Waswahili husema; achekaye mwisho ndiye hucheka zaidi, na ndivyo ilikuwa kwa Arsenal waliotoka nyuma na kuwafunga Crystal Palace 2-1 kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Alikuwa ni Aaron Ramsey aliyemaliza udhia wa Palace waliogangamala kutaka kuondoka na pointi moja Emirates, kwa kufunga bao katika dakika za mwisho, likiwa ni la pili baada ya lile la mlinzi Laurent Koscielny.
Maelfu ya washabiki walikusanyika uwanjani katika Jumamosi iliyokuwa ya joto kiasi kutokana na Jua kuangaza kaskazini mwa London, na walishuhudia mabingwa hao wa Kombe la FA na Ngao ya Jamii wakifungwa bao la kushitukiza dakika ya 35 kupitia kwa Brede Hangeland.
Koscielny alifunga bao zuri kutokana na mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na mchezaji mpya kutoka Barcelona, Alexis Sanchez dakika 10 baada ya bao la Palace. Ramsey alifunga bao lake katika dakika ya 89 na kuwainua maelfu ya washabiki wa Arsenal.
Kadi nyekundu ya tatu kwa siku ya Jumamosi kwenye mechi zote ilitolewa na mwamuzi Jonatham Moss kwa Jason Puncheon aliyemchezea vibaya Nacho Monreal aliyeingia kipindi cha pili badala ya Kieran Gibbs.
Wachezaji watatu waliokuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, Mesut Ozil, Lukas Podolski na nahodha msaidizi Per Mertesacker hawakuwapo kwenye kikosi cha Arsenal.
Jumapili hii Liverpool wanawakaribisha Southampton kwenye Uwanja wa Anfield, huku Liverpool wakiwa wamesajili wachezaji watatu kutoka klabu hiyo, wakati Newcastle watawakaribisha mabingwa watetezi, Manchester City. Jumatatu Chelsea watakwenda kucheza na wageni wa ligi, Burnley.
Comments
Loading…