*Shabiki apiga 999 polisi kulalamikia kadi
*Man U kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu
Wakati Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) likisema halina tatizo na kadi nyekundu aliyopewa Luís Carlos Almeida da Cunha ‘Nani’ wa Manchester United, shabiki ameripoti tukio hilo polisi.
Uefa wamesema katika taarifa yao kwamba hawana tatizo lolote na refarii Cuneyt Cakir wa Uturuki aliyemtoa nje Nani katika mechi dhidi ya Real Madrid Jumanne hii.
Nani alimpiga kwa daluga mbavuni mchezaji wa Real, Alvaro Arbeloa dakika ya 56, aliyelazimika kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Luka Modrik aliyesawazisha bao, kwani United walikuwa wakiongoza 1-0.
Polisi wameonya watu kutopoteza muda wao, kwani shabiki wa Man U alipiga simu ya 999 Polisi kulalamika juu ya mchezaji wao Nani kupewa kadi nyekundu.
Kijana mwenye umri wa miaka 18 wa Nottinghamshire aliona kadi hiyo ilikuwa jinai, hivyo akawataarifu polisi kama wangeweza kuchukua hatua yoyote, lakini baadaye aliomba radhi, akasema alifadhaishwa na hali hiyo.
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Cristiano Ronaldo alikomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mashetani Wekundu hao kwa kufunga bao la pili na kuwatupa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha Alex Ferguson alionesha kukasirishwa tangu uwanjani, akalalamika wazi wazi na baada ya mechi alikataa kuhudhuria vikao vilivyopangwa kwa mujibu wa kanuni za Uefa.
Kwa kadi hiyo nyekundu na ukwepaji wajibu wa United, Uefa wameanza uchunguzi rasmi dhidi yao, kwa upande mmoja United wakionekana kutotekeleza wajibu wao kwa vyombo vya habari baada ya mechi.
Kwa upande wa kadi nyekundu ya Nani, Uefa wataangalia iwapo akose mechi moja au kuna haja ya kuongeza adhabu, kulingana na ukubwa wa kosa alilotiwa nalo hatiani na mwamuzi.
Real Madrid wanaofundishwa na Jose Mourinho ‘The Onlu One’ wamewatoa United kwa jumla ya mabao 3-2.
Mourinho alisema timu bora ilitolewa, akimaanisha United, jambo linalotafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kwamba anatafuta nafasi ya ukocha Old Trafford kwa kujidai kuwahurumia.
Ferguson hakutokea kwa mahojiano baada ya mechi, badala yake alikuwapo msaidizi wake, Mike Phelan, aliyesema bosi wake alikuwa amekasirishwa mno hivyo hangeweza kuzungumza.
Ferguson anaweza kukumbana na rungu la Uefa kwa kuwatoroka wanahabari, lakini anaweza kuwa amelinganisha adhabu ipi kwake inaweza kuwa kubwa.
Iwapo angetokea na kumshambulia mwamuzi moja kwa moja kwa maneno yake, angeweza kukumbana na faini kubwa kuliko kukacha kutokea.
Wachambuzi mbalimbali wameeleza kutoridhishwa na kadi nyekundu dhidi ya Nani, kwa madai hakufanya hivyo kwa makusudi.
Hata hivyo, mchambuzi wa michezo wa televisheni ya ITV, Roy Keane, alisema kadi hiyo ni sahihi, kwani Nani alimpa nafasi mwamuzi kuamua hivyo, kwani alijua hakuwa mwenyewe uwanjani au eneo lile kiasi cha kunyanyua daluga na kulisukuma juu kiasi hicho kuwania mpira.
Hata hivyo, Keane aliondoka United kwa kutoelewana na uongozi wa klabu, kabla mkataba wake kumalizika, baada ya kuwachagiza wachezaji wenzake kwa kucheza hovyo wakati fulani na kuzidiwa na timu ‘ndogo’.
Kadhalika wachezaji wa Man U hawakusimama kuzungumza kwenye eneo ambalo ni utaratibu kufanya hivyo. Rio Ferdinand alimwendea mwamuzi na kupiga makofi mbele ya uso wake, kana kwamba alikuwa akishangilia.
“Hatuna tatizo lolote na mwamuzi Cakir, hakuna lolote la ajabu kwetu kuhusiana na kutolewa nje kwa mchezaji huyo. Tunasubiri taarifa rasmi za mechi kama ilivyo kawaida,” msemaji wa Uefa alisema.
Pamekuwapo hisia kwamba United hupendelewa na baadhi ya waamuzi kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Hata hivyo, Nani si mchezaji wa kwanza kupewa kadi nyekundu kwenye historia ya michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wengine waliopata kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na mchezo mbaya ni Rafael Da Silva, Paul Scholes na Nicky Butt.
Comments
Loading…