USHINDI wa magoli 3-1 waliopata Yanga dhidi ya TP Mazembe kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaonesha safari ya miamba hiyo ya Dar Es Salaam kujiwinda na kufuzu hatua ya robo fainali imeanza. Yanga waliuanza mchezo huo taratibu huku wakiwa na wanakabiliwa na miamba yenye uzoefu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ingawa Yanga waliruhusu bao mapema na hivyo kuwaweka katika shinikizo zaidi na kurudisha imani ya mashabiki. Kwa ushindi huo Yanga wamejikusanyia pointi 4 kutokana na michezo minne wastani wa pointi moja kila mchezo. TANANIASPORTS inakuletea tathmini ya mchezo huo na masuala mbalimbali yaliyojitokeza kifundi kuanzia kwa benchi la ufundi na wachezaji binafsi.
Imani ya mashabiki wa Yanga
Kama kuna kazi kubwa waliyonayo watu wa benchi la ufundi na uongozi ni kurudisha imani ya mashabiki wao. Yanga waliwazoesha kushinda, waliwapa raha, walizoea shangwe kila siku lakini ghafla kwenye mashindano haya wameanza vibaya ambapo walikung’utwa mabao 2-0 nyumbani na Al Hilal.
Safari ya Yanga kwenye mashindano hayo iliingia hofu ambapo mashabiki walikuwa wanajaribu kuisoma akili na umahiri wa kocha wao mpya Sead Ramovic ambaye aliajiriwa kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyvunjiwa mkataba baada ya kipigo kutoka Tabora United.
Mashabiki bado wanamhitaji Ramovic kuwaonesha uimara wake na kuwapa raha walizozoea. Mashabiki wa Yanga wana CV kubwa kwani timu yao ilishafika fainali ya Kombe la Shirikisho na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kitu ambacho kocha wao hana uzoefu nacho. Kwa kuzingatia hayo ni wajibu wa viongozi na benchi la ufundi kuwaaminisha wanayanga kuwa raha zinakuja na sasa wameanza kujipata.
Magoli ya Video
Haya ni magoli ya aina yake na yenye mvuto kwa watazamaji na hata wachezaji wenyewe huoni ufundi waliotumia kufunga. Katika mchezo huo Yanga imetoa mabao mabao mawili ya video ambayo yamekuwa maarufukwenye mitandao mbalimbali Afrika kuanzia ule wa Shirikisho la Soka CAF.
Bao la kwanza lilifungwa Clement Mzize lilitokana na shuti kali la nje ya 18. Mashuti ya namna hiyo yameandimika kwenye viwanja vya soka, nap engine mchezaji pekee ambaye kwa sasa anafanya kama Clement Mzize ni Federico Valverde wa Real Madrid.
Valverde ndiye ni mtaalamu wa mabao ya mashuti makali na yenye kasi. Mzize alifunga bao hilo baada ya kumchungulia golikipa wa TP Mazembe ambaye alifanya kosa la kuliacha lango mita takribani tano na hivyo kuacha mwanya nyuma yake. Shuti hilo lilikwenda moja kwa moja wavuni na kuwashtua mashabiki juu ya uwezo na uimara wa nguvu za miguu alionao mshambuliaji wao.
Bao la pili la video lilifungw ana staa wao Stephanie Aziz Ki ambaye alipokea pande safi kutoka kwa kiungo mkabaji Khalid Aucho kutoka wingi ya kulia. Pasi hiyo mpenyezo ilikutana na maarifa ya staa wa Burkina Fasso, Aziz Ki ambaye kwa utulivu mkubwa alimchungulia golikipa kisha kupiga mpira mdogo uliompita ‘Tobo’ golikipa wa TP Mazembe. Magoli haya yameipa thamani Yanga na kuonesha namna wachezaji wao wanavyoweza kubadili mambo.
Bila mfumo Yanga wanacheza
Nyakati hizi makocha wanazungumzia sana mfumo, lakini kiuhalisia mpira lazima uchezwe. Kocha wa Yanga alianza kwa 3-4-2-1 ambapo ambapo aliwapa nafasi washambuliaji wawili Prince Dube na Clement Mzize kuongoza safu ya ushambuliaji. Aziz Ki kama kawaida alipewa jukumu la kuwa mchezaji huru akishirikiana na Pacome Zouzoua. Kiufundi Clement Mzize ndiye alikuwa mchezaji mwenye uhuru mwingi kushambulia , kucha wingi zote mbili (kulia na kushoto) kisha kama mshambuliaji namba mbili.
Mabadiliko hayo ya ndani yalimpa uhuru pia Aziz Ki kucheza wingi ya kulia na wakati mwingine nyuma ya Prince Dube. Pia Pacome Zouzoua alicheza nafasi zote tatu; wingi ya kulia, nyuma ya Prince Dube na upande wa kushoto. Kwahiyo kocha huyo alikuwa na wachezaji watatu waliokuwa wanaendesha timu kuanzia katikati ya dimba kuelekea lango la adui.
Pengine huo si mfumo wa ajabu kwa sababu wamecheza mara nyingi na kocha alichofanya kuwapa uhuru wa kucheza. Uchezaji wa Yanga ya sasa ni ule wa kasi na mbio, huku kiwango cha upigaji wa pasi kikiwa kimepungua. Wakati wa kocha Nasredine Nabi na Miguel Gamondi wote wawili walipenda kuona timu zao zinapiga pasi nyingi kabla ya kupachika mabao. Lakini chini ya Ramovic Yanga wanashambulia zaidi, bila kujali mtiririko wa pasi na kutawala mchezo.
Prince Dube anakuja na michomo
Pamoja na kwamba hakufunga bao katika mchezo huo lakini mchango wa Prince Dube ni dhahiri upo na sababu hiyo kocha alimwacha katika dakika zote 90. Kiuchezaji Dube ni mshambuliaji mwenye kuhitaji nafasi chache kupachika mabao hasa kama wanaompikia pasi za mabao wanaelewa namna ya kumtumia.
Katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu ameonesha umahiri na kufunga mabao muhimu na kufikisha matano. Katika mfumo wowote ule Dube anafaa kucheza kwa namna ambavyo kocha anavyopanga timu yake.
Kupenya katika kundi
Yanga wameshinda mchezo huu ambao ulikuwa muhimu kufufua matumaini yao ya kufuzu hatua yarobo fainali. Katika msimamo wa kundi hilo Yanga wana pointi nne tu. Wanahitaji pointi sita ili kufikisha pointi 10 kufuzu robo fainali. Mechi zao mbili watachezaji nyumbani na ugenini; dhidi ya Al Hilal ya Sudan (ugenini) na MCA ya Algeria.
Katika michezo hiyo Yanga wanahitaji kushinda sio kutoka sare ya aina yoyote. Michezo yote miwili ni muhimu kwa sababu watajihakikishia kufuzu. Je watamudu hatua hiyo? Ni jambo la kusubiri na kuona, angalau sasa wameanza kujitafuta.
Comments
Loading…