*Wawashusha daraja Wigan, wawatengua Spurs
Arsenal wamenyakua tena nafasi katika nne bora, wakiwashusha Tottenham Hotspurs hadi nafasi ya tano na kuwashusha daraja Wigan Athletic.
Katika mechi iliyochezwa Emirates saa 72 tangu Wigan kutwaa Kombe la FA dhidi ya Manchester City uwanjani Wembley, Arsenal walianza kuongoza, lakini Wigan walisimama kidete na kusawazisha kabla kipindi cha kwanza hakijamalizika.
Washabiki wa Arsenal walikuwa tumbo joto kutokana na ukamiaji wa Wigan wanaojulikana kwa kuvimbia wapinzani wao mwishoni mwa msimu na kuepuka kushuka daraja, ambapo bao la Lukas Podolski la kichwa la dakika ya 11 lilifutwa na Shaun Maloney mwisho wa kipindi cha kwanza.
Baada ya mawaidha ya kocha Arsene Wenger na Roberto Martinez kwa upande wa Wigan, nusu ya pili ilikuwa kama fainali ya aina yake, kwani Arsenal walihitaji pointi tatu ili kuweka hatma ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mikononi mwao, na Wigan walizihitaji pia kuweka hai matumaini ya kubaki Ligi Kuu ya England (EPL) msimu ujao.
Hata hivyo, ufanisi wa wachezaji wa Arsenal ulianza kuwafunika Wigan kadiri mechi ilivyosonga mbele, ambapo kuanzia dakika ya 63 mambo yaliwaendea kombo wageni, kwani Theo Walcott alicheka na nyavu kabla ya Podolski dakika tano baadaye na Aaron Ramsey dakika ya 71. Santi Cazorla alikuwa mchezaji bora, wakati ushirikiano wa mabeki wa kati, Laurent Koscienly na Per Mertesacker ulionesha uimara mkubwa, kwa mara nyingine nahodha Thomas Vermaelen aliachwa kando, akaingia dakika za majeruhi, kwani baada ya mechi Washika Bunduki wa London walizunguka uwanja kuwashukuru washabiki wao, kwani ndiyo mechi ya mwisho msimu huu.
Mabao hayo manne yalikuwa mwiba mchungu kwa Wigan, iliyomaliza rasmi safari yake EPL na mwakani watacheza ligi ngazi ya pili – Championship – na kipa wake, Joel Robles alilia machozi baada ya mechi na kutulizwa na wenzake. Washabiki kadhaa wa Wigan nao waliangua kilio kutokana na athari za kichapo hicho.
Katika mechi nyingine, Manchester City wamewafunga Reading waliokwishashuka daraja mabao 2-0, kupitia kwa Sergio Aguero na Edin Dzeko, hivyo kupunguza pengo kati yao na mabingwa, Manchester United hadi kufikia pointi 10.
Wigan wanaungana na Reading na Queen Park Rangers (QPR) kushuka daraja, wakati Arsenal, Chelsea na Spurs wanawania nafasi mbili za Ulaya, Spurs wakisubiri kuteleza kwa wenzao, maana wana pointi chache na wote wamebakiza mechi moja moja. United na City wameshafuzu.
Arsenal wanakipiga na Newcastle; Spurs na Sunderland wakati Chelsea watamalizia na Everton katika mzunguko wa mwisho Jumapili hii.
Martinez anaweza kuepuka ligi hiyo ya chini, iwapo chapuo analopigiwa la kuwanoa Everton litatimia, ili achukue nafasi inayoachwa na David Moyes atakayewanoa Manchester United msimu ujao, akirithi mikoba ya Sir Alex Ferguson anayestaafu.
Kuanguka kwa Wigan imekuwa kicheko kwa Sunderland waliokuwa wakipumuliwa na vijana hao wa Martinez, na pia Aston Villa, Fulham na Southampton ambao wangeweza kufikiwa kwa pointi zao 40.
Comments
Loading…