*Ziongezwe kutoka Afrika na Asia
Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michael Platini ametaka timu zitakazoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2018 ziwe 40.
Platini anasema ipo haya ya kuyaongezea mabara ya Afrika na Asia nafasi ili kuyatanua mashindano hayo makubwa zaidi badala ya kuikumbatia Ulaya.
Platini amekwenda mbali zaidi na kutaka timu za Ulaya zinazoshiriki mashindano hayo zipunguzwe, kwani kwa sasa bara hilo linatoa timu 13 kati ya 32 zinazoshiriki michuano hiyo.
Afrika inatoa timu tano tu wakati Asia ambalo ndilo bara lenye idadi kubwa zaidi ya watu ikitoa timu nne au tano kutegemeana na mchujo mmoja baina yao na Amerika Kusini.
Pendekezo hilo linaonesha uwezekano wa kutokea mabadiliko makubwa kwenye michuano inayoanzia 2018, kwani hata ile ya 2020 kuna kila dalili haitafanyika ama wakati au nchi ilikopangwa.
Michuano ya 2014 inafanyika Brazil na haitarajiwi kuwa na mabadiliko yoyote maana mambo mengi yamekamilika, lakini itakayofuata itakuwa na mambo mengi mapya.
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Seppp Blatter aliandika akisema Afrika na Asia zinahitaji uwakilishi mpana zaidi wa timu kwenye mashindano hayo, kwa kuzingatia kwamba zina mashirikisho mengi kuliko Ulaya na Amerika Kusini.
Hata hivyo, Blatter amekuwa madarakani tangu 1998 na hajaweza kuongezea mabara hayo timu zaidi ya hizo 10 au pungufu. Ulaya inaongoza kwa soka safi lakini, kwa vigezo vyovyote vile.
Platini – mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa anasema hesabu zake zinaonesha kwamba kuongeza timu nane hakutaathiri mengi, kwani mashindano yataongezewa siku tatu tu.
“Hili ni jambo zuri kwa kila mmoja, nakubaliana kabisa na Blatter kwamba tunahitaji timu zaidi kutoka Afrika na Asia, lakini badala ya kupunguza za Ulaya, tunaweza kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki na kuwa 40,” akasema Platini.
Comments
Loading…