*Waingereza wasema wamefaidika kiuchumi
*Wengi waanza mazoezi, huduma zaboreshwa
Waingereza wameeleza kuridhishwa na matumizi ya pauni bilioni 8.77 kwa ajili ya kugharamia mashindano ya Olimpiki ya London 2012.
Utafiti uliofanywa na BBC unaonyesha kwamba zaidi ya theluthi ya wananchi wanaamini kwamba ilikuwa sahihi kutumia fedha hizo za walipa kodi kufanikisha mashindano hayo.
Nchi nyingi, hasa za Afrika, zimekuwa zikikwepa kuandaa mashindano mbalimbali, sababu mojawapo ikitolewa kuwa ni ukosefu wa fedha.
Hata hivyo, ikiwekwa mipango mizuri na wadau wengi kushirikishwa mapema, mashindano hutumika kama njia ya kufungua nchi kwa dunia na hatimaye kukuza uchumi kupitia biashara mbalimbali na utalii.
Uingereza, kwa mfano, iliyokuwa katika hali ngumu kiuchumi kabla ya mashindano hayo, ilikuja kupanda kidogo na kutoka kwenye myumbo, sababu moja ikielezwa ni mashindano hayo.
Asilimia 74 ya Waingereza wanasema kwamba wangependa mashindano hayo yafanyike tena nchini mwao, licha ya usumbufu wa hapa na pale uliotokea, kwa sababu wanaamini kuna faida katika kipindi kirefu.
Kwa upande mwingine, utafiti huo unaonyesha kwamba watu wamekuwa wakijishughulisha zaidi na mazoezi tangu waliposhuhudia michezo hiyo, ambapo asilimia 11 waliokuwa wakifanya mazoezi kabla imeongezeka hadi asilimia 24 kwa watu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 24.
Mashindano hayo makubwa pamoja na yale yaliyofuata ya paralimpiki yaligharimu mara tatu zaidi ya bajeti ya awali ya bilioni 2.4, wataalamu wa uchumi wakasema kwa mashindano hayo, uchumi ulipigwa jeki kwa pauni milioni 9.9 katika biashara na uwekezaji.
Utafiti huu umefanyika ikiwa ni mwaka mmoja tangu mashindano hayo makubwa yafanyike, lengo likiwa kuona umma uliyachukuliaje mashindano hayo na zipi athari zake kwa jamii.
Asilimia 32 wanasema mashindano yalikuwa na athari chanya kwao, asilimia 22 wanasema yamesaidia kukuza uchumi wao, wakati asilimia 21 wamesema mashindano hayo yamesababisha huduma za umma kuboreshwa.
Comments
Loading…