Yanga wamefanikiwa kusonga mbele kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kupata ushindi wa jumla ya mabao 3-2.
Katika mechi ya mkondo wa pili nchini Botswana, Yanga walilala kwa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Jeshi ya BDF, lakini ushindi wake wa 2-0 jijini Dar es Salaam ukawa na maana.
Yanga waliwachapa BDF 2-0 kwa mabao ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Amisi Tambwe kabla ya jana kufungwa 2-1 mjini Gaborone, Botswana mwishoni mwa wiki.
Yanga wanatinga hatua inayofuata ya CAF na watakutana na mshindi baina ya Sofapaka wa Kenya na Platnum kutoka Zimbabwe.
Yanga walijilinda vyema kipindi cha kwanza, wakitambia ushindi wa mechi ya awali na nusura
Mrisho Ngassa afunge bao mapema alipompita beki wa kati na kubaki na kipa, lakini alitoa mpira nje.
BDF walimpoteza beki wa kushoto, Othusitse Mpharitlhe aliyelambwa kadi nyekundu kwa rafu dhidi ya Simon Msuva dakika ya 20 lakini waligangamala.
Alikuwa Ngassa aliyefunga bao dakika ya 30 baada ya kutiliwa pasi na Tambwe
BDF walisawazisha bao kupitia kwa Moreetsi Mosimanyana dakika ya 49 kisha Danny Mrwanda wa Yanga akatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuwa ameoneshwa ya kwanza ya njano, ikimaanisha atakosa mechi inayokuja.
BDF walidhamiria kushinda, na walipata bao lao la ushindi dakika tano kabla ya kukamilika saa moja na nusu ya mchezo, na ilikuwa uzembe wa mabeki wa Yanga kushindwa kujipanga vyema.
Timu zilikuwa – Yanga: Ally Mustapha, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Msuva, Haruna Niyonzima, Tambwe, Ngassa na Mrwanda.
BDF walikuwa Ontiretse Gaothobogwe, Bonolo Phuduhudu, Pelontle Lerole, Othusitse Mpharitlhe, Moreetsi Mosimanyana, Mosha Gaolaolwe, Thato Ogopotse, Kabelo Seakanyeng, Master Masitara, Mompati Thuma na Vicent Nzombe.
Comments
Loading…