KAMA kuna swali linasumbua vichwa vya waandishi na wachambuzi wa Michezo nchini Tanzania ni namna gani akili ya Walid Regragui inavyofikiria kuhusu Kundi F la AFOCN. Ni kundi linalojumuisha timu za Morocco,Tanzania, DRC na Zambia. Uchunguzi wa TANZANIASPORTS umebaini kuwa wakali kutoka Morocco ndiyo timi inayogopeka na kuibua maswali mengi. Akilini mwa kocha wa Morocco anafikiria nini kuhusu Taifa Stars? Anaionaje kuwa nayo katika kundi moja la AFCON? Ni namna gani Taifa Stars itakabiliana na Morocco kwenye AFCON?
Mastaa wa Morocco wanaitazamaje Taifa Stars? Katika mchezo wa soka kumekuwa na matukio au timu Fulani kuibuka na maajabu yake. Morocco ni miongoni mwa nchi zilizoibuka majaabu kwenye Fainali za Kombe la Dunia. Kwenye michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Taifa la Kiarabu, Qatar mamilioni ya washabiki wa soka walishangazwa na mafanikio ya Morocco ambayo ilitinga nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Sifa kubwa ya Morocco ilikuwa kutopoteza mchezo, na iliandika historia yake kwa kuwachapa Ureno waliokuwa na nyota wao hodari Cristiano Ronaldo. Ilikuwa kama haiwezekani kwa Morocco kuwafunga Ureno, lakini mamilioni ya mashabiki walishuhudia kitu cha aina yake. Wakati huo Morocco walikuwa wanaongozwa na kocha mtanashati, aliyevali suti safi nyeusi ya kimichezo, pamoja na raba nyeupe. Hapo unafikiria hivi Walid Regragui anaifikiriaje Tanzania?
TAIFA STARS WANA NINI?
Mara baada ya kukamilisha matangazo ya kundi F, bila shaka Walid Regragui alikuwa na taarifa nyingi kuhusu wachezaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pengine alimfikiria mshambuliaji wao anayetikisa viwanja vya soka Afrika, Fiston Mayele. Lakini akikumbuka nyota huyo alipata mafanikio akiwa na klabu ya Tanzania, Yanga. Hapo akili yake ifikirie kuhusu Taifa Stars. Kwanza Walid Regragui anafahamu anayo hazina kubwa ya wachezaji wa Morocco.
Wapo timu kubwa katika ligi za EPL, Uholanzi, Italia,Ufafaransa, Hispania, Saudi Arabia na kwingineko. Akigeuka upande mwingine ni DRC peke yake wanaweza kukaribi kumtikisa kwa sababu wanao wachezaji wengi nje ya nchi yao. Kwanza DRC ni mabingwa wa zamani wa AFCON, mwaka 1968 na 1974, lakini wamewahi kutinga fainali mara mbili pia mwaka 1998 na 2015. Vile vile DRC wameshiriki Kombe la Dunia mara moja.
DRC wana nyota Ufaransa,England,Ugiriki,Hispania na kwingineko. Ukigeukia Zambia nao wana wachezaji wengi barani ulaya, kuanzia England, Austria,Ufaransa,Saudi Arabia na kwingineko. Zambia ni mabingwa wa AFCON mwaka 2012. Lakini mwaka 1974 na 1994 ilifika fainali. Kwa haraka Walid Regragui atakuwa na habari chache kuhusu wanasoka wa Tanzania. Katika ligi za nje anaweza kupata habari chache kwa sababu kikosi cha Taifa Stars kina nyota 12 wa uhakika wanaoitwa kikosini. Hadi hapo unajikuta unashangaa Walid Regragui anaifikiriaje Taifa Stars? Anaionaje, kama timu isiyofahamika lakini anaongopa inaweza kufanya kama Morocco ilivyofanya kwenye Fainali za Kombe la Dunia?
ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA
Walid Regragui alikuwa uwanjani kuwatazama Simba walipomenyana na Wydad Casablanca. Alianza mwanzo wa mchezo hadi mwisho, na mara kadhaa kamera zilikuwa zikionesha alivyokuwa akizungumza na watu wake wa karibu. Sijui alikuwa anazungumziaje kikosi cha Simba. Sijui alikuwa anazungumziaje soka la Tanzania linavyozidi kunyanyuka na kutikisa vigogo. Sijui alikuwa anazungumziaje jinsi Wydad Casablanca walivyohaha kutafuta bao la kusawazisha na matokeo kumalizika dakika 90 ikiwa 1-0.
Hivyo ilimaanisha dakika 180 timu hizo zilitoka 1-1. Walid Regragui huenda alikuwa anawatazama wachezaji wake wa Morocco na kufanya tathmini ikiwa angeweza kumvutiwa na wachezaji hao ili awaite timu ya taifa. Kwa kuangalia baadhi ya nyota wa Tanzania Walid Gegragui anatuonaje? Maswali haya ndiyo yanapaswa kutukumbusha kuwa Morocco ni mlima wetu kwenye kundi F la AFCON. Hawa majirani zetu Zambia na DRC tunawamudu ikiwa tutakuwa na nidhamu na mipango.
Kufika hapo Walid Regragui atakuwa anawasaka nyota wengi wa Tanzania katika klabu za Afrika na Ulaya kuona uchezaji wao. Naye anakihofia kivuli alichokionesha wakati wa Fainali za Kombe la Dunia, ingawaje akilini mwake nina uhakika anakunywa kahawa kwa utulivu akiamini Tanzania haitamfanya chochote. Ila mpira unadunda.
Comments
Loading…