HAYAWI hayawi sasa yamekuwa, Michuano ya 30 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanaanza Jumamosi hii, huku waandaaji, wachezaji na washabiki wakiwa na shauku ya kuona ustawi wa soka ya Afrika licha ya machungu yanayolikabili bara.
Ni Novemba mwaka jana tu Guinea ya Ikwete ilikubali ombi la ghafla la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuwa mwenyeji wa michuano hiyo, baada ya Morocco kujitoa, kwa kisingizio cha hofu ya ugonjwa hatari wa Ebola ulioyakumba mataifa matatu ya Afrika Magharibi.
Morocco walitaka michuano isogezwe mbele, ikiwa CAF bado waliwahitaji kuwa wenyeji, na CAF wakawakatalia, wakatafuta wenyeji wengine, ndipo Rais Teodoro Obiang Nguema wa Afrika ya Kati alipokutana na Rais wa CAF, Issa Hayatou na wakakubaliana dili.
Rais Nguema binafsi amelipia tiketi za baadhi ya washabiki kwa ajili ya kuhudhuria michuano hiyo mikubwa Afrika, inayofanyika kwenye nchi ndogo, yenye watu wachache, utajiri mkubwa wa mafuta ambao hata hivyo inasemwa unamilikiwa na watu wachache, zikiwamo familia za watawala.
Pamekuwapo na hofu juuu ya iwapo wageni wengi wanaofika watapata nafasi za kutosha, lakini pia juu ya watazamani kuwa wachache, kutokana na udogo wan chi lakini pia mwamko mdogo wa soka nchini humo.
Baadhi ya viwanja vipo katika maeneo ya pembezoni mwa nchi, ambapo baadhi ya wadau wamekuwa wakihoji iwapo kweli kuna miundombinu ya kufaa na kutosha. Wenyeji mara zote wamekuwa wakiwatoa wasiwasi, kwa kusema udogo wa taifa hilo si udogo wa fedha mfukoni na mtaji wa kuweka miundombinu inayotakiwa.
Taifa hili lenye watu 740,000 lilikuwa mwenyeji mwenza wa michuano kama hii 2012 pamoja na Gabon, lakini wasiwasi umetokana na kwamba sasa wameandaa wenyewe na kwa notisi ya miezi miwili hivi.
Mechi zitachezwa kwenye miji minne ya Bata na Malabo – kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita, lakini kuna miji mingine ya Mongomo na Ebebiyin. Viwanja katika miji hii miwili ya mwisho vinaweza visiwe vizuri sana, kutokana na mazingira halisi ya mashindano na notisi yenyewe.
Kwa mfano, uwanja wa Ebebiyin una uwezo wa kuchukua watu 5,000 tu. Hata hivyo, kwa eneo lenyewe, si ajabu hata watu hao 5,000 wa kuujaza wasipatikane, badala yake wengi wakafurahia mashindano kupitia seti zao za televisheni. Kuna mechi ambazo zilihudhuriwa na hata watu 200 mwaka 2012.
Yawezekana mwamko mdogo au umasikini wa watu vinachangia katika mahudhurio hafifu, na sasa kutoka mfukoni mwake mwenyewe, Rais Nguema amelipia watu 40,000 kuhudhuria mechi hizo.
“Tunatakiwa kununua tiketi ili kujaza viwanja. Tafadhali, wale wenye uwezo wawasaidie masikini,” anatoa rai Rais Nguema wakati akilipia hao 40,000.
Uwezo wa hoteli kwenye miji inayokuwa wenyeji kwa mara ya kwanza pia unaelezwa kuwa mdogo, ambapo imekuwa mshikemshike kwa wanahabari na washabiki kupata nafasi za kufaa, kwani kipaumbele kilipewa kwa wachezaji na maofisa wa timu na mashirikisho ya soka.
Tayari kocha wa Kongo, Claude Le Roy amelalamika juu ya ufinyu wa nafasi hotelini na pia maeneo ya jirani, ambapo alitaka nafasi tele kwa ajili yake na wachezaji kujinafasi.
Ama kuhusu uwezo wa timu yao, Guiney a Ikweta haipo vyema sana, kwani kwenye hatua za awali ilitolewa mapema kwa kumchezesha mchezaji ‘mamluki’, Thierry Fidieu Tazemeta aliyezaliwa nchini Cameroon. Ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Mauritania.
Kwa kosa hilo walienguliwa kwenye mashindano, lakini Rais Nguema aliponyoosha mkono na kuwaalika wakacheze Guinea, CAF wakawarudisha haraka kundini wana Guinea ya Ikweta wanaokwenda kwa jina la ‘National Thunder’, yaani ‘Radi ya Taifa’. Itakuwa tetemeko la dunia iwapo watakuwa wenyeji wa 12 kutwaa kombe hilo.
Wanaingia uwanjani huku kocha wao mpya kutoka Argentina, Esteban Becker, akiwa ameteuliwa siku 11 tu kabla ya kuanza mashindano hayo, hawajui wachezaji, hajui mazingira na pengine pia hajui timu pinzani.
Ebola imekuwa tishio kubwa kwa Waafrika na wageni kadhalika, kutokana na makali yake, ambapo tangu kuzuka kwake Machi 2014 imeua watu karibu 8,500 katika nchi sita, lakini zilizoathiriwa zaidi ni Liberia na Sierra Leone.
Guinea ya Ikweta ilichukua hatua madhubuti kuzuia Ebola kuingia kwao, ikiwa ni pamoja na serikali ya nchi hiyo kutumia fedha nyingi kuajiri madaktari wa Cuba kuweka program maalumu kuhakikisha kirusi hicho hakiingii kwenye ardhi yao. Wachezaji wote, kama ilivyo kwa wageni wote, wanaoingia Guinea wanapimwa kwanza hali yao ya afya.
Comments
Loading…