in , , , ,

Abou Diaby: Jembe lililovunjika mpini

Mfululizo wa matukio ya kuumizwa au kuumia kiungo mahiri wa Arsenal, Vassiriki Abou Diaby yanazua utata juu ya hatima yake kisoka. Washika Bunduki wa London walifurahi msimu huu ulipoanza, baada ya kuona Diaby (26) aliyekaa nje muda mrefu kwa majeraha alikuwa anarejea.
Lakini amecheza mechi chache na sasa habari kwamba atakuwa nje kwa miezi tisa baada ya kuumia goti akiwa mazoezini, zinakatisha tamaa.
Hata kabla hajaumia, alikuwa akipigiwa hesabu iwapo angecheza mechi baada ya Ligi Kuu ya England (EPL) kusimama kwa wiki mbili, maana alikuwa majeruhi tena.
Wapo wadau walioanza kusema kama hali yake ingetengamaa, ni vyema akauzwa msimu huu ukimalizika, ili Arsenal wahesabu kwamba hayupo nao tena.
Lakini wakati akijiweka fiti kutetea timu yake iingie kwenye nne bora, ameumia tena, atafanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni na kama ni kurudi uwanjani ni mwaka kesho.
Nakumbuka miaka miwili iliyopita, katika mechi dhidi ya Liverpool, Mfaransa huyo aliingia uwanjani dakika ya 53 baada ya Jordan Henderson kumuumiza kiungo mwingine Mikel Arteta aliyepelekwa hospitali.
Jamaa mmoja aling’aka kwa nini Diaby ameingia, kwa sababu naye ni majeruhi na kama sivyo ni majeruhi mtarajiwa. Alicheza vizuri sana kwa dakika chache, lakini ilipotinga dakika ya 80 alitoka nje akichechemea baada ya kuumia, nafasi yake ikachukuliwa na Alex Oxlade-Chamberlain.
Ukweli ni kwamba Diaby amekuwa mtiifu, mwenye kujituma kwa Arsenal tangu ajiunge 2006 akitoka Auxerre, na ni mmoja wa wachezaji waandamizi na tegemeo.
Alipoumia mwaka jana, wadau kadhaa walisema hangerudi tena dimbani, lakini kama alivyofanya miaka iliyopita, hupona na kurudi, kabla ya kuumia tena na kuuguzwa hadi apone.
Nakumbuka awali kabisa aliumizwa vibaya na Dan Smith wakati Arsenal wakiwapopoa Sunderland mabao 3-0.
Diaby alikuwa kwenye eneo la hatari, tena dakika ya 90, Smith akamjia kama treni na kumvunja mguu. Mwamuzi Dermot Gallagher akampa Smith kadi ya njano, washabiki wa Arsenal wakapiga mayowe kumlaani Smith.
Diaby alipona mguu aliovunjwa, akarudi tena uwanjani, lakini kila arudipo, amekuwa akiumizwa, na waliomfanya asicheze vyema mpira wake kwa kumjeruhi baada ya hapo ni Joey Barton, Michael Essien na Paul Robinson, na wagumu wengine wengi kwenye EPL.
Umekuwa mzunguko huo huo, wa kuumizwa, kuwa nje na kutibiwa na kupona, kurejea uwanjani na kuumizwa tena.
Mwaka huu alikuwa Liberty Stadium, dimba la Swansea kule Wales, Arsenal walikokuwa wakitafuta pointi muhimu, na huko jamaa mmoja alikuwa akipiga kelele kutoka jukwaani, eti akisema ana wasiwasi Diaby atavunjika mguu. Sasa kavunjika kweli mguu, miezi tisa nje!
Lakini Diaby amekuwa akiumizwa akicheza ili Arsenal washinde, hajavunjika mguu kwenye pati ya Noeli au ulevi wala kwenye kukabiliana vibaya na wapinzani wake uwanjani, hivyo hastahili kulaumiwa.
Ni muhimu kuona kwamba waamuzi na EPL wanawalinda wachezaji, vinginevyo kuna akina Jack Wilshere nao wameanza tena kurejea majeraha mara kwa mara.
Yote hayo ndio ukweli, lakini tukirudi kwenye soka na kinachotakiwa kufanywa, ni wazi kwamba nafasi yake sasa lazima ijazwe.
Aliyekuwa na wazo la kumuuza awali hakukosea, maana wapo waliosema hivyo kwa Robin van Persie, mhanga mwingine wa majeruhi, ambaye ni msimu uliopita na huu tu amekuwa fiti muda mwingi, japokuwa sasa amesita kufunga mabao.
Pamoja na ubinadamu, upendo na kujali alivyo navyo kocha Arsene Wenger na wakuu wengine wa Arsenal, ni wazi kwamba Diaby unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wake.
Katika umri wa miaka 26 bado ana nguvu, akili na ujuzi, lakini mwili ukishakuwa katika silika ya kuumizwa kila mara na kuwa nje ya soka, ni vigumu kubaki na soka imara mguuni.
Diaby ametoa kila kitu kwa ajili ya Arsenal, ndiyo maana ni vigumu kwa klabu kuachana naye
Ni msimu wa 2009-10 tu ambao Diaby alikuwa mzima kwa muda mrefu. Baada ya kucheza jumla ya mechi 39 za EPL katika misimu yake mitatu Arsenal, Diaby alicheza nne msimu uliopita akianzia benchi na 11 tu msimu huu.
Ingawa hivyo, Diaby amebaki tegemeo, ndiyo maana alionesha vitu adimu mwanzoni walipocheza na Liverpool, kisha Stoke. Aliingia Arsenal lengo likiwa kuziba pengo la Patrick Vieira, na ana sifa kama zake, lakini ndio amekuwa kama jembe lililovunjika mpini.
Iwapo wangemuuuza, Arsenal wangepata kitita kizuri, ambacho kingeongezwa na zaidi ya pauni milioni 70 zinazotengwa kununua nyota wapya. Lakini sasa, unauzaje mgonjwa? Unauzaje mchezaji aliyevunjika mguu? Diaby atabaki kuwa wa Arsenal tu, hata baada ya msimu huu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Manchester United safi ukuzaji vipaji

Ipo haja ya kuimarisha (Kufufua): Umitashumta, Umiseta, Shimivuta..