Kocha mkuu wa Young Africans Mwinyi Zahera ametoa visingizio baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya kombe la shirikisho la soka barani Afrika CAF, dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda walioibuka na ushindi wa 1-0 kwenye uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali juzi jioni.
Zahera ambaye bado hajapata nafasi ya kukaa kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo kufuatia vibali vyake vya kufanyika kazi kuendelea kushughulikuwa na viongozi wa Young Africans, amesema mchezo huo dhidi ya Rayon Sports ulitawaliwa na mambo mengi ambayo yalikua kinyume na taratibu za mchezi wa soka, huku akiwahusisha waamuzi kwa kusema walichangia.
Kocha huyo kutoka Jamuhuri ya Kidekrasia ya Kongo ameongeza kuwa, pamoja na kupoteza mchezo, bado kikosi chake kilionesha soka la ushindani na kuonyesha umahiri wa kupambana katika uwanja wa ugenini kwa dakika zote 90.
“Uwanja ulikuwa mbaya, tulikuwa tunacheza na wachezaji 14, Kumi na moja uwanjani na wengine watatu nje ya uwanja pembeni walifanya mambo ya hovyo sana, mambo hayakuwa mazuri ila nawashukuru wachezaji wangu walicheza vizuri sana kutokana na program yetu ambayo tulianza nayo toka Morogoro,” Zahera amesema.
Yanga imemaliza michezo ya hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika CAF, ikiwa inaburuza mkiwa wa kundi D kwa kupata alama 4, ikitanguliwa na Gor Mahia ya Kenya yenye alama 8 huku Rayon Sports wenye alama 9 na USM Algers wenye alama 11 zikifuzu kwa hatua ya robo fainali.