Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kimeweka bayana kwamba, kimesitisha ushirikiano wa aina yoyote na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hadi hapo kisiwa hicho kitakapotambuliwa na kupewa haki za msingi.
Kauli hiyo imetolewa mjini Zanzibar na Msemaji wa ZFA, Maulid Hamad Maulid alipozungumza na waandishi wa habari.
Akifafanua zaidi kuhusu kauli yake hiyo, Maulid alisema kwamba kwa zaidi ya miaka 40 sasa Zanzibar inawakilishwa kimataifa na iliyokuwa FAT na sasa TFF, lakini haifaidiki na mambo mbalimbali ya msingi ya kuendeleza soka nchini.
”Wenzetu wamejisahau na kufanya mambo ya maamuzi ya uwakilishi bila ya ridhaa yetu, tunaamini uongozi huu wa TFF unafahamu ndani ya Tanznaia kuna vyama viwili vya soka vyenye haki sawa ya kuendesha soka, lakini ni wakaidi kutekeleza tunayokubaliana,” alisema.
Aliongeza kusema kwamba, TFF wanachofanya sasa ni kukwepa kukutana na ZFA na hata inapotokea wakipanga kukutana wamekuwa wa kwanza kuahirisha bila ya kuwepo sababu za msingi.
Alisema kwamba mara zote wanafikia makubaliano na TFF kuhusu mambo ya msingi, lakini linapokuja suala la utekelezaji TFF wamekuwa wagumu.
Ameyataja miongoni mwa mambo waliyokubaliana na ambayo TFF haitaki kuyatekeleza ni pamoja na kupatiwa kiasi cha misaada kutoka FIFA na CAF na zaidi dola 250,000 (zaidi ya sh milioni 250) ambazo TFF imekuwa ikipatiwa kila mwaka kutoka FIFA.
Maulid alitolea mfano wa mradi maalum wa `Goal Project’ unaofadhiliwa na FIFA ambao umetumika kujenga hosteli ya timu ya Taifa pamoja na fedha nyingine zilizotumika kuweka nyasi na kuhoji vipi nafasi ya ZFA katika mgao huo.
”FIFA wanapotuma misaada ya aina hiyo wanatuma kwa jina la Tanzania na si Tanzania Bara, tunashindwa kuelewa ni kwa nini wenzetu wanatutenga katika hilo wakati wanatambua kwamba ZFA inawakilishwa FIFA kwa mwamvuli wa TFF,” alisema.
Alidai kwamba, awali walitarajia mabadiliko makubwa baada ya uongozi wa Leodegar Tenga kuingia madarakani.
“Lakini siku tunashangaa siku zinavyokwenda mabadiliko yanayofanywa si katika kiwango tulichokitarajia,” alisema na `kuuma na kupuliza’ akidai bado wana imani na Tenga, ingawa kuna wanaomzunguka na kumpotosha kwa maslahi yao.
Kutokana na hali hiyo, alisema ZFA imeamua kuwaandikia barua mawaziri wanaohusika na michezo wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na mabaraza yote mawili yanayohusika na usimamizi wa michezo kuelezea kilio chake.
Nadhani Zanziba wana point! Ni vizuri serikali ya muungano ikaliangalia hili suala kwa ukaribu san, vinginevyo ni aibu tupu kwa Taifa letu.
Katika kipindi hiki ambacho watanzania wengi wameamka ki michezo hasa mchezo wa mpira wa miguu, ni ukweli ulio wazi kwamba vyama vya mpira nchini vipunguze au kuacha kabisa tabia ya ubabaishaji ktk uongozi. Sisi wadau tunachukizwasana na migogoro ya kila siku kwani ni aibu kwa Taifa lenye jina zuri kama tanzania.Tuanze kuweka mikakati bora tangu vilabuni mpaka ngazi ya ligi kuu hatiamaye timu ya Taifa na vyama vyote vya mpira. ZFA na TFF kaeni chini myamalize acheni siasa ktk mpira tumechoshwa na malumbano ya kila siku.