in , ,

Yanga ina kikosi chepesi katika michuano migumu

Kuna habari nyingi sana huwa zinanichanganya kichwa, habari ambazo huwa zinanifanya niwaze.

Tafakuri yangu huchukua muda mrefu sana lakini majibu yake huwa tofauti na mitazamo ya walio wengi.

Ndimi za watu wengi zinakiri kuwa ligi yetu ni ngumu, ndimi hizi huwa zinanichosha pale zinapohubiri ugumu wa ligi yetu kutokana na ushindani unaoonekana kwenye ligi yetu.

Ligi ambayo haina wadhamini wengi wa kutosha, ligi ambayo vilabu vyake vinalia njaa kwa sababu ya kushindwa kujiendesha kibiashara.

Ligi ambayo haina makocha ambao wana elimu kubwa ya kufundisha mpira na makocha wasiopenda kujifunza mabadiliko ya mpira wa kisasa.

Ligi ambayo ina viongozi wanaoongoza vilabu vyao katika misingi ya kijamaa, bakuri ndiyo huwa msaada tosha katika kuendesha timu zao, bakuri ambalo halina ujazo wa motisha kwa wachezaji.

Nguvu za kupigana huishia nje ya uwanja kwa sababu hakuna kinachowafanya wapigane kwa nguvu.

Ndipo hapo vilabu vya Simba na Yanga vinapochukua upenyo wa kubadilishana makombe.

Ni vilabu vikongwe, haviendeshwi katika misingi ya kisasa lakini vina watu ambao huvipenda kwa dhati mpaka kufikia hatua ya kujitolea pesa zao ili kuiimarisha timu yao kwa msimu husika.

Usajili unaofanyika huwa unafanyika katika viwango vya kawaida, wachezaji wanaoletwa Simba na Yanga huwa hawapishani kwa kiasi kikubwa na wachezaji wa timu zingine, kinachowatofautisha ni huduma tu.

Huduma ndiyo huamua nani ni bingwa wa ligi yetu na ninani anastahili kushuka daraja.

Mwenye huduma  nzuri katika msimu husika ndiye ambaye huwa na uwezo mkubwa wa kuchukua kombe la ligi kuu ya Tanzania.

Hatua inayofuata ndiyo huwa inakuwa kichekesho kwa mwakilishi wetu wa mechi za vilabu vya kimataifa.

Hutia aibu, hutia simanzi na hutia huruma ambayo hugeuka kuwa mshangao, na nirahisi sana kujiuliza maswali yenye mshangao mkubwa ndani yako unapomuona bingwa wa nchi yako anaposhindwa kupambana na bingwa wa nchi nyingine tena kwa kupokea kipigo cha fedhea!.

Ndipo hapo akili yangu inapokuja kujihoji swali moja, iko wapi ligi ya ushindani tunayoihubiri?, uko wapi ubora wa ligi yetu kama timu zetu haziwezi kushindana na timu zenye nguvu katika michuano ya CAF?

Jibu ni jepesi tu, ligi yetu inampata bingwa kutokana na utofauti wa huduma iliyopo ndani ya Simba, Yanga na vilabu vingine.

Hakuna ubora uliopo kwenye ligi yetu, hata hizi timu ambazo tunazihubiri ni kubwa na ni bora hazina vikosi imara vya kushindana katika mashindano ya kimataifa.

Vikosi vyao vina wachezaji ambao wana uwezo wa kushindana katika michuano yetu ya ndani tu, michuano ambayo hupeleka mwakilishi kwenye michuano ya kimataifa, mwakilishi ambaye hana kikosi imara cha kushindana kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Hapo ndipo mwanzo wa kutengeneza uongo wa kutufurahisha unapoanza. Uongo huu huanza kutufurahisha kumuona Emmanuel Okwi anapoifunga Azam Fc timu ambayo haina kikosi imara kama timu tunazokutana nazo katika mechi za kimataifa.

Uongo huu hutufurahisha kweli na cha ajabu hututia upofu na kushindwa kuona wenzetu wanavyofanya usajili imara kwa ajili ya michuano hii ya kimataifa.

Tabia yetu ya kusajili kwa mazoea huendelea, tunasajili mchezaji kutokana na matakwa ya mtu na siyo kulingana na matakwa ya benchi la ufundi, ndipo hapo tunapojaza wachezaji wa kawaida katika vilabu visivyo vya kawaida.

Yanga ya jana ilikuwa Yanga iliyojaza wachezaji wa kawaida katika klabu isiyo ya kawaida.

Wachezaji ambao hawana ushindani, hapana shaka walienda Algeria kwa ajili ya kupunguza idadi ya magoli ya kufungwa.

Hawakuwa na wachezaji wa kushindana kwa nguvu ili kupata alama katika uwanja wa nyumbani.

Wote walikuwa wakiwa kama makinda ya ndege yaliyoachwa na mama yao bila msaada wowote.

Hakukuwepo na kiongozi kuanzia katika benchi la ufundi mpaka ndani ya uwanja. Idara zote tatu (ulinzi, kiungo na ushambuliaji) zilikosa mtu wa kuongoza.

Safu ya ulinzi ilikuwa inashindwa jinsi ya kukaa na kujilinda nyuma ndiyo maana magoli yao waliyofungwa yalikuwa ni kwa sababu ya ‘marking’ mbovu.

Hata kuanzisha mashambulizi walinzi walishindwa, viungo wakakosa cha kufanya hali iliyowafanya washambuliaji wakose cha kutenda.

Hakukuwepo na kiongozi yoyote wa kuwaongoza ili wafanye maamuzi yaliyokomaa uwanjani, hakukuwepo na mchezaji wa kuibeba timu kuanzia golini mpaka kwa mshambuliaji.

Na kibaya zaidi hata benchi la ufundi walishindwa kipi wanatakiwa kufanya kuanzia mwanzo wa mchezo mpaka mwisho wa mchezo, timu ilikuwepo pale kukamilisha dakika 90 tu bila mpango wowote wa kutoka na alama yoyote.

Mail to: [email protected]

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kwa heri Arsene Wenger, tutakukumbuka

Tanzania Sports

YALIYOJIRI LIGI KUU YA ENGLAND