*Alia na ubaguzi Kombe la Dunia
Kiungo mahiri wa Ivory Coast, Yaya Toure ametikisa ulimwengu wa soka kwa kuwaambia Manchester City kwamba anataka kuondoka kiangazi hiki.
Toure (31) amekuwa na mafanikio makubwa City katika misimu yake minne, na bado ana mkataba wa miaka mitatu Etihad.
Sababu anazotoa Toure kutaka kuondoka ni pamoja na kutaka kupumzika baada ya ugonjwa uliomsibu mdogo wake, Ibrahim ambaye alifariki mwezi uliopita kutokana na saratani.
Hata hivyo, hivi karibuni Toure alitishia kuondoka, akisema kwamba haheshimiwi na wamiliki wa klabu hiyo, ambapo hakuna mmiliki wala viongozi waliompa salamu siku ya kuzaliwa kwake.
Huyu ni mmoja wa viungo mahiri zaidi duniani, akibobea zaidi kwenye ushambuliaji na kupachika mabao 20 msimu uliopita kabla ya kuwaongoza Ivory Coast kwenye fainali za Kombe la Dunia Brazil ambako hawakufanya vizuri.
Toure ni mmoja wa wachezaji aghali zaidi duniani na iwapo ataondoka Etihad litakuwa pigo kubwa kwa kocha Manuel Pellegrini.
Ni wazi kwamba patakuwapo klabu nyingi zitakazotaka kumsajili lakini itabidi zivunje benki kuweza kumlipa mshahara wake mkubwa anaotaka.
Paris Saint-Germain wametajwa kutaka kumsajili, na alipoulizwa hivi karibuni, Toure alisema ingekuwa heshima kubwa kucheza huko Paris.
Toure aliyepata kuchezea Barcelona amefunga jumla ya mabao 51 katika mechi 184 alizochezea Ligi Kuu ya England (EPL).
Katika tukio jingine, Toure Amelia kwamba Waafrika wanabaguliwa, ndiyo maana hakuna anayejali kwa jinsi Ivory Coast walivyotolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Tembo hao wa Afrika walitolewa na Ugiriki ambapo walihitaji sare tu, lakini bao la penati tata katika dakika za lala salama ziliwazamisha.
Toure anasema ingekuwa si timu ya Afrika, watu wengi wangehoji utata katika kutolewa kwa timu husika na uhalali wa penati ya Georgios Samaras.
“Nilitaka sana mwamuzi aone vyema jinsi Samaras alivyojirusha badala ya kutoa penati kirahisi namna ile.
“Waamuzi hawakuwa upande wetu maana tulikataliwa penati mbili za wazi tulipocheza na Japan na dhidi ya Ugiriki imepikwa penati ya uongo.
“Hii ya kutolewa kwetu haiumizi mtu yeyote maana ni timu ya Afrika. Nani anajali? Kosa hili linatugharimu sana, ni kashfa na kwa bahati mbaya haionekani kuwagusa watu wengi,” akasema kiungo huyo kwa uchungu.
Hivi karibuni, Toure aliunga mkono maoni ya mchezaji mwenzake wa City, Samir Nasri aliyesema Toure angekuwa mchezaji bora zaidi duniani iwapo hangekuwa Mwafrika.
Toure anasema washabiki tu ndio wanaheshimu timu na wachezaji wazuri wa Afrika na kwamba daima atasimamia ukweli. Toure ndiye mchezaji bora wa Afrika maka huu.
Comments
Loading…