Mabao mawili yaliyofungwa na Maurice Sunguti jana yaliiwezesha Yanga kusoga mbele katika Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya AS Adema ya Madagascar.
Yanga awali ilionekana kama ingetolewa katika mashindano hayo baada ya kushindwa kufunga bao lolote hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Watani zao na Yanga, Simba nao jana walifuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kutoka sare ya 1-1 na Awassa ya Ethiopia katika mchezo uliofanyika Ethiopia na kuifanya timu hiyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-1.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam karibu wiki mbili zilizopita, Simba ilishinda 3-0.
Mshambuliaji huyo wa Kenya aliifungia Yanga mabao yote hayo katika kipindi cha pili katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Sunguti alifunga bao la kwanza kwa penati katika dakika ya 53. Mwamuzi wa Sudan alitoa penati hiyo baada ya beki wa Adema kumchezea vibaya Mrisho Ngasa katika eneo la hatari.
Sunguti aliongeza bao katika dakika ya 69 na kuihakikishia Yanga nafasi ya kusonga mbele, ambapo sasa itacheza na mwakilishi wa Chadi au Libya katika mchezo unaofuata.
Adema iliifunga Yanga 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Madagascar wiki mbili zilizopita na hivyo kuifanya Yanga kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.
Kocha wa As Adema Frank Rejaomarisamba aliwalalamikia waamuzi akidai kuwa walikuwa wakiibeba Yanga, huko kocha wa Yanga Dusan Kondic akifurahia ushindi na kuipongeza timu yake.
Katika hatua nyingine, wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Simba nao walisonga mbele baada ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji wao Awassa, katika mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye uwanja wa Addis Ababa jana.
Meneja wa Simba Innocent Njovu akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Addis Ababa kuwa Awassa ilikuwa ya kwanza kufunga katika dakika ya kwanza kabisa kabla ya Athumani Machupa kusawazisha katika dakika ya 12.
Simba katika mchezo wa kwanza aliifunga Awassa 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Simba sasa ina kibarua kigumu katika hatua inayofuata wakati itakapocheza na Enyima ya Nigeria katika mchezo wa kwanza utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kurudiana huko Lagos, Nigeria.
Comments
Loading…