*Chelsea wapigwa, Manchester City wabanwa
*Man U waibuka, Liverpool wapewa mwanya
Ilikuwa Jumamosi yenye matokeo yaliyoshangaza wengi, yakienda kinyume na matarajio ambapo matumaini ya ubingwa bado yamesambaa kwa timu kadhaa.
Chelsea walipigwa na timu dhaifu ya Crystal Palace kwa bao 1-0 kwenye mechi ambayo vijana wa Jose Mourinho walitarajiwa kuchanga vyema karata zao na kuendelea kupaa juu ya msimamo wa ligi, lakini walishindwa kabisa kuwakabili vijana wa Tony Pulis.
Baada ya matokeo hayo yaliyowadhoofisha Chelsea kiasi cha wachezaji kujigaragaza uwanjani wakiwa na masikitiko huku wakipozwa na kocha wao, Mourinho alidai kwamba kipigo hicho kimefifisha matumaini yao ya kutwaa ubingwa msimu huu. Matokeo hayo mabaya kwa Mreno huyo yanakuja siku chache tu baada ya kuwateketeza Arsenal 6-0.
Manchester City nao wanaoaminika kwa uwezo mkubwa wa kufunga mabao mengi na ambao iwapo wangeshinda mechi yao ya usiku wangekuwa wanaongoza ligi, walibanwa na Arsenal. Ni man City hawa hawa waliokwenda kwenye ngome ya Old Trafford na kuwafumua Manchester United 3-0 mchezo uliopita.
Lakini Jumamosi hii, katika dimba la Arsenal waliochukuliwa kuwa dhaifu baada ya mchezo uliopita kwenda sare na Swansea hapo hapo Emirates, Man City walibanwa vilivyo na Arsenal walioonesha dhamira ya dhati kulinda heshima yao na kufufua matumaini ya kupigania nafasi ya kwanza siku zijazo.
Hata hivyo, David Silva alitangulia kuwapatia City bao dakika ya 18 tu na kuwatia hofu washabiki wa The Gunners, lakini walizidi kuwashangilia na dakika ya 53, Mathieu Flamini akamtungua kipa Joe Hart kwa kuandika bao la kusawazisha.
City wangeweza kuondoka na kipigo, kama si kipa Hart kuokoa kwa mguu mchomo wa Lukas Podolski uliokuwa ukielekea wavuni, ambapo dakika za mwisho City walionekana pia kuchoka. Kocha wao, Manuel Pellegrini alisema kwamba bado Arsenal wapo kwenye mbio za ubingwa.
Wakati baadhi ya washabiki wakitaka David Moyes afukuzwe Manchester United, na ndege iliyotoa ujumbe ‘The Wrong One – Moyes Out’ ikipingana na jinsi anavyoitwa hapo ‘The Chosen One’, Man U walitoka nyuma kwa bao moja walilokuwa wamefungwa na Aston Villa, wakasawazisha na kuongeza mengine matatu na kumpatia faraja kocha wao.
Kwa matokeo hayo, Liverpool ambao Jumapili hii wanacheza na Tottenham Hotspur watakuwa na nafasi ya kuongoza ligi hata kwa kupata sare tu, hasa ikizingatiwa watakuwa uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.
Matokeo mengine jana yalishuhudia Southampton wakiwakandika Newcastle 4-0, Stoke wakishinda dhidi ya Hull kwa 1-0, Swansea wakiwabomoa Norwich 3-0 na West Bromwich Albion wakienda sare ya 3-3 na Cardiff. Everton leo watakuwa wageni wa Fulham.
Chelsea wanaongoza ligi kwa pointi 69 baada ya michezo 32, Liverpool wanafuata kwa pointi 68 kwa michezo 31, Man City pointi 67 baada ya mechi 30, Arsenal Β pointi 64 wakiwa wameshacheza mechi 32, Everton mechi zao ni 30 na wamekusanya pointi 57 wakati Spurs wana pointi 56 kutokana na mechi 31.
Comments
Loading…