in , , ,

Kulikoni Higuain anachelewa Arsenal?

*Mazungumzo yakwama…yaanza tena

*Chelsea wamchukua Marco van Ginkel

 

Mchakato wa Gonzalo Higuain kuhamia Arsenal unaelekea kucheleweshwa, kama si kukwama.
Mpachika mabao huyo wa Real Madrid alishajua kwamba kila kitu ni kamili kwake kuingia London kaskazini tangu wiki iliyopita, lakini ucheleweshaji unaofanyika unaonesha kwamba si ajabu dili zima likakwama.
Zilikuwapo ripoti wiki chache zilizopita kwamba klabu mbili hizo zilishakubaliana ada ya pauni milioni 22 na malipo binafsi wka mchezaji, kiasi kilichokadiriwa kufikia £130,000 kwa wiki.
Kitu pekee kilichokuwa kimebaki katika mpango huo wa uhamisho ilikuwa ni kukamilishwa kwanza kwa uteuzi na kuingia kwa kocha mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti wiki iliyopita.
Hilo lilikamilika, na ilitarajiwa kwamba uteuzi wake, kukubali na kuingia Santiago Bernabeu kungeharakisha mchakato wa Higuain kuondoka na kujiunga na kikosi cha Arsene Wenger.
Ilielezwa pia kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alishafanyiwa vipimo vya afya jijini Madrid, lakini washabiki wa Arsenal wakapigwa na butwaa wiki hii, waliposikia Jumatano wiki hii kwamba majadiliano yamekwama.
Wapinzani wakubwa wa Arsenal katika kumpata mchezaji huyo ambao ni Juventus ya Italia, wamefanikiwa kuwasajili Carlos Tevez na Fernando Llorente na kuacha watu hawajui wapi anakoelekea Higuain msimu ujao.
Higuain mwenyewe anaelezewa kuchanganyikiwa, kwa sababu haoni kwamba atakuwa na nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza cha Real Madrid msimu ujao, lakini pia angependa kuingia Ligi Kuu ya England (EPL).
Wachunguzi wa masuala ya soka wanasema si ajabu kuna klabu nyingine inayomtaka Higuain kwa siri, na pamekuwapo tetesi kwamba Monaco ya Ufaransa wanamhitaji, kama ilivyo kwa Inter Milan ya Italia.
Arsenal wenye kitita cha zaidi ya pauni milioni 70 wanatakiwa kuimarisha kikosi chao, ili kuweka hai matumaini ya kutwaa tena makombe, ambapo Higuain alishawapa matumaini makubwa.
Kigugumizi cha kumsajili Higuain kinawarejeshea uchungu washabiki wa Arsenal, kwa vile wanakumbuka jinsi wamepoteza fursa nyingi za kunasa nyota katika miaka iliyopita, yote akilaumiwa kocha Wenger kwa ubahili.
Wapinzani wao tayari wamenasa wachezaji wazuri, kama Manchester City waliowasajili Fernandinho na Jesus Navas wakati Andre Schurrle anakamilisha mchakato wa kwenda Chelsea. Liverpool nao wamesajili wachezaji kadhaa, na walipata kuhusishwa na Higuain pia.
Hata hivyo, habari zilizopatikana asubuhi ya Alhamisi hii, zinasema kwamba Real Madrid wamewapa Arsenal ruhusa ya kuzungumza na Arsenal juu ya usajili huo.
Baba yake, Jorge ambaye pia ni wakala wake anasema anaiona safari ya mwanawe EPL ikielekea kwenye mchakato mzuri. Vyanzo vya habari vinasema kwamba kuna dalili mkwamo wa awali baina ya klabu hizo umelainishwa na mambo yanakwenda.
Real Madrid wanadaiwa kutaka malipo ya euro milioni 25 wakati Arsenal wanadai wapo tayari kutoa euro milioni 20 tu, japokuwa inaelekea wamejadiliana na kufikia makubaliano ya kiwango cha kulipa.

Jorge Higuain amenukuliwa Alhamisi hii akisema: “Tumepewa ruhusa na Real Madrid kuzungumza na Arsenal…nadhani hii ni bahati na sasa nitamwona mwanangu akiingia EPL hivi karibuni.”
Zipo habari kwamba Higuain ataingia England mwishoni mwa wiki hii kukamilisha usajili wake, lakini baba yake anasisitiza kwamba hawajakubaliano chochote na Arsenal kuhusu malipo binafsi.
“Hakuna chochote hadi sasa kilichosainiwa, lakini mazungumzo yamefika mahali pazuri sana…hatujazungumzia mkataba bado, Arsenal wametoa ofa kubwa, kama walivyofanya Juventus,” anasema Jorge Higuain.
ARSENAL WAUZA KIPA, LIVERPOOL WAMTWAA MIGNOLET
Katika hatua nyingine, golikipa namba tatu wa Arsenal, Mtaliano Vito Manonne amehama na kujiunga na Sunderland kwa mkataba wa miaka miwili na ada ya uhamisho ya pauni milioni mbili.
Anaondoka wakati magolikipa Wojiech Szczesny na Lukasz Fabianski wakisubiri changamoto ya kupata namba, baada ya mazungumzo ya Arsenal na kipa namba moja wa Brazil, Julio Cesar kufikia mahali pazuri, kumsajili kutoka Queen Park Rangers (QPR).
Liverpool walimsajili kipa namba moja wa Sunderland, Simon Mignolet katika kujiimarisha, na hiyo ni changamoto kwa kipa wao namba moja, Pepe Reina, ambaye hata hivyo amekuwa akihusishwa na kurudi kwao Hispania kuchezea Barcelona, kwani Victor Valdes ataondoka mkataba wake ukiisha mwakani, au hata kabla. Liverpool wameimarisha beki yao kwa kumchukua Kolo Toure kutoka Manchester City.
Jonjo Shelvey (21) wa Liverpool amenyakuliwa na Swansea City kwa pauni milioni tano kwa mkataba wa miaka minne. Kiungo huyo alipata kutumiwa kama mshambuliaji na Brendan Rodgers pale Liverpool walipokuwa na uhaba wa washambuliaji, wakiwa na Luis Suarez pekee.
Habari nyingine ambazo si rasmi, zinagusia kwamba kuna uwezekano kwa Suarez kujiunga Arsenal, japokuwa alipata kusema kwamba anataka kuondoka nchini England moja kwa moja, kwani vyombo vya habari havimpendi na Chama cha Soka kinamuonea.
Chelsea nao wamefikia makubaliano na klabu ya Vitesse Arnhem kwa ajili ya kumsajili kiungo wa Uholanzi, Marco van Ginkel.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Hatimaye Serikali yakabidhiwa rasmi Uwanja wa Taifa

Tanzania Yaenda Urusi kwa Riadha Dunia