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya mechi ya mwisho dimbani hapo dhidi ya Hull msimu uliopita, ambapo walimaliza ukame wa mataji wa miaka tisa kwa kutwaa Kombe la FA.
Hata hivyo waliingia wakiwa na kumbukumbu isiyo nzuri dhidi ya timu kubwa za Ligi Kuu ya England kama Man City, ambao mechi ya mwisho ya msimu uliopita waliwakung’uta 6-3 wakati emchi ya kwanza walikwenda sare.
Alikuwa ni kiungo Santi Cazorla aliyewanyanyua maelfu ya washabiki wa Arsenal dakika ya 21 kwa kupachika bao la kwanza, la pili likitiwa kimiani na kiungo mwingine, Aaron Ramsey dakika ya 42 kabla ya Olivier Giroud aliyetokea benchi akipachika bao la tatu kwa ufundi wa aina yake dakika ya 60 na kuwakata kabisa maini Man City.
Arsenal walianza na wachezaji wake wanne wapya, Alexis Sanchez, Calum Chambers, Mathieu Debuchy na baadaye Joel Campbell ambao waling’ara sambamba na wengine kama Yaya Sanogo aliyepika bao la pili.
Katika hali isiyo ya kawaida, Wenger aliwachezesha mabeki wa kushoto, Nacho Monreal na Chambers kama mabeki wa kati lakini waling’ara kabla ya Laurent Koscielny kuingia kipindi cha pili.
Arsenal waliwakosa Per Metersacker, Mesut Ozil na Lukas Podolski wakati Man City hawakuwa na Sergio Aguero, Joe Hart, Vincent Kompany na Pablo Zabaleta.
Manuel Pellegrini alionekana kukosa mbinu za kubadili mchezo, ambapo golini alianza na kipa wake mpya, Willy Cabalero aliyesema ni namba moja sambamba na Joe Hart. Timu zote ziliwakosa wachezaji waliofika hatua za mbele za fainali za Kombe la Dunia na mataifa yao, kwani wanahitaji mapumziko.
Hii ni Ngao ya Jamii ya kwanza kwa Arsenal tangu 2004 na ushindi huo ni salamu tosha kwa timu zinazoshiriki ligi kuu ya England kwamba msimu huu Arsenal hawataki utani. Arsenal wanaanza ligi kuu wikindi hii kwa kucheza na Crystal Palace nyumbani wakati Man City wanasafiri kupambana na Newcastle
Comments
Loading…