Kama utani vile, wenyeji wa mashindano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Guinea ya Ikweta wametinga robo fainali baada ya kuwazidi nguvu Gabon na kuwafunga 2-0.
Guinea ya Ikweta ndiyo timu iliyokuwa ya chini zaidi kwenye mashindano haya kwa kiwango cha soka, lakini wamefanikiwa kuvuka kihunzi cha kwanza na kuingia hatua inayofuata, hali iliyowatia kiwewe washabiki na taifa kwa ujumla.
Wakiwa wameandaa mashindano chini ya notisi ya dharura baada ya Morocco kujitoa kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola, Guinea ya Ikweta wana kila sababu ya kufurahia kuvuka kwao, ikizingatiwa pia ni nchi ndogo na yenye wananchi wachache.
Mshambuliaji Javier Balboa alifanikiwa kucheka na nyavu baada ya dakika 55 za ukame, ikiwa ni kwa penati kutokana na kuchezea vibaya na Lloyd Palun wa Gabon. Dakika nne kabla ya mechi kumalizika, walijiweka pazuri kujihakikishia ushindi, pale Salvador Iban aliyetokea benchi akipachika wavuni mpira uliorudishwa uwanjani kutokana na kiki ya Emilio Nsue.
Guinea waliingia uwnajani wakijua kwamba ni ushindi tu ungeweza kuwavusha kwenda hatua ya mtoano, na Gabon walishindwa kutumia nafasi walizopata kuwafunika, na sasa wanajuta kwa kuanza mpira kwa shaka shaka.
Gabon hawakuamini kwamba mpira mkali wa kichwa uliopiga na nyota wa Borussia Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang haungetinga wavuni, lakini kipa Ovono alionesha uwezo wake kwa kuudaka. Gabon waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na uimara wa kikosi chao, walionekana kama vile wanacheza wenyewe na hawakuwa na ubunifu wa kutosha mara nyingi.
Kuelekea mwisho wa mchezo Gabon waliamka, wakapeleka mashambulizi mengi na kupata mipira kadhaa yaa dhabu ndogo, lakini kipa Ovono alikuwa sawa nao, kwa kuzuia pale akina Aubameyang na Frederic Bulot wa Charlton walipofanikiwa kuvusha mpira mbele ya mabeki wake.
Guinea ya Ikweta wanaungana na Kongo Brazzaville kuwa wa kwanza kuvuka hatua ya makundi, baada ya Kongo kuwatandika Burkina Faso 2-1 kwenye mechi ambayo Wabukinabe, hata hivyo, walitawala zaidi lakini wakashindwa kutumia fursa walizopata.
Hata wakati mechi ikielekea ukingoni mwa dakika 90, mabao yalikuwa 1-1, ambayo Kongo pia wangevuka, kwani baada ya Bifouma Koulossa kufunga katika dakika ya 51, Burkina Faso walilirudisha kupitia kwa Aristide Bance dakika ya 86, lakini dakika moja tu baadaye wakalizwa mchezaji Germain Sanou kuparaza mpira kwenye bega la Fabrice Ondama na kutinga nyavuni.
Kuvuka kwa Kongo kunaongeza heshima ya kocha wao, Claude LeRoy, aliyefanikiwa kuingiza timu robo fainali mara nane akiwa na mataifa matano tofauti. Kongo wamemaliza mechi tatu wakiwa na pointi saba, Guinea ya Ikweta tano, Gabon tatu na Wabukinabe moja, zikipungua mbili mbili toka juu hadi kwa aliyeshika mkia.
Comments
Loading…