Ni usiku wa manane; Septemba Mosi. Washabiki wa Arsenal kote duniani wanaendelea na kile ambacho wamezoea kufanya.
Wapo kama kawaida, bila kujifikirisha juu ya umuhimu wa muda huo, wala kuwa na hofu ya siku ya mwisho wa uhamisho wa wachezaji, kwani hawana hata mmoja wanayemsubiri.
Mambo yalikuwa poa kiangazi
Robin Van Persie, au wengi wapendavyo kumwita, RVP, hakuwa na kikubwa cha kujivunia kwenye Mashindano ya Euro, na alirejea London mapema, kwa kiasi fulani akiwa mnyonge.
Akiwa amepungukiwa na kujiamini kidogo kuliko alivyokuwa Mei, Van Persie aliongeza mkataba wake na washika bunduki hao wa London hadi 2016.
Marouane Chamakh aliyeshindwa kabisa kuwika amehamia Montpellier. Andrey Arshavin akaenda Zenit. Sebastian Squilacci, mtu aliyesahauliwa kaenda kwenye timu mpya iliyopanda daraja Hispania. Benayoun keshaondoka, kama Bendtner na Vela.
Joel Campbell kaenda kwa mkopo kwenye timu iliyomaliza ikiwa katikati ya Ligi Kuu ya England (EPL), huku suala la Denilson likimalizwa chini chini kwa muda wa mkopo wake Sao Paolo kuongezwa.
Idadi ya kawaida ya wachezaji wa akiba imetolewa kwa mkopo pia (wakiwamo Bartley, Wellington na Afobe).
Wachezaji wawili wapya walisajiliwa: Lukas Podolski na Olivier Giroud.
Ryo Miyaichi akarejea klabuni na Pedro Botelho kadhalika, mchezaji aliyepata kibali cha kazi baada ya msimu wa kuvutia kwenye La Liga.
Ignasi Miquel, ambaye mwili wake umeongezeka kuliko alivyokuwa mwaka jana, amepandishwa hadi kwenye timu ya kwanza.
Washabiki wengi wa Arsenal wanakiona kiangazi kama msimu uliokuwa na mambo machache kuliko walivyozoea.
Hakuna usajili mpya kwa ajili ya wachezaji viungo, licha ya tetesi zilizosambaa kwa muda kuhusu
Yann M’Vila.
Washika bunduki hawa wa London wanaona kana kwamba kikosi chao kinapwaya. Kadhalika, suluhu ya tatizo la beki wa kushoto ilipatikana lakini ikaacha wasiwasi, achilia mbali ukweli kwamba kununua washambuliaji hao wawili lilikuwa jambo la kipekee.
Malengo ya timu na wajibu wa washambuliaji hao ni tata: Podolski, mchezaji kiraka mwenye uwezo mkubwa, alidhamiriwa kucheza wingi ya kushoto na kumlisha mipira Van Persie.
Giroud ambaye kimsingi ni mshambuliaji anaonekana kutokuwa chaguo zuri la tatu kukamilisha jopo la maangamizi.
Hata hivyo, Septemba Mosi, washabiki wa Arsenal wanahisi furaha kubwa juu ya klabu yao. Mechi mbili zimeshachezwa kwenye ligi na hadi sasa Arsenal imeshinda zote. Kiangazi sasa kinaonekana kuwa cha mafanikio makubwa.
Unaona sasa, Arsene Wenger, profesa wa soka aliyejizolea sifa kutokana na akili yake, alikuwa na mradi mkubwa alioufanyia kazi kwa muda mrefu.
Baada ya kukamilisha usajili aliopangia muda wake vizuri wakati wa msimu wa kiangazi, Wenger kwa mafanikio makubwa (na ya kushangaza) alibadili mfumo wa uchezaji kuwa 4-4-2, au, kwa usahihi zaidi, 4-2-2-1-1.
Ukweli ni kwamba wazo hilo peke yake halikuwa na cha kushangaza, kwani wengi walishabashiri mabadiliko ya aina hiyo, lakini ni wachache waliokuwa wameamini kwamba yangetekelezwa ipasavyo kama hivi.
Hii ndiyo hali ya sasa ya Arsenal:
Wojciech Szczęsny na Lukasz Fabianski ndio magolikipa wa kikosi cha kwanza. Kwa sababu ya majeraha yake, Fabianski hakuhama wakati wa kiangazi.
Katika safu ya ulinzi, tunao Bacary Sagna (anayeendelea kujiuguza baada ya kuvunjika mguu na anatarajiwa kuwa dimbani ndani ya wiki chache), Carl Jenkinson, Per Mertesacker, Laurent Koscielny, Thomas Vermaelen, Johan Djourou (ambaye hajapata kuacha kuhama), Ignasi Miquel, Kieran Gibbs, André Santos na Pedro Botelho. Song na Coquelin pia wanaweza kuwa viraka hapo.
Ukuta huu umeruhusu mabao, lakini si zaidi ya mara moja kwa mechi. Washabiki wa Arsenal wana hofu kidogo kuhusu nafasi ya beki ya kulia, lakini si sana, kwani Jenkinson ameonesha ugumu.
Kwenye kiungo, tuna Abou Diaby ambaye hajapata kutegemewa sana, kijana wa dhahabu Jack Wilshere, Mikel Arteta, Aaron Ramsey, Tomáš Rosický, Alex Song, Francis Coquelin na Emmanuel Frimpong.
Mabadiliko zaidi yawezekana kwenye kiungo
Wazo la mabadiliko ni kuwa na kiungo mmoja atawale eneo hilo wakati mwingine akisonga mbele kusaidia mashambulizi.
Wakati mwingine wote wanaweza kubadilishana majukumu, hasa ukiwa na mchanganyiko wa Song, Arteta, Wilshere au Coquelin wakishirikiana.
Unapokuwa na wachezaji wanane kwa nafasi mbili, basi kiungo cha Arsenal ni safi. Song alianza mechi zote, akatoka kumpisha Le Coq kwenye mchezo wa kwanza.
Arteta alianza kukipiga mechi ya awali kabla ya Ramsey kuchukua nafasi yake, huku Wilshere akianza kwenye mechi ya pili, ambapo kipindi cha lala salama nafasi yake ilichukuliwa na Diaby.
Timu Ipo Kwenye Fomu Nzuri
Wachezaji wetu wa pembeni ni Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain (Ox), Gervinho na Ryo Miyaichi. Ni Walcott tu kati ya wanne hao asiyeweza kucheza wingi zote mbili.
Ox na Walcott wameanza mechi zote mbili na wamefunga mabao. Gervinho aliingia kuchukua nafasi ya Walcott kwenye mchezo wa kwanza.
Mwisho, lakini muhimu zaidi, makombora ya maangamizi ya Arsene Wenger tangu msimu wa kiangazi ni washambuliaji wake:
Yupo nahodha wa tmu, Robin Van Persie, Lukas Podolski, Olivier Giroud na (bado yuko hapa!) Park Chu Young.
Kama vile kusikilizia zama zile Invincible (msimu wa 2003/2004 ambapo Arsenal ilimaliza mechi zote bila kushindwa hata moja), sasa inachezesha mshambuliaji wa kati na wa pili nyuma yake.
Washambuliaji wote wanne wanaweza kubeba majukumu yote, wakijifuma kwa mzunguko na kuwachanganya adui.
Sasa Arsenal inaweza kuwachezesha Van Persie na Giroud na kumudu timu zenye wachezaji wenye kasi na wagumu kama Stoke, au kumchezesha Podolski dhidi ya timu zinazocheza taratibu zaidi.
Upo utajiri mkubwa wa wachezaji, kwa hiyo bado kuna mbadala (japokuwa Park bado si mmoja wao kwa kweli).
Hata wakitokea majeruhi, bado kuna viraka na ikibidi, Arsenal ina uwezo wa kubadili mfumo na kuwa na mshambuliaji mmoja.
Van Persie na Podolski wote walianza kukipiga mechi ya kwanza, lakini Podolski alitoka kumpisha Giroud, aliyefunga bao. Ushirikiano wa Van Persie na Giroud ulionekana kwenye mechi ya pili.
Japokuwa Podolski anaonekana kana kwamba amechoka, safu ya ushambuliaji imetulia, huku RVP akichanua na kutekeleza ipasavyo jukumu lake kwa umahiri zaidi.
Washabiki wa Arsenal wana matumaini makubwa, na waandishi waliokuwa wanahoji usajili wa Giroud sasa wanaonekana wajinga. Ni wazi kwamba Arsenal sasa wapo kwenye ushindani wa kweli wa mataji.
Haya ni makadirio kwa mwanzo wa msimu
Ukiangalia kwa juu juu, yaweza kuonekana kana kwamba kuna matumaini mno au kukosa uzoefu. Hata hivyo, kwa kuzingatia mambo yalivyo sasa, huu ndio uwezekano mkubwa zaidi wa yatakayotokea baada ya uamuzi wa msimu wa kiangazi.
Wenger anatumia Pauni milioni 23 tu na kutengeneza Pauni milioni 27 hivi.
Bosi huyu anajulikana kwa jinsi anavyobana matumizi, na atafanya kila awezalo kupunguza hata hiyo Pauni milioni 23.
Hii ndiyo sababu naamini kwenye makadirio haya. Jamaa hatatumia pesa nyingi kwenye usajili, na pengine hana haja ya kufanya hivyo.
saria@tanzaniasports.com