Baada ya kuwa nje ya michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati kwa miaka miwili kutokana na kufungiwa na kukosa ubingwa wa Bara, Yanga inarudi kwenye Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza tangu 2008 ikitafuta taji la nne la michuano hiyo.
Licha ya kuchuakua ubingwa wa Bara mara nyingi zaidi katika historia — 22 — Yanga inaishi katika kivuli cha Simba iliyofungua michuano hiyo jana, kwa wingi wa vikombe vya eneo hilo la Afrika.
Wakati Simba iliyotwaa ubingwa wa Bara mara nne pungufu ya Yanga ndiyo inayoshikilia rekodi ya mataji sita, la mwisho likiwa hivi karibuni mwaka 2002, Yanga iliibuka kidedea katika miaka ya 1975, 1993 na 1999.
Ili kucheza Kombe la Kagame Yanga imelipa faini ya dola za Marekani 20,000 kwa shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, na kupunguziwa kwa miaka miwili adhabu ya kuwa nje ya michuano hiyo kwa kosa la kuikacha Simba katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu mwaka 2008.
Na ikiwa na si tu kocha mzoefu wa Kombe la Kagame Sam Timbe wa Uganda bali pia kikosi kinachooneka kuwa kikali kikisheheni wachezaji nyota wa nyumbani na nchi za jirani pamoja na Ghana, Yanga ina kila sababu ya kuthibitisha kuwa haikuwekwa kimakosa kuongoza Kundi B la Kombe la Kagame.
Ipo pamoja na timu za El Mereikh ya Sudan, Bunamwaga ya Uganda na Elman ya Somalia.
Timu mbili, pengine Yanga na mabingwa mara mbili El Mereikh zinazofungua pazia leo, zitasonga mbele kutoka kundi hilo kuingia robo-fainali.
Mbali na mechi ya Yanga, mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame timu ya APR inatarajiwa kuanza vizuri michuano hiyo katika mchezo wa Kundi C dhidi ya Ports Authority ya Djibout mjini Morogoro.
Kesho Jumatatu, Kombe la Kagame litazikutanisha Bunamwaya na Elman za Kundi B pamoja na Ulinzi na St George mjini Morogoro.
Comments
Loading…