SHIRIKISHO la soka nchini Brazil limemfukuza kazi kocha wa timu ya Taifa ya nchi hiyo Dorival Junior baada ya kukumbana na kipigo kikali cha mabao 4-1 toka kwa Bingwa wa Dunia Argentina katika hatua ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026. Kipigo walichokipata Brazil kwenye jiji la Buenos Aires kiliwaacha Brazil wakiwa na pinti 10 nyuma ya Argentina, huku vyombo vya habari vikibainisha kuwa kichapo hicho ni sababu tosha ya kufutiwa kibarua chake. Upo uwezekano wa Brazil kufuza fainali za kombe la Dunia mwaka 2026, kwani katika fainali hizo kutakuwa na timu 48 ikiwa na maana bara la Amerika kusini litakuwa na wawakilishi 6 moja kwa moja.
Brazil wapo mbele ya Venezuela kwa pointi 6 huku zikiwa zimebaki mechi 4 kumalzia mtangane wa kuwania kufuzu fainali hizo. Lakini matokeo waliyopata Brazil kwenye mchezo wao dhidi ya Argentina umetajwa kuwa sababu za kocha huyo kuondolewa katika benchi la ufundi. Dorival Junior mwenye miaka 62 katika mechi 15 alizoongoza Brazil ameshinda mechi 5 tangu alipochukua jukumu la kuinoa timu hiyo Januari mwaka 2024.

Moja ya matokeo ya kuumiza ni pale Brazil chini ya Dorival Junior ilipotupwa nje ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Amerika kusini, maarufu kama Copa America. Kwenye mashindano ya Copa America walitolewa na Uruguay katika hatua ya robo fainali ambapo bingwa alikuwa Argentina. Kama kuna timu ambayo inahcukia kufungwa na Brazil basi ni Argentina, hali kadhalika kama kuna timu inachukia kufungtwa na Argetina basi hiyo ni Brazil. Yaani upinzani wa timu hizi umechangia kuanzishwa kwa Dabi yao ya kila mwaka kupimana ubavu.
Wapenzi wa soka wa Amerika kusini wanatambua kuwa upinzani mkali kati ya Argetina na Brazil umevuka mipaka na wakati mwingine mchezo wao huambatana na matukio ya vurugu. Kutokana na ushindani huo, Brazil na Argentina ziliamua kuwapa raha wapenzi wao kwa kuwa na dabi yao kila mwaka ambapo hupangwa mahali pa kuchezwa sehemu mbalimbali.
Kimsingi dabi kati ya Brazil na Argentina imevuka mipaka ya burudani na sasa ni biashara kubwa ambayo inavutia wawekezaji mbalimbali wa kimataifa ambao wanataka kujitangaza pamoja na kupata faida za fedha kutokana na ukubwa wa nchi hizo kwenye ulimwengu wa soka.
Jumatano iliyopita Brazil ilipata kipigo kinawachoudhi mashabiki wengi ambao walianza kuimba nyimbo za kuwakashfu wachezaji na benchi la ufundi wakiamini mabao 4-1 ni kipigo kikubwa sana kwa hadhi ya nchi yao dhidi ya Argentina.
Brazil hawakukumbana na kipigo kikali tangu walipotandikwa mabao 7-1 na Ujerumani kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la dunia mwaka 2014 katika fainali ambazo walikuwa wenyeji. Hivyo basi kipigo hiki kimesababisha chama cha soka Brazil kumfukuza kazi kocha wao Dorival Junior.
Utamaduni wa Brazil kwa makocha
Tangu mwaka 2014 Brazil haijawahi kuvuka katika hatua ya robo fainali. Hivi sasa wanataka kumwajiri kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti. Hata hivyo kocha huyo hajawahi kufundisha timu ya Taifa, na endapo ataajiriwa atakuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuifundisha timu ya taifa ya Brazil. Nchi hiyo imenyakua mataji matano ya Dunia wakiwa na makocha wao wazawa. Kocha wa mwisho kutwaa taji hilo ni Luis Felipao Scolari mwaka 2002, na ndiye alifikisha nusu fainali mwaka 2014 katika awamu ya pili.
Hata hivyo msingi wa ukocha wa Brazil ni kufundishwa na wazawa. Falsafa hiyo imejengwa kwenye msingi wa kwamba wao wametwaa ubingwa mara tano bila kuajiri kocha wa kigeni. Kwahiyo wanaamini kuwa kocha wao ni mzawa. Endapo Carlo Acelotti ataajiriwa atakuwa wa kwanza wa kigeni. Chama cha soka cha Brazil kimekuwa na dhamira ya kumwajiri Ancelotti tangu mwaka 2023, na amekuwa akitazamwa kama kocha sahihi wa kurithi mikoba ya Dorival. Lakini Ancelotti hakujiunga na Brazil kama ilivyotarajiwa kwani hakuondolewa kwenye kiti chake kwenye klabu ya Real Madrid.
Ripoti zinabainisha kuwa Ancelotti mwenye mkataba na Real Madrid hadi mwaka 2026 anaweza kujiunga nao kama ataondolewa kwenye nafasi yake pale Santiago Bernabeu.
Uongozi uwanjani
Brazil ya sasa inakabiliwa na changamoto ya wachezaji viongozi ndani ya uwanja. Wengi wa wachezaji waliokuwa wakiitwa na Dorival Junior ni vijana ambao hawakuwa wameunganishwa na wakongwe. Neymar Junior ndiye mchezaji pekee ambaye anaonekana kuw aalama ya nchi hiyo na mwenye uwezo wa kubeba majukumu ya kuipaisha nchi yake kwenye mechi ngumu. Katika mchezo dhidi ya Aregntina Neymar Junior hakuwepo kikosini kwani anapambana kuimarisha utimamu wa miwli baada ya kuumia na hivyo kutakiwa kukaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja. Brazil wanakabiliwa na uhaba wa miamba ya soka ndani ya dimba huku wale waliopo wanaonekana kuwa “watoto wa kishua wa ulaya” ambao wamepungukiwa udambwidambwi wa Kibrazil au maarufu kama ‘O Jogo Bonito’ ama Samba.
Kama Simba na Yanga
Hakuna kitu kinachowaudhi mashabiki wa Yanga kama kufungwa na Simba. Hakuna kitu kinachowaudhi Simba kama kufungwa na Yanga. Unaweza kutafuta video za wachezjai wa Simba wakiangusha kilio baada ya timu yao kufungwa mabao 5-1 na Yanga. Si wachezaji pekee bali hata viongozi na mashabiki wao baadhi huwa wanazimia kabisa kutokana na kutoamini matokeo. Mechi nyingi za SImba na Yanga zimekuwa sababu za makocha kufukuzwa. Pande zote kwa nyakati tofauti zimefukuza makocha sababu ya kufungwa na Simba au Yanga. Kwahiyo Dorival Junior amefukuzwa kwa sababu ya kufungwa na Argentina, na hata Argentina wangefungwa tayari wangeanza chokochoko dhidi ya kocha wao bila kujali furaha aliyowatia Argetina kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 huko Qatar.
Comments
Loading…