Mabingwa wapya, Simba, jana walikamilisha msimu wao mzuri wakati walipowabwaga mahasimu wao wakubwa Yanga, waliobaki tisa uwanjani, katika mechi ya aina yake iliyojaa magoli, ambapo Wekundu walishinda 4-3.
Kinara wa mabao Mussa Hassan ‘Mgosi’ alifunga mara mbili katika mechi ambayo wachezaji wawili wa Yanga walitolewa kwa kadi nyekundu kabla ya Hillary Echessa wa Simba naye kutolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 90 baada ya kuvua shati wakati akishangilia kuwafunga Yanga goli la ushindi, wakati alishakuwa na kadi ya kwanza ya njano.
Mgosi sasa amefikisha magoli 16, mawili zaidi ya wapinzani wake katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora huku ikiwa imebaki mechi moja ligi kumalizika. Mrisho Ngassa wa Yanga na John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC wana magoli 14 kila mmoja.
“Nimedhihirisha kuwa mimi ndiye mshambuliaji bora wa Tanzania msimu huu,” alisema Mgosi aliyejaa furaha tele baada ya mechi hiyo, ambayo wachezaji wa Yanga Wisdom Ndlovu (dk.57) na Amir Maftah (dk.85) walitolewa kwa kadi nyekundu. Ndlovu alitolewa kwa kumpiga kiwiko Nico Nyagawa wakati alikuwa tayari ana kadi ya njano, na Maftah aliyekuwa na njano pia alitolewa baada ya kumpiga kichwa Juma Nyosso.
“Haya ni matunda ya mshikamano,” alisema Selemani Matola, aliyechukuliwa kumsaidia kocha msaidizi wa Simba Amri Said, baada ya kocha mkuu Mzambia Patrick Phiri kushindwa kurejea nchini kuiandaa timu hiyo, kufuatia kwenda kwao kumuuguza mwanaye wa kiume aliyekuwa amelazwa hospitali. Hata hivyo, Matola hakukaa kwenye benchi la Simba.
Kipa wa Simba, Juma Kaseja, ambaye alisujudu wakati timu yake ilipofunga goli la pili kupitia kwa Mgosi, alilia sana wakati alipofungwa kwa goli la penalti aliyoisababisha iliyofanya matokeo yawe 3-3, na alilia tena wakati Echessa alipofunga goli la nne lililoizamisha timu hiyo aliyoichezea msimu mmoja uliopita.
Baada ya ushindi huo mgumu katika mechi iliyotawaliwa na funga-nikufunge, wachezaji wa Simba walivishwa medali za dhahabu na wakabidhiwa kombe lao la ubingwa walilolitwaa mechi moja kabla ya kucheza na Yanga jana, huku wana Jangwani hao wakipewa kombe dogo na medali za fedha.
Kocha wa Yanga, Kostadin Papic, alisema kuwa makosa ambayo timu yake ilifanya katika kipindi cha pili ndiyo yaliyowagharimu, lakini anafuraha kwamba ameibadili timu hiyo.
“Msimu ujao Yanga itakuwa ni timu nzuri sana,” alisema Papic.
Mechi ya funga-nikufunge ilianza mapema katika dakika ya tatu wakati mshambuliaji wa Simba aliyerejea kwenye kiwango baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi, Uhuru Selemani, kufunga goli baada ya kumtoka Maftah na kupiga shuti lililompita kipa Mserbia Obren Curkovic.
Kiungo wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ alisawazisha goli hilo katika dakika ya 31, Mgosi akaongeza la pili kwa Simba katika dakika ya 53 kabla ya John Tegete aliyekuwa ameingia dakika tatu tu zilizotangulia alipoisawazishia Yanga katika dakika ya 67 wakati wachezaji wa Simba walipomsindikiza golini.
Mgosi akaifungia Simba bao la tatu katika dakika ya 73, kabla ya Tegete kufunga bao lake la pili jana katika dakika ya (89) kwa njia ya penalti lililofanya matokeo yawe 3-3, baada ya Kaseja kumwangusha Abdi Kassim ‘Babi’ aliyekuwa akienda kufunga goli, kitendo kilichomzawadia kipa huyo kadi ya njano. Echessa akafunga goli la nne katika dakika ya 90, lililoipa Simba pointi zote 6 dhidi ya mahasimu wao Yanga msimu huu.
Comments
Loading…