Menu
in , ,

YEYE ALIMPIGA KOFI MWINYI, MIMI NITAMKARIBISHA KIKOMBE CHA KAHAWA MAGUFULI.

Timu ya Tanzania katika michezo ya kimataifa


Shida yangu kubwa ipo hapa, ufanisi wa michezo kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla
.

Kumuonesha sera yake ya kubana matumizi ninaiunga mkono nitamkaribisha kwenye mgahawa wa hali ya kawaida kama ule alioingia Mwanza.

Safari hii sitotaka wananchi wajue uwepo wake kwa sababu nitakuwa na na mazungumzo nyeti na yeye.

Nitaanza mazungumzo yetu kwa kumuuliza swali, ” Hivi mheshimiwa unajua nchi ina njaa? “. Najua atashusha kikombe chake cha kahawa kwa kasi nakunikazia jicho.

Tabasamu langu litapokea jicho lake, kisha nitamwambia kuwa kwa kipindi kirefu nchi yetu imekuwa ikikumbwa na njaa ya mafanikio kwenye nyanja ya michezo.

Taratibu atakohoa na kushika kikombe chake cha kahawa kisha atakunywa taratibu huku akiniangalia usoni.

Nitamsubiri mpaka ashushe kikombe chake chini kisha niendelee kuongea.

Nashukuru sana kwa sera ya viwanda nchini, kwa sababu nchi yoyote inayotaka kuendelea lazima ipitie kwenye mapinduzi ya viwanda.

Kuna kiwanda kimoja ambacho kama kikiwekewa jicho la ziada naamini kitakuwa ni chachu kubwa sana katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa raisi, baada ya ofa yangu ya kahawa unatakiwa ukaonane na Mheshimiwa Dioniz Malinzi.

Muulize jukumu kubwa la Baraza la Michezo Tanzania ( BMT) ni lipi? Najua atakuambia ni kusimamia michezo yote nchini.

Lakini mkumbushe kitu kimoja siku zote muda huenda sahihi lakini sisi hatuendi sahihi. Kisha moyoni mwako baki na tumaini moja, sawa tumechelewa ila ni muda sahihi wa sisi kununua ua muda wa wenzetu walio lala.

Kuwa na taifa lenye watu wenye Afya, wakakamavu na ufanisi kwenye michezo kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Hii ndiyo dira ya BMT mheshimiwa Raisi, najua unapenda sana jamii unayoiongoza iwe na maendeleo makubwa sana.

Ni jambo jema sana, chukua muda wako uitafakari dira ya BMT, mimi sina shida na kuwafanya watu wa taifa lako kuwa wenye Afya na wakakamavu.

Shida yangu kubwa ipo hapa, ufanisi wa michezo kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.

Maendeleo ya viwanda unayoyahubiri yanaweza yakawa na tija kubwa sana kama utawekeza nguvu na muda kwenye kiwanda cha michezo.

Dira ya BMT inaelezea wazi kufanikisha maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, jaribu kumuuliza Dioniz Malinzi ni lini amekaa na kupanga, kuishauri wizara yenye dhamana ya michezo juu ya sera ya ukuzaji wa michezo Tanzania kama jukumu mojawapo la BMT?

Naamini mwenye kufuli ndiye aliye na funguo, ndiyo maana tulimwitaji sana John kwa kuamini anavyo vyote hivo.BMT ndiyo mama wa michezo lakini mama huyu amewasahau wanae kwa kiasi kikubwa.

Huwezi kuzivaa kofia zote mbili kwa wakati mmoja, lakini mpangilio wako sahihi wa muda ndiyo utakaokufanya uzivae vizuri hizo kofia mbili kila moja kwa wakati wake.

Kofia yako ya kijani inavutia sana, lakini ushawahi kujiuliza kijani ni alama sahihi ya uoto wa asili?. Siku zote kijani huvutia machoni mwa mwanadamu yoyote, lakini Mheshimiwa viwanja vinavyomilikiwa na kofia yako ya kijani havivutii kama ivutiavyo rangi ya kofia yako.

Kuna viwanja vingi sana ambavyo viko chini ya kofia yako ya kijani lakini vimekosa usimamizi dhabiti, vimechakaa kuanzia nje mpaka ndani ya uwanja.

Hivi unajua Uwanja kama wa Kirumba hutegemea mvua ili kusitawisha nyasi zile? Maji ya ziwa Victoria yako karibu na uwanja kwa nini kusiwepo miundombinu ya kupeleka maji kwenye kiwanja kama kile?

Maandalizi yetu yako tofauti sana na wenzetu, ndiyo maaa mara nyingi tukitamani suti huwa tunaingia kwenye ndoa.

Maandalizi ya ndoa hayaishii kwenye suti. Tunatakiwa Tujiulize maono yetu yakoje?

Mara nyingi macho yetu yana upofu wa tongotongo ndiyo maana viongozi wengi wa michezo ukiwauliza wanaona nini baada ya miaka kumi ijayo kwenye maendeleo ya michezo? Wengi wao huona giza.

Tunaona nini kwenye ligi zetu?, tunaona nini kwa wanariadha wetu? Tuna njaa ya kupata medali ya dhahabu, kushiriki AFCON, World Cup lakini hatuna maono yakutufanya tushibishe njaa zetu.

Ndiyo maana muda mwingi tunatumia kulisha njaa zetu na siyo maono yetu. Miaka imekuwa inaenda lakini hatusogei, tumekuwa watu wazuri sana kwenye kufukuza kivuli, ndiyo maana tumechoka sana bila kujua tunachokifukuza ndicho kinachotuchosha.

Ya Mungai tuyaache, hebu tulifikirie tena shindano la Umiseta na Umitashumita.

Nchi yetu ina mikoa takribani 30, huu ni mtaji mkubwa sana kwenye kiwanda hiki cha michezo.

Kwanini tusiboreshe sera ya uendeshwaji ya mashindano haya ili tupate vipaji vyenye tija?.

Hivi hawa vijana wanaopatikana kwenye hii michuano huwa wanapotelea wapi? Kwanini msitenge shule moja kila mkoa ya kulea vipaji hivi huku Wakiendelea na masomo.

Mheshimiwa Raisi, Ubelgiji unayoiona sasa hivi iko pale ilipo kwa sababu ya sera nzuri za michezo mashuleni ndiyo maana tunawaona kina Vincent Company.

Ushirikiano wako na mataifa mengine uko vizuri tena wanakusifu sana, nakushauri omba Ushirikiano na vituo vya kulelea vipaji kwenye mataifa mbalimbali ili upeleke baadhi ya watoto wanaopatikana kwenye michuano hii.

Tuachane na somo la Stadi za kazi maana huo ulikuwa mradi wa walimu kujipatia mwiko na mifagio. Hivi huoni umuhimu wa kuanzisha shule maalumu na chuo cha kufundisha michezo ili tupate wakufunzi wazuri wa masula ya michezo?

Kodi kwenye vifaa vya vikilimo imefutwa kwa sababu kilimo ni kiwanda muhimu sana hapa kwetu, hebu tazama kwa upande wa pili wa kiwanda cha michezo, bila vifaa bora hakiwezi endelea jaribu kuangalia kwa jicho lenye umakini, sikushauri ufute kodi, ila nakushauri uangalie upya.

Vita kuu yako imekuwa kupambana na mafisadi, hivi unataarifa kuwa ligi zetu zinakabiliwa na rushwa? Kama huna taarifa Takukuru watakufikishia, usisahau kuwauliza wameshughulikiaje hili suala.

Mimi sitaki kusababisha taifa langu liitwe kichwa cha mwendawazimu, karibu Magufuli kwenye kikombe cha kahawa.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version