Kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia ziliandaliwa na nchi mbili ilikuwa mwaka 2002 wakati Japan na Korea kusini ziliposhirikiana kushinda uenyeji wa mashindano hayo.
BARA la Afrika liliweka rekodi ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2010. Fainali hizo zilifanyika nchini Afrika kusini mbele ya rais mstaafu Nelson Mandela. Afrika kusini ilipata nafasi hiyo baada ya kuikosa mwaka 2006, lakini pia ilizishinda nchi zingine ikiwemo wapinzani wao wa karibu bara la Afrika, Morocco. Sasa ni dhahiri rekodi nyingine huenda ikaandikwa kwa mabara ya Afrika na Ulaya kuandaa fainali za Kombe la Dunia. Kwanini? Soma uchambuzi huu.
Fainali zijazo za Kombe la Dunia mwaka 2026 zitaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Marekani,Canada na Mexico ambako timu 48 zitashiki kwenye mashindano hayo. Kwa mujibu wa shirikisho la soka duniani, FIFA fainali za mwaka 2926 zitakuwa kwanza kushirikisha timu 48 badala ya 32 iliyozoeleka.
Marekani iliwahi kuandaa fainali hizo peke yake mwaka 1994 ambako Brazil ikiwa na kapteni wake Carlos Dunga na wakali kama Romario Bebeto waliinyanaysa dunia kwa kulitwaa kombe hilo, huku Ronaldo De Lima akiwa kinda aliyeshuhudia kaka zake wakifanya mambo makubwa dimbani. Hali kadhalika Mexico imewahi kuandaa fainali hizo mara ya mwisho mwaka 1986 ambako Argentina waliabuka kuwa mabingwa.
Kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia ziliandaliwa na nchi mbili ilikuwa mwaka 2002 wakati Japan na Korea kusini ziliposhirikiana kushinda uenyeji wa mashindano hayo. Hivyo bara la Asia lilikuwa la kwanza kuonesha njia ya kuandaa fainali hizo. Na sasa inaonekana inawezekana nchi zaidi ya mbili zikaandaa fainali hizo.
FIFA ipo katika kibarua cha kuchagua nchi wenyeji wa fainali za Kombe la dunia mwaka 2030. Nchi tatu zimejitokeza kuwania nafasi ya kushirikiana kuwa wenyewe fainali hizo. Nchi hizo ni Morocco, Hispania na Ureno. Kwa maana hiyo ombi la uenyeji hapa linazihusu nchi tatu zilizoko. Morocco ni mwanachama wa Shirikisho la soka Afrika (CAF), wakati Ureno na Hispania ni wanachama wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA). Morocco iliingia katika mpango wa kuandaa fainali kwa pamoja ikichukua nafasi ya Ukraine kwa mtindo wan chi tatu kuwa wenyeji. Awali Ukraine ingeweza kushirikiana na Hispania na Ureno kusaka tiketi ya uenyeji wa fainali hizo.
Waziri wa michezo wa Morocco aliwahi kuviambia vyombo vya habari kuwa nchi hiyo ya Afrika kaskazini iliamua kuungana na Ureno na Hispania kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2030 jambo ambalo linatarajiwa kuunganisha nguvu na kuimarisha uhusiano kati ya mabara hayo mawili.
Katika mpango hupo, nchi nyingine zilizowasilisha ombi la kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2030 kwa ushirikiano ni Ugiriki, Saudi Arabia na Misri. Hii ina maana ombi hili la lpili nalo linahusisha mabara ya Afrika na Ulaya, pamoja na kuongezeka Asia (Saudi Arabia). Kwamba mpira wa miguu utawaunganisha watu bila kujali rangi,mipaka,utamaduni na uchumi. Ombi la tatu kwa FIFA la uenyeji wa ushirikiano linazihusu nchi za Uruguay,Argentina,Paraguay na Chile kwa mwaka 2030. Tofauti iliyopo ni kwamba kundi la mwisho la nchi mwombaji lina timu zinazotoka bara moja la Amerika kusini.
Kimichezo, ushirikiano wa Morocco,Ureno na Hispania unaleta ladha na ukweli kwamba mvuto wake unahusisha timu zenye mafanikio zaidi. Ingawaje Morocco na Ureno hazijawahi kutwaa kombe la hilo kama Hispania, lakini kimashindano ni timu iliyofanya vizuri zaidi kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka 2022.
Hii ina maana bara la Afrika litakuwa nan chi mbili zilizoomba uenyeji, Morocco na Misri. Hali hiyo inaonesha kuwa timu hizo pinzani kisoka zimedhamiria kuufanya mchezo huo kuunganisha jamii mbalimbali duniani bila kujali rangi na jiografia. Historia ya Misri kwenye kombe la dunia si nzuri sana kama Morocco lakini ni nchi kigogo wa soka barani Afrika.
Pengine hii ni tafsiri nyingine ya kuwa Afrika ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Ulaya au nchi kubwa kuliko kugeuzwa mtoto wa kulelewa. Morocco inatuma ujumbe kuwa CAF wanahitajika kuunganisha nguvu kuhakikisha wakati mwingine inayakumbusha mataifa ya Afrika kuungana yenyewe kusaka tiketi ya kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia miaka ijayo. Hilo linawezekana ikiwa uongozi utaamua kwa dhati kuhakikisha umoja katika nchi za Afrika unapewa kipaumbele kwenye uenyeji wa Kombe la dunia iwe kanda au namna yoyote inayowezekana.
Comments
Loading…