Menu
in

Zacharia Hans Poppe mtetezi,mkosoaji wa soka la Tanzania

Zacharia Hans Poppe

Zacharia Hans Poppe

“Hata kama mimi ni kiongozi, lazima niwe na maoni yangu. Nakwambia alicheza chini ya kiwango katika mchezo ule”

Hiyo kauli ambayo niliambiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usaili ya Simba, Zacharia Hans Poppe baada ya mchezo mmoja wa watani wa jadi. Hans Poppe ametangazwa kufariki dunia hivi karibuni jijini Dar es salaam. Katika makala haya ninaeleza masuala machache yaliyowahi kujitokeza katika majadiliano naye.  

Nakumbuka katika majadiliano yetu kwenye kundi sogozi la michezo, Hans Poppe aliletwa kwa sababu ya kutoa kauli iliyotajwa na waandishi wa habari za michezo kuwa ya utata na inazua mgogoro miongoni mwa wachezaji wa Simba.

Siku hiyo kiongozi huyo alionekana kwenye picha za video akihojiwa na televisheni moja mara baada ya mchezo wa Simba na Yanga uliomalizika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sare ya mabao 1-1.

Kwa maoni yake kiongozi huyo alitaja kuwa Cletous Chama alikuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza chini ya kiwango. Kauli hiyo ndiyo ililalamikiwa na waandishi hao kuwa haikupaswa kutolewa na kiongozi wa aina yake.

Nikiwa miongoni mwa waliompachika maswali na kumkanya kuwa viongozi wa Simba wasiwe chanzo cha chokochoko katika timu, lakini Hans Poppe alijitetea kuwa yeye ni shabiki wa mpira mbali ya kuwa kiongozi wa soka.

Kwa Hans Poppe siku hiyo alikuwa anatetea hoja yake kwa namna mbili; kwamba alikuwa sahihi kutoa maoni hayo kwa mtangazaji wa televisheni, lakini pia alikuwa sahihi kutoa maoni hayo kwa kuwa naye ni shabiki wa mpira licha ya kuwa kiongozi wa Simba.

UCHAWI NA SAYANSI

“Mpira wetu umekuwa na changamoto nyingi. Unakuta mchezaji hayupo tayari kupokea matibabu ya Hospitali badala yake anawaambia viongozi wamache ashughulikie matibabu yeye mwenyewe kwa waganga na atarudi katika hali ya kawaida. Hilo siyo sawa, lazima tupokee sayansi pia,”

Hiyo ni kauli nyingine kuambiwa na Zacharia Hans Poppe juu ya mwenendo wa wachezaji wa soka wa Tanzania. kwamba baadhi ya wachezaji wanapoumia hawataki kupata katibabu hospitali badala yake wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji. Kiongozi huyo alikuwa anapingana na dhana hiyo kwa sababu iliwadhoofisha wachezaji badala ya kuwajenga.

“Yule mchezaji (jina linahifadhiwa) aliugua miezi 6 tukiwa naye Simba. Kila siku anapiga chenga kupewa matibabu hospitali, tena tulitaka kumpeleka Southa Africa, akawa anakimbilia kwa walozi huko kutumia mitishamba. Sisi tukawa tunamlipa fedha kama kawaida. Mwisho wa siku nikamwambia sasa tumekuchoka, tunakata mishahara au kuvunja mkataba. Hatuwezi kumlipa mchezaji halafu hakuna kazi unayofanya. Kuona hivyo ndio akakubali kwenda South Africa, hadi leo mnamuona anacheza vizuri na hana shida.”

Katika kauli hiyo Hans Poppe alikuwa anamzungumia mchezaji nyota wa Simba ambaye alikuwa anawasumbua kwenye suala la matibabu, huku akikazania kutumia mitishamba badala ya kufuata utaratibu wa klabu waliompangia.

Kwamba wapo wachezaji ambao wanaamini kuwa kuugua kwao kunatokana na nguvu za giza hivyo wanatakiwa kwenda kupata matibabu kwa waganga wa kienyeji. Mkasa huyo unamhusu mchezaji mkubwa mno na ambaye yuko kikosi cha kwanza cha Simba na Timu ya Taifa, Taifa Stars. Nyota huyo ni kiwakilishi cha baadhi ya tabia za wachezaji kuwa wapo tayari kugharamia matibabu kwa waganga wa kienyeji kuliko sayansi.

MISUMARI

Katika dhana ya uchawi, Zacharia Hans Poppe aligusia pia tabia ya wachezaji kupigana misumari kwa maana ya kurogana. Dhana hiyo pia alizungumzia kama kitu ambacho kinamaliza soka la Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla. Alisema kama ndivyo soka linavyopaswa kuwa basi mafanikio ya Afrika yangekuwa makubwa duniani.

Suala la kupigana misumari limekuwa kubwa na kwamba baadhi ya wachezaji wanaoumia hudhaniwa wamefanyiziwa vibaya.

“Mchezaji anatoka likizo, halafu anakuja anaanza mazoezi makali, lazima achanike misuli ya mapajani, maana anakuwa hajachukua tahadhari, hapo hakuna misumari. Madokta wetu wanatoa tahadhari mara nyingi, lakini kuzembea kupo,” amewahi kusema Hans Poppe katika majadiliano yetu kwenye kundi sogozi.

NANYOOSHA TU

Miongoni mwa mambo yaliyowahi kujadiliwa ni tabia ya kiongozi huyo kuzungumza kwa kunyoosha maneno bila kuvunga ama kama wasemavyo kuwa kubana koromoe kwa maana ya kunyamaza.  Hata hivyo Hans Poppe amewahi kueleza kuwa, hajali sana watu watachukuliaje, lakini yeye ananyoosha na kusema kile kilicho sahihi wala hana sababu za kupindisha.

Kwa mfano alipozungumzia ssbabu za mchezaji kucheza chini ya kiwango alisema hivyo kwa uso mkavu mbele ya televisheni. Na hata alipobanwa kwenye majadiliano katika kundi sogozi alisema hana sababu za kunyamazia upotofu na badala yake atatumia njia hiyo hiyo ya kunyoosha.

Miezi kadhaa iliyopita Hans Poppe ni kiongozi wa ngazi za juu aliyejitokeza kumkosoa aliyekuwa msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara kuwa aliondolewa klabuni hapo kwa sababu hakufuata masharti ya mkataba mpya uliokuwa umewekwa mezani.

Kiongozi huyo alibainisha masharti yote na kuonesha kuwa Simba hawakuwa tayari kuendelea naye kikazi. Tabia ya kutonyamazia mambo ndiyo imejenga taswira ya Hans Poppe na kuwa kiongozi ambaye haoni aibu kujitokeza hadharani kutoa mtazamo wake uwe unakubalika au haukubaliki.

Nimalize kwa kusema Hans Poppe alikuwa miongoni mwa hazina za viongozi wa soka nchini Tanzania. amefanya kazi yake kwa wakati wake, na sasa zamu imekuwa kwa upande wa wale waliohai kuendeleza weledi,msimamo nay ale yote ambayo alisimamia katika uongozi wake.   

HANS POPPE NI NANI?

Alizaliwa mwaka 1956 jijini Dar es salaam. Alipata elimu ya msingi na sekondari kabla ya kujiunga na Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambako alifanikiwa kufikia ngazi ya Kapteni. Baadaye aliachishwa kutokana na kukutwa na tuhuma za uhaini , katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza ya Julius Nyerere mwaka 1983.

Mnamo mwaka 1995 Hans Poppe aliachiliwa huru kwa msamaha wa rais Ali Hassan Mwinyi muda mfupi kabla hajamaliza ngwe ya uongozi wake.  Hans ni shabiki kindakindaki wa Simba tangu miaka 1970, na wakati wa uhai wake alikuwa kwenye kundi la Friends of Simba. Alikuwa mfanyabiashara mkubwa na kiongozi thabiti.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version