Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ipo tena, safari hii ikifanyika nchini Guinea ya Ikweta baada ya Morocco kusuasua kwa kuhofia athari za ugonjwa wa Ebola.
Mashindano haya yanakuja huku mabingwa watetezi, Nigeria, kwa aibu kubwa, wakiwa wamevuliwa ubingwa kwa kushindwa kufuzu.
Huu ni wakati wenye mvuto kwa washabiki na wadau wa soka wa Afrika, ambapo nyota kadhaa wanaokipiga Ligi Kuu ya England (EPL) wanachezea timu za nchi zao.
Guinea ya Ikweta walikuwa wenyeji wenza wa michuano hiyo 2012 waliposhirikiana na Gabon na waliokoa jahazi dakika za mwisho, bila shaka kutokana na utajiri wao mkubwa wa mafuta.
Wakati ule walitoa viwanja vinne lakini sasa watabeba mzigo wote wenyewe, na baadhi ya watu wanatilia shaka juu ya upatikanaji wa nafasi za kutosha kwa hoteli kwa ajili ya wachezaji, wajumbe na wageni wengine.
Mataifa yanaingia AFCON yakiwa na rekodi tofauti. Algeria walifanya vyema kwenye michuano ya Kombe la Dunia licha ya wachezaji wake kuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hata hivyo, tangu wakati huo, Cameroon waliovurunda hawajapata kupoteza mchezo wowote, hivyo wanatazama mbele kwa matumaini makubwa kwenye michuano hii.
Kuna wengine, kama Burkina Faso na Zambia wasiopewa nafasi sana lakini wanaweza kuteka fursa mpya hii na kufanya maajabu.
Michuano hii inaanza Januari 17 hadi Februari 8 mwaka huu, ambapo wenyeji watakuwa kwenye mechi ya wkanza dhidi ya Kongo.
Guinea ya Ikweta hawakuwa kwenye kundi la kushiriki michuano hii, lakini kwa sababu ya kujitolea uenyeji, wamepewa nafasi hiyo waliyokuwa wameikosa kwa kupokonywa pointi walipochezesha mchezaji ambaye hakuwa na sifa.
Haki za kurusha michuano hii zimepewa kwa kituo cha televisheni cha ITV4 watakaokuwa wakionesha moja kwa moja kila mchezo, na wengine wanaweza kufanya hivyo kwa kuchukua kwao kwa makubaliano maalumu.
Algeria waliofanya vyema zaidi kwenye Kombe la Dunia mwaka jana, wanaanza kuchuana na wababe wengine wa Afrika – Algeria wakatiSenegal wakikutana na vigogo wengine katika jina la Ghana.
Mabingwa wa 2012 ambao hawakupata kung’ara tangu hapo, Zambia watapepetana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wakali wanaoibukia, Cape Verde wanacheza na Tunisia, Gabon wakipimana ubavu na Burkina Faso.
Ivory Coast ya Yaya Toure (mchezaji bora wa Afrika) na kakaye Kolo watacheza dhidi ya Cameroon, huku Guinea wakipimana ubavu na Mali.
Kundi A lina timu za Guinea ya Ikweta, Kongo Brazzaville, Gabon, Burkina Faso.
Kwenye kundi B wapo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Cape Verde na Tunisia. Kundi C lina timu za Ghana, Senegal, Afrika Kusini na Algeria.
Kundi la mwisho linajumuisha timu za Ivory Coast, Guinea, Cameroon na Mali.
Ni wazi kwamba Cameroon watakuwa wanataka kurejea makali yao na kujionesha kwamba bado ni simba wasiofugika na kwamba kwenye Kombe la Dunia waliteleza tu.
Algeria wanapewa nafasi kubwa, wakiwa pia na mchezaji bora wa Afrika kwa kura za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Yacine Brahini; mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Islam Slimani na Nabil Bentaleb wa Tottenham Hotspur.
Huwezi kuwadharau Ivory Coast kwa sababu ya vipaji vyao vingi.
Comments
Loading…