*Liverpool bado hawajakaa sawa
Arsenal wamefanikiwa kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa msimu wa 15 mfululizo, baada ya kuwalaza Borussia Dortmund 2-0.
Katika mechi hiyo, Yaya Sanogo alifunga bao lake la kwanza kwa Arsenal katika mechi ya kishindani wakati Alexis Sanchez alitikisa nyavu kwa mara ya tatu katika mechi tano za mashindano hayo.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Dortmund wanaoongoza kundi hilo wakiwa na pointi 12 kufungwa, huku Arsenal wakifikisha pointi 10, wakiwaacha Anderlecht wakiwa na pointi tano na Galatasaray wakiwa na moja tu.
Sanogo alifunga dakika ya pili tu ya mchezo baada ya kugongeana vyema na Santi Cazorla, huku Sanchez akifunga lake kwa ufundi mkubwa kipindi cha pli.nusura Alex Oxlade-Chamberlain afunge jingine, lakini shuti lake liligonga mtambaa wa panya.
Kocha wa Dortmund Jurgen Klopp aliyechezesha nyota wake alikuwa ameonya mapema kwamba licha ya kwamba walishafuzu, hawangewaonea huruma Arsenal. Kuna tetesi kwamba Arsenal wanataka siku Wenger akiondoka, Mjerumani huyo achukue hatamu Emirates.
Washabiki pamoja na mitandao ya jamii walionesha kutofurahia waliposikia jina la Sanogo kwamba angeanza ushambuliaji wa kati badala ya Lukas Podolski, lakini alikata ngebe zao mara moja kwa kukwamisha mpira wavuni, ikiwa ni mechi yake ya 19 kwa Arsenal na alikuwa hana bao. Mechi za kabla ya msimu, hata hivyo, alifunga mabao manne.
Arsenal pia walicheza na kipa namba tatu, Emmiliano Martinez, kutokana na wakubwa zake kutokuwa katika hali ya mchezo. Dakika za lala salama aliokoa bao la wazi baada ya Adrian Ramos kutaka kucheka na nyavu. Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Anderlecht waliwafunga Galatasaray 2 – 0.
LIVERPOOL BADO, ILA WANAWEZA KUVUKA
Liverpool usiku wa Jumatano walikubali bao la kusawazisha katika dakika za mwisho kutoka kwa Wabulgaria Ludogorets na kujiwekea mazingira magumu, lakini yanayowezekana, ya kuvuka hatua hii ya kwanza ya UCL.
Kipa Simon Mignolet aliyeng’ara msimu uliopita, ameendeleza madudu yake, ambapo alifanya makosa na kuruhusu bao la kwanza kupitia kwa Dani Abalo dakika ya tatu tu ya mchezo, lakini Rickie Lambert akasawazisha kwa kichwa dakika tano baadaye na kuwarejesha Liverpool mchezoni.
Jordan Henderson aliwaweka mbele Liverpool kwa kufunga bao la pili dakika ya 37 na wakaamini kwamba wangeondoka Bulgaria na ushindi lakini dakika mbili kabla ya mpira kumalizika, Georgi Terziev akasawazisha kwa kichwa. Mwezi ujao Liverpool watacheza mechi yao ya mwisho dhidi ya Basel dimbani Anfield.
Kwa matokeo hayo, Liverpool wamefikisha pointi nne, sawa na Ludogorets, lakini Wabulgaria hao wakiwa mkiani kwa tofauti ya bao moja, Basel wanazo pointi sita katika nafasi ya pili wakati Real Madrid ni vinara wenye pointi 15 kutokana na mechi tano walizocheza na wameshafuzu.
Katika matokeo mengine Jumatano hii, Atletico Madrid waliwachakaza Olympiakos 4-0, Malmo FF wakalala kwa Juventus 2-0, Basel wakafungwa na Real Madrid 1-0, Zenit St Petersburg wakawafunga Benfica 1-0 na Bayern Leverkusen wakalambwa 1-0 na Monaco.