Michuano ya CECAFA inaendelea kwa kuzikutanisha timu za taifa za wakubwa za nchi wanachama na nchi waalikwa kutoka kanda tofauti na ukanda ukanda huu wa CECAFA.
Michuano ambayo inahistoria kubwa sana katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla.
Ndiyo mashindano yenye umri mrefu, kitu ambacho ndicho tumebaki kujivunia nacho.
Neno “Ubora” tumelisahau sana kwenye michuano hii na kulitazama neno “Ukongwe” zaidi.
Ndiyo maana sitosita kusema ni moja ya michuano ambayo inakutanisha asilimia kubwa ya timu ambazo ni dhaifu, timu ambazo misingi ya soka ya nchi zao ni mibovu.
Ndiyo maana ukanda huu unabaki kuwa ukanda ambao uko nyuma kwenye maendeleo ya soka kila siku.
Sijambo la kushangaza kwa sababu nchi wanachama nyingi zimeweka kando misingi imara ya kuimarisha mpira wetu.
Hata nchi ambazo tunazialika kwenye michuano hii zinaleta vikosi dhaifu.
Tuliwahi kushuhudia Ivory Cost ikileta kikosi cha wachezaji waliochini ya umri wa miaka 20.
Kikosi ambacho wachezaji wake wanatafuta nafasi ya kuingia kwenye soka la ushindani.
Michuano hii hutumiwa na nchi nyingi kama sehemu ya kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawana nafasi kubwa sana katika vikosi vya kwanza vya timu ya taifa.
Hili linafanya pia michuano hii kuonekana haina ushindani mkubwa.
Unapoisifia timu inayofanya vizuri kwenye michuano hii ambayo haina ushindani mkubwa ni sawa na kuipumbaza kitu ambacho kitaifanya isahau vitu vya msingi ambavyo inatakiwa kufanya.
Huu siyo wakati wa kuisifu Zanzibar, ila ni wakati wa kuielekeza na kuikumbusha Zanzibar wapi wanatakiwa kufanya kipi.
Msimu jana timu zake mbili Zimamoto na KVZ zilitolewa awali kabisa katika michuano ya vilabu vya Afrika.
Zimamoto ilifanikiwa kushinda goli 2-1 kwa moja kwenye uwanja wa Amaan dhidi ya Ferroviaro de Beira ya Msumbiji
Walipoenda Msumbiji walifungwa goli 3-1, wakati KVZ ikitolewa na Messager Ngozi ya Burundi kwa kufungwa magoli 3-0 mjini Bujumbura , na kwenye uwanja wa Amaan KVZ wakashinda 2-1.
Hadithi za vilabu vya Zanzibar kutolewa awali katika michuano ya CAF haijaanza msimu jana tu, hata msimu juzi pia timu zake za KMKM na Polisi zilitolewa mapema.
Hadithi hii mara nyingine huja na matokeo ya kutisha kwa timu za Zanzibar kufungwa goli 7-0.
Hiki ni kitu cha kawaida sana kwa vilabu vya Zanzibar, ukawaida huu ZFA hawauoni kwa kiasi kikubwa na watabaki kila siku kufurahia pongezi za kuwaangamiza kisa wamewafunga Tanzania bara.
Ni wakati wa ZFA kukaa chini na kuja na mikakati ya kusimamisha ligi ambayo ina nguvu na yenye ushindani.
Tunaona kila uchwao vilabu vya Zanzibar vikishindwa kuvuka hatua ya awali ya mashindano ya CAF kwa sababu ligi yao dhaifu haitoi wawakilishi imara.
Na hii ndiyo sehemu ambayo ZFA inatakiwa ianze nayo na kuzipuuzia pongezi za CECAFA ambazo hazina faida.
Waiendeshe ligi yao katika misingi ya kibiashara ili wadhamini waje wawekeze pesa kwenye ligi.
Timu zipate fedha za kujikimu ili zitoe ushindani kwenye ligi, ushindani ambao utapelekea kutoa timu ambazo imara na kuiwakilisha vyema Zanzibar.
Zanzibar wakifanikiwa kutengeneza ligi imara ndipo hapo na mimi nitashawishika kuyapiga makofi yangu kuwapongeza.
Ila siwezi kuwapongeza kwa timu yao ya taifa kufanya vizuri kwenye michuano dhaifu ya CECAFA.