in , , ,

Yanga yashika usukani wa Ligi…

Dar Young Africans

Yanga iliongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuifunga Azam FC magoli 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana huku Simba wakikumbana na kipigo cha kwanza msimu huu kilichommwaga machozi nahodha Juma Kaseja cha 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar ugenini Morogoro.

Kinara wa mabao Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza ‘Diego’ walifunga goli moja-moja kila kipindi na kumkaribisha kocha aliyerejea Azam, Stewart Hall kwa kipigo kama kilichomfukuzisha kazi cha fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame) Julai 28, 2012.

Ushindi unaifanya Yanga iongoze ligi kwa kufikisha pointi 26 baada ya mechi 12 huku Simba ikiangukia katika nafasi ya pili kwa pointi 23. Azam inabaki kuwa ya tatu ikiwa na pointi 21, lakini ina mechi moja mkononi na wanaweza kuwashusha Simba hadi nafasi ya tatu kama watashinda mechi yao hiyo.

Yanga walipata goli la kwanza katika dakika ya 9 kupitia kwa Didier Kavumbagu aliyemalizia gonga safi baina ya Haruna Niyonzima, Simon Msuva na Mbuyu Twite, bao lililodumu hadi wakati wa mapumziko.

Mganda Kiiza alionyeshwa kadi ya njano kwa kuvua jezi yake wakati akishangilia goli la pili la Yanga alilolifunga katika dakika ya 68 kufuatia krosi ya Athumani Idd ‘Chuji’ na kuonyesha fulana ya njano isiyo na mikono yenye maandishi ya Kiingereza yaliyomaanisha “Pumzika kwa amani Mafisango. Naku-miss kaka yangu.”

Kocha wa Azam, Hall alikiri kwamba walizidiwa kwa kila kitu katika mechi hiyo.

“Yanga wamecheza vizuri, walituzidi karibu katika kila idara, hatukujilinda vizuri, eneo la katikati palikuwa ovyo na safu yetu ya ushambuliaji haikucheza vizuri, kwa kifupi tumecheza ovyo. Cha muhimu ni kujipanga kwa ajili ya mechi zetu zilizobaki,” alisema kocha huyo Muingereza.

Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na akaelezea furaha yake kwa mahasimu wao Simba kupoteza mechi yao ya kwanza.

“Timu imecheza vizuri licha ya makosa kadhaa katika dakika 20 za kwanza. Baada ya hapotulicheza vizuri kwa uelewano. Tumepata taarifa kuwa Simbawamepoteza mechi yao. Hiyo ni nzuri kwa sababu sasa tunaongoza ligi. Mwisho wa mechi hii ni mwanzo mzuri wa maandalizi ya mechi ijayo,” alisema Brandts.

Mjini Morogoro, Mtibwa ambao waliifanya Yanga imtimue kocha wao waliyedumu naye kwa siku 80 tu Mbelgiji Tom Saintfiet baada ya kuwadhalilisha kwa kichapo cha magoli 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, waliendelea ubabe wao kwa vigogo katika mechi ambayo Simba waliendeshwa puta mno kiasi cha kuwafanya kipa Kaseja na mshambuliaji Emmanuel Okwi watake kuzichapa wenyewe kwa wenyewe kabla ya kuamuliwa na kocha wao wa makipa James Kisaka wakati Simba wakiwa nyuma 1-0.

Mtibwa ilipata goli la kuongoza katika dakika ya 34 kupitia kwa Mohammed Mkopi aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Juma Kaseja kufuatia shuti la Vincent Barnabas.

Kipindi cha pili Simba ilijaribu kujiimarisha kwa kuwaingiza Mrisho Ngassa, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ badala ya Daniel Akuffor, Patrick Ochieng na Jonas Mkude lakini ni Mtibwa walioanza kipindi hicho kwa kulishambulia mfululizo lango la Simba.

Kaseja alimwaga kilio baada ya mtokea benchi, Hussein Javu, alipofunga goli la pili katika dakika za lala salama wakati wachezaji wa Simba wakipanda mbele kujaribu kusawazisha.

Balaa lilianza wakati Kaseja alipotoka langoni kwenda kujaribu kuuzuia mpira uliokuwa miguuni mwa Barnabas lakini mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars alimpasia Javu aliyekuwa katika nafasi nzuri na kufunga kirahisi goli lililozima ndoto ya Simba ya kumaliza mzunguko wa kwanza bila ya kupoteza mechi.

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alisema amekubaliana na matokeo kwani ndio soka lilivyo hata hivyo hakuacha kuwatupia lawama waamuzi akisema wanachangia kushusha morari ya wachezaji. Judith Gamba kutoka Arusha ndiye aliyekuwa refa wa mechi hiyo.

Mecky Mexime, kocha wa Mtibwa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, alisema amefurahishwa na ushindi huo na kwamba pointi za jana zimewasaidia kwani walikuwa katika hali mbaya ingawa ligi bado ni ngumu.

Mwanasoka bora wa Afrika wa zamani, Abedi Pele, ambaye amekuja nchini katika programu maalum ya kuendeleza michezo ya FIFA, alitambulishwa uwanjani kabla ya mechi ya Yanga na Azam kuanza.

Katika mechi ya utangulizi, Yanga B iliifunga Azam B kwa mabao 2-0, ushindi uliomkosha aliyekuwa makamu mwenyekiti wa kllabu hiyo, Davis Mosha ambaye aliwazawadia yosso hao Sh. milioni 1 akishirikiana na wajumbe wa klabu hiyo, Bin Kleb na Mussa Katabaro.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa:

Azam: Mwadini Ali, Erasto Nyoni/ Sahim Nuhu (dk.59), Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Morad, Bolou Michael, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jabir Aziz Stima, John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche na Mcha Khamis/ Abdi Kassim ‘Babi’ (dk. 62).

Yanga: Ali Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima.

Vikosi kwenye Uwanja wa Jamhuri vilikuwa:
Polisi Moro: Hussein Shariff, Hassan Kessy, Issa Rashid, Rajab Zahir, Salum Sued, Shaban Nditi, Jamal Mnyate/ Ally Mohammed (dk. 48), Babu Ally, Mohammed Mkopi, Shabani Kisiga na Vincent Barnabas/ Said Mkopi (dk.90).

Simba: Juma Kaseja, Shomary Kapombe, Amir Maftah, Komalmbil Keita, Pascal Ochieng, Jonas Mkude/ Ramadhani Chombo ‘Redondo’ (dk.68), Daniel Akuffor, Amri Kiemba, Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto na Emmanuel Okwi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Liverpool yaimarika, lakini bado makali, yalazimisha sare….

Clattenburg awavutia pumzi Chelsea