*Barcelona waongoza barani Ulaya
*Klabu za Ufaransa nazo zajivunia
Manchester United ni miongoni mwa klabu zinazowika zaidi England kwa kuzalisha chipukizi bora wanaotamba kwenye soka barani Ulaya.
Man United wanaounyemelea ubingwa wa England walioupoteza mwaka jana, wana jumla ya wachezaji 24 wanaotamba katika ligi tano za madaraja ya juu kabisa barani.
Kadhalika, United wanaofundishwa na Alex Ferguson tangu mwaka 1986 wana nyota tisa katika kikosi kinachoshiriki Ligi Kuu ya England (EPL), walioanzia kwenye shule yao.
Hao wanatofautiana kwa umri na uzoefu, kutoka Ryan Giggs hadi Danny Welbeck na Tom Cleverly walio na kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, klabu inayotoa nafasi kwa chipukizi zaidi katika timu yao kwa sasa ni Athletic Bilbao, yenye wachezaji 16 waliokaa klabuni hapo kwa walau miaka mitatu wakiwa na kati ya umri wa miaka 15 na 21.
Bilbao wanatambulika kwa wingi wa wachezaji kutka eneo la Basque na sera yao ya ‘Cantera’.
Barcelona wanafuatia, wakitamba na shule yao ya mafunzo maarufu kwa jina la ‘La Masia’ iliyozalisha wachezaji 14 wanaochezea timu ya wakubwa.
Hao ni pamoja na Xavi, Andres Iniesta na Lionel Messi wakati Real Sociedad (kutoka eneo la Basque pia) wakiwa na idadi hiyo hiyo ya wachezaji waliokuzwa, lakini wenyewe ni katika jimbo la Guipuscoa.
Manchester United ndiyo klabu pekee ya Uingereza miongoni 10 bora katika kukuza vipaji, ikiungana pia na klabu za Ufaransa – Montepellier, Sochaux-Montpeliard, Lyon na Bordeaux, wakionesha umahiri wao katika kukuza vipaji.
Klabu hii ya Ferguson inajivunia rekodi ya nne bora zaidi miongoni mwa klabu katika ligi tano bora za Ulaya – Premier League, La Liga, Serie A, Bundesliga na Ligue 1.
Inaheshimika kwa jinsi inavyokuza wachezaji na kuwawezesha kubaki kwenye klabu yao, au kupata ajira kwenye ligi nyingine bora barani Ulaya.
Wanaoongoza njia katika ukuzaji vipaji barani Ulaya ni Barcelona wenye wachezaji 38 waliozalishwa na La Masia wanaotamba kwenye ligi bora barani Ulaya.
Lyon ya Ufaransa inao 32 wakati Real Madrid inatambia wachezaji wake 29.
Unyakuaji wa wachezaji kutoka Bernabeu unazidi kuinyima Real Madrid vipaji vyake, ambapo waliosajiliwa kutoka hapo ni pamoja na kiungo wa Chelsea, Juan Mata, Javi Garcia wa Manchester City na mshambuliaji wa Sevilla, Alvaro Negredo waliotokana na kituo cha mafunzo cha Castilla cha Real Madrid.
Pamoja na simulizi za siku nyingi juu ya Arsenal na kocha wao, Arsene Wenger kuwa maarufu kwa kukuza vipaji, wanao wachezaji sita tu waliotengenezwa hapo, lakini wengine 14 waliruhusiwa kujiunga na mahasimu wa klabu kwenye ligi mbalimbali Ulaya.
Comments
Loading…