Picha mbili zilionesha hali halisi ya kocha wa Yanga, Saed Ramovic. Kocha alikuwa aminamisha kichwa huklu kamera za televisheni zikionesha kwa ukaribu zaidi. Hali kadhalika, picha nyingine ilimvuta na kuonesha akiwa ameshikilia kidevu chake. Uso wake ulikuwa umejaa taharuki na akilini bila shaka mlikuwa na mawazo mengi. Yanga walikuwa wamefungwa mabao 2-0 ya ajabu ajabu na timu ambayo haikuwa na kiwango cha kutisha ya MC Alger ya Algeria. Lakini wakati MC Alger wakishinda kwa mabao 2-0 upande wa Yanga haukuwa na kitu cha kujivunia kiwanjani. TANZANIASPORTS inafahamu kuwa mojawapo ya changamoto ya timu hiyo ni matumizi sahihi ya wachezaji na mkakati wa ushindi unaondaliwa na mkuu wa benchi la ufundi.
Namna Yanga wanavyosomeka
Tangu kuingia kwa kocha Saed Ramovic amefungwa mabao manne katika kipindi cha pili kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Mkakati wa Yanga kipindi cha kwanza unakuwa imara ingawaje haujaleta matokeo mazuri. Kipindi cha kwanza Yanga wanacheza vyema, wanazuia vyema,wanajaribu kupanga mashambulizi yao, lakini katika hatua ya mwisho wanashindwa kumalizia. Katika mchezo dhidi ya Al Hilal washambuliaji wa Yanga walishindwa kutumbukiza mabao wavuni.
Kipindi cha pili Al Hilal walibadilika kwa kiasi kikubwa na kufunguka kuanzia eneo la katikati ya kiwanja kwa kupiga pasi ndefu za mashambulizi ya kushtukiza yaliyowapatia mabao mawili safi. Kocha wa Yanga hakuwa na jambo la ziada kuwaokoa wachezaji wake kimbinu na hata mabadiliko aliyofanya hayakuwa na mwelekeo. Katika mchezo dhidi ya MC Alger hali ya Yanga ilijirudia kwani walipigwa mabao 2-0 kipindi cha pili, tena yalikuwa mabao ya ajabu ajabu mno.
Mashambulizi ya MC Alger hayakuwa yale ya kuitisha Yanga, wala timu yenyewe kwa ujumla haina waarabu wakali kama zamani. MC Alger ilibadilika kipindi cha pili kwa kufahamu kuwa Yanga wanakatikati mno kuanzia eneo la kiungo hadi ulinzi. Kwa vile safu ya ushambuliaji haikuwa na maajabu, ikawapa pumziko MC Alger na kuongeza ari ya kushambuliaji. Kwa maana hiyo mabao mawili ya MC Alger yalikuja kipindi cha pili. Mabao ya Al Hilal nayo yalikuja kipindi cha pili. Katika kipindi hicho kocha hana mpango mbadala wa kuifanya Yanga iwe na makali kuliko kipindi cha kwanza. Hapo ndipo tunaona Yanga wanasomeka lakini wenyewe hawasomi mbinu mbadala za wapinzani wao.
Mbinu zinawaumiza wachezaji
Katika eneo la kiungo kocha aliwatumia Duke Abuya na Mudathir Yahya. Hata hivyo eneo hili lilikuwa linapokea pasi butu au kupoteza mipira katika mazingira mepesi. Mipira mingi ilikuwa ikipotea eneo hili na kuwafanya MC Alger wapokee na kuipeleka pembeni kwa wachezaji wao. Mara nyingi wachezaji walioonekana hawaelewi wasimame katika nafasi ipi ili kutekeleza mkakati wa timu.
Kiungo mshambuliaji Maxi Nzengeli ni mwathiri wa mkakati ya kocha Saed Ramovic. Uchezaji wa Maxi Nzengeli unaonesha wazi unamchanganya kujua majukumu yake katika kushambuliaji na kujilinda. Katika dkaika 180 ametumika katika kuzuia zaidi kuliko kuwa grisi ya kulainisha mambo ya safu ya ushambuliaji na kiungo.
Mfumo wa “Double Pivot” umempa umaarufu sana Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya lakini kocha Ramovic anawaweka wacheze upande mmoja mmoja. Mechi ya pili timu inapotea kipindi cha pili maana yake kocha ameshindwa kuwajua wapinzani wake, ila wapinzani wake wanamsoma na kumchapa kipindi cha pili. Dube Abuya ni mchezaji mzuri lakini si kiungo mkabaji wa kumaloiza shughuli ya kuwalinda walinzi wake. Abuya anacheza vizuri akiwa na viungo wenzake wawili wenye majukumu ya kumpunguzia shinikizo la wapinzani. Yaani viungo wenzake wanakuwa na kazi ya kuwezesha mambo yake yaende vizuri hasa akiwa eneo la namba 8.
Dakika 90 bila mashuti
Matatizo ya Yanga ni ya kiufundi zaidi kuliko kuwatazama wachezaji mmoja mnmoja. Ile kombinenga yao katika mechi imesambaratishwa na ufundi ambao hauwaongezei maarifa zaidi ya kuwachanganya. Timu inacheza dakika 90 za mchezo dhidi ya MC Alger bila kuwa na shuti lolote la maana langoni (Shot on target). Hawa ni wachezaji waliotamba,walitetemesha Afrika na kuogopeka inakuwa ajabu ghafla wawe wameishiwa makali ndani ya kiwanja. Hii ndiyo timu iliyokuwa inawatisha waarabu kuanzia kwenye kombe la shirikisho hadi Ligi ya Mabingwa. Lakini ghafla timu haisomeki inacheza mifumo gani ya ushindi. Dakika 90 haiwezi kupiga shuti hata moja langoni mwa adui, ni kwamba kocha na wachezaji wake hawakuwa uwanjani.
Pengo la namba 9
Uzoefu unaonesha kuwa eneo la kiungo ndilo injini ya timu. Yanga walianza mchezo bila mshambuliaji kamili wa eneo la namba tisa. Aziz Ki sio mshambuliaji bali kiungo mchezeshaji, wakati Kennedy Musonda alipelekwa upande wa kushoto hivyo kuliacha eneo la namba 9 likiwa tupu. Kama kocha alihitaji huduma ya Aziz Ki na Pacome Zouzoua alitakiwa kuchagua mmojawapo kisha kumpa nafasi mshambuliaji.
Ni kweli kwamba Prince Dube hajaanza vizuri kwenye kikosi cha Yanga lakini si mshambuliaji wa kutilia shaka kwenye uwezo wa kupachika mabao. Mwalimu wa Yanga aliwafanya wachezaji wake wabunifu wachoke mapema sana kwa sababu kazi yao ya kuwalisha washambuliaji iliporwa kwa kukabidhiwa wao kuwa na jukumu la kuwa washambuliaji. Aziz Ki na Pacome wakaishia kuwa wakimbizaji wa mpira kuliko kuiandalia timu mabao.
Mwishowe kocha wa Yanga alimpumzisha Aziz Ki mara baada ya kumalizika kipindi cha kwanza. Hapo mwalimu alijificha katika makosa yake na ufahamu mdogo katika matumizi ya wachezaji pamoja na mashindano makubwa. Mabadiliko yake hayakuwa na jambo lolote la kuifanya Yanga ipandishe makali yake kwa sababu walikuwa na pengo la namba tisa. Baadaye Prince Dube alipoingia hakuweza kurudisha uhodari wa timu kwa sababu walishaji walishachoka na jukumu lilibaki kwa Pacome Zouzoua pekee.
Comments
Loading…