*Wawa wa kwanza kuwafunga Ligi Kuu
*Mwanasoka Omar Changa afariki dunia
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania, Yanga ya Dar es Salaam wameweka rekodi kwa kuwa wa kwanza kuwafunga Mbeya City katika michuano hiyo.
Mbeya City wanaofundiswa na kocha Juma Mwambusi walimaliza awamu ya kwanza ya ligi hiyo kwa ama kushinda au kutoa suluhu na sare mechi zote.
Waliwahi Dar es Salaam mapema baada ya kwenda sare mkoani Pwani kabla ya kukumbana na Yanga ambao pia walikuwa wametoka suluhu na Coastal Union ya Tanga Jumatano.
Hata hivyo, Yanga ndio waliocheka zaidi baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mrisho Ngasa katika dakika ya 16.
Kocha Mwambusi alieleza kusikitishwa kwake na matokeo hayo ambayo hata hivyo alisema wanayakubali na kwamba wataeweka jitihada zaidi kwenye mechi zinazofuata.
AZAM WATOA KICHAPO CHA HAJA
Katika mechi nyingine kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam, Azam waliwachabanga Kagera Sugar 4-0.
Haikuwa rahisi kuamini matokeo hayo kutokana na uimara uliozoeleka wa Kagera Sugar, lakini ndivyo ilivyotokea na Azam kuendelea kukalia uongozi wa ligi kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Yanga.
Brian Omony alifunga mabao mawili wakati kinda Kevin Sunday na Jabir Aziz walifunga moja moja.
TANZIA: OMAR CHANGA AFARIKI DUNIA
Katika tukio jingine la kusitikisha mchezaji wa Moro United aliyepata pia kuzichezea Yanga na nyinginezo, Omar Changa amefariki dunia.
Maiti ya Changa ilikutwa eneo la Jangwani Darajani na haikujulikana chanzo cha kifo chake.
Viongozi wa Moro United walieleza kwamba walikuwa wakishughulikia maandalizi ya maziko yaliyotarajiwa kufanyika Jumatatu hii. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Comments
Loading…