*Lakini wawavurugia rekodi Wajerumani
*Porto wamewatambia Malaga nyumbani
Arsenal wamepoteza mchezo wa kwanza wa timu 16 bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, na sasa wanahitaji nguvu kubwa kwenye marudiano.
Hadi dakika ya 21 Arsenal walisharuhusu mabao mawili, moja likifungwa na kiungo mshambuliaji Toni Kroos aliyepokea majalo kutoka upande wa kulia wa uwanja akiwa ndani ya eneo la penati.
Bao la pili liliwekwa kimiani na Thomas Muller, baada ya Aaron Ramsey kumsahau beki wa kati, Daniel van Buyten aliyeelekeza mpira golini, ukazuiwa na kipa Wojciech Szczesny, lakini Muller akaupokea ulipotemwa na kuzitikisa nyavu za Emirates.
Baada ya magoli hayo ndipo Arsenal walipoanza kujikusanya, wakijua kwamba ni mlima mrefu kuvuka, watakapokwenda kurudiana nao katika uwanja wa Allianz Arena, Ujerumani.
Mchezaji wa Kijerumani wa Arsenal, Lukas Podolski aliyecheza kwa nguvu, alifanikiwa kupachika bao la kichwa kutokana na mpira wa kona, ambao golikipa Manuel Neuer alishindwa kuudhibiti.
Arsenal walidhani wangeweza kusawazisha, kutokana na jinsi wachezaji walivyojituma, ikiwa ni pamoja na Olivier Giroud kuishia kumlenga golikipa alipomwagiwa majalo na Theo Walcott.
Mambo yaliharibika Bayern walipopata bao la tatu kiaina, na ikawa chungu kwa Arsenal.
Bao hilo lilipatikana kwa gonga ya namna hii; Arjen Robben aliyeingia badala ya Franck Ribery alikimbia na mpira na kumpatia nahodha Philip Lahm.
Baada ya hapo akapewa Mario Mandzukic aliyeanguka na Bacary Sagna wakiuwania, Mandzukic aliugusa kidogo, ukamwendea vibaya Szczsesny, ukapaa juu kabla ya kutinga wavuni.
Hii ni mara ya tatu tu kwa Arsenal kupoteza mechi mbili mfululizo katika uwanja wake wa Emirates, nyingine zikiwa Mei 2009 na Novemba 2010. Kipindi cha kwanza kilishuhudia Bacary Sagna, Thomas Vermaelen na Mikel Arteta wakilimwa kadi za njano kwa rafu, wakijitahidi kwa kila hali kuwazuia Bayern.
Timu hiyo inayofundishwa na Jupp Heynckes anayestaafu msimu wa kiangazi na kumwachia mikoba kocha wa zamani wa Barcelona, Joseph ‘Pep’ Guardiola, imeshinda mechi 10 kati ya 11 zilizopita za ugenini.
Na goli la Podolski lilitia uchafu kwenye rekodi yao, kwa sababu walikuwa wamepitisha dakika 450, yaani mechi tano zilizopita bila kufungwa bao lolote.
Wanaongoza Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa tofauti ya pointi 15.
Katika mechi nyingine, Porto ya Ureno imeifunga Malaga ya Hispania bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika nchini Ureno.
Bao hilo lilifungwa na Joao Moutinho katika kipindi cha pili, na kuwapa faida wenyeji hao katika mechi ya marudiano itakayopigwa Hispania.
Wenyeji walitawala karibu muda wote wa mchezo, hivyo kwamba iligeuka kuwa mechi ya upande mmoja, wakiwaachia Malaga kubisha hodi golini kwao mara moja tu.
Hata hivyo, Porto walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata pamoja na fursa ya kuutawala mchezo kupachka mabao zaidi.
Matokeo hayo yanafuta rekodi ya Malaga kutofungwa katika mashindano ya msimu huu tangu yalipoanza kwenye ngazi za makundi.
Comments
Loading…