Kiungo mahiri wa Manchester City, Yaya Toure ametishia kuondoka klabuni hapo huku akisema hajui atachezea klabu gani msimu ujao.
Toure ameweka mazingira kuwa tete Etihad siku chache tu baada ya klabu hiyo kutwaa ubingwa wa England, mwenyewe akiwa na mchango mkubwa.
Toure (31) anaona kwamba hapewi heshima anayostahili na wamiliki wa klabu hiyo, ambapo wakala wake, Dimitri Seluk alidokeza kwamba anaweza kuondoka kwa sababu hana raha klabuni hapo.
Mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast amesema kwamba milango ipo wazi na lolote laweza kutokea kwake juu ya hatima ya soka na klabu atakayochezea.
“Hatujui lolote juu ya kesho, najielekeza kwenye Kombe la Dunia kwa sasa na tutaona itakavyokuwa baada ya hapo, kila kitu kipo wazi,” akasema kiungo huyo aliyefunga mabao mengi akiwa na City.
Alipoulizwa iwapo kuna uwezekano wa yeye kuchezea klabu nyingine alisema ndio, na kuongeza kwamba soka ni kitu chenye mambo mengi na si rahisi kwa wakati huu mtu kujua mambo yajayo.
Toure alisema kutokana na klabu hiyo kuwa na msimu mzuri, kila mtu anamzungumzia yeye na kwamba hata wakala wake muda wote huwa anapigiwa simu, kwamba ndiye anajua cha kufanya kwa sababu anamuanini sana.
Inajulikana kwamba Man City wanamtegemea sana Toure na hawana nia ya kumuuza wala kusikiliza ofa kutoka kwa klabu yoyote. Katika mechi ambazo hakucheza, timu yake hiyo haikufanya vizuri. Ana mkataba wa miaka minne na sasa amemaliza mwaka mmoja tu. Analipwa pauni 200,000 kwa wiki.
Inadaiwa kwamba hakuna kiongozi wala mmiliki yeyote wa City aliyempa Toure salamu za siku ya kuzaliwa kwake na anasema kuna heshima waliyomkosea ambayo ataieleza baada ya masuala ya Kombe la Dunia kwa nchi yake kumalizika.
Comments
Loading…