Wakati soka ikitarajiwa kurejea kwa Ligi Kuu ya England (EPL) kumalizia mechi 92 zilizobaki kwa msimu huu wa 2019/2020, akili ya kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger imekuja na mambo mapya.
Ofisa huyo mpya wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) anasema kwamba wakati janga la virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu kuelekea kumalizika, klabu imara zitazidi kuimarika wakati zile nyonge zitazidi kwenye unyonge wake.
Akichambua juu ya ni kwa vipi gemu itakuwa baada ya kusimama tangu Machi mwaka huu, Wenger amesharejea Zurich, Uswisi kwa ajili ya kuendelea na mijadala juu ya namna bora ya kuendesha soka baada ya balaa hilo kubwa lililoitikisa dunia na kuua maelfu kwa maelfu ya watu.
Mkuu huyo wa maendeleo ya soka duniani yupo katikati ya majadiliano juu ya jinsi ya soka itakavyoendeshwa wakati ambapo moja ya nguzo zake muhimu – washabiki, hazitakuwapo hadi ligi kumalizika, kwani itakuwa wachezaji, makocha, waamuzi na maofisa wachache tu watakaoingia uwanjani, ambapo si zaidi ya watu 300 wataruhusiwa.
Wenger anasema janga ni kubwa, ambapo klabu kubwa zitaendelea kustawi na zile zitakuwa katika hali mbaya, kwa sababu hazina msuli mkubwa wala imara wa kifedha. Anasema kwamba ana shauku ya kuiondoa soka kwenye changamoto inazokabiliana nazo, akisema ana nia njema kabisa na klabu zote.
Kocha huyo ambaye ni mchumi kitaaluma na kwa kusoma, anasema kwamba ukitazama mchanganuo na utabiri wa mwekeleo wa masuala ya uchumi, tija itapungua kwa kati ya asilimia nane na 10 karibu kote Ulaya. Hata hivyo, Benki Kuu ya Ulaya inatabiri kwamba mambo yatakuwa chanya mwakani.
Kwa tafsiri ya Wenger, ni klabu kubwa na zilizo imara zitaweza kuimarika zaidi lakini zile dhaifu zitazidi udhaifu kwa muda. Anasema mabadiliko hayatakuwa makubwa sana kwa klabu kubwa japokuwa kwa zile ndogo yatakuwa makubwa na hasi.
“Tatizo kubwa kwenye gemu hii si kwa klabu kubwa, bali hizo za chini, na kwa hakika zitapata tabu sana, zitaathirika kwa kiasi kikubwa. Tatizo kubwa lipo huko chini kwa sababu klabu zimeachwa tupu kwa kiasi kikubwa,” anasema Wenger.
Anaongeza kwamba tatizo hilo halitakuwa kwa England, Ujerumani, Hispania, Ufaransa na Italia tu zenye ligi maarufu zaidi, bali litasambaa kote duniani na kazi yake anasema ni kusaidia kuhakikisha kwamba tatizo hilo linamalizika.
“Kuna kazi nyingi sana huko tunakokwenda. Naona sasa katika FIFA kuna tofauti kati ya Ulaya na maeneo mengine duniani na tofauti inazidi kuwa kubwa zaidi kadiri muda unavyokwenda. Kuna mengi yanayotakiwa katika maendeleo ya soka kuhakikisha tunapata mashindano zaidi kuanzia kwenye ngazi za chipukizi. Tunatakiwa kutafuta na kutenga fedha za dharura kwenye ligi ili kusaidia klabu ili ziweze kuvuka kwenye majaribu haya,” anasema Wenger.
Mfaransa huyu anaamini kwamba soka inaweza kuvuka kwenye janga hili na kuonesha njia kwa jamii nyingine juu ya jinsi watu na taasisi wanatakiwa kujiongoza wakati wa matatizo kama haya ya Civid-19.
“Tunazungumza sana juu ya ubaguzi wa rangi sasa. Soka imeegemea kwenye sifa tu – si kwenye wewe ni nani, unatoka wapi na unafanyaje kazi. Hiyo ni njia bora ya kuifundisha dunia jinsi tunavyotakiwa kujiongoza kitabia. Michezo, kwa ujumla, ni kiongozi mkubwa katika namna hiyo,” anasema Wenger.
Wenger ni mtu aliyesomea na kujiongoza kwenye masuala ya soka tangu utoto wake, anaijua ndani nje na sasa anasema imekuwa ngumu kukaa kwa muda mrefu bila mashindano – bila mechi kufanyika na sasa soka inarudi bila washabiki. Anasema matumaini yalikuwa madogo sana kwa jinsi ugonjwa ulivyokuwa ukizidi kusambaa na kuua watu. Anasema amekuwa na mikutano mingi kwa njia ya simu juu ya kipi cha kufanya kuondokana na hali hiyo mbaya.
Anasema kwamba England ni nchi ya kipekee kwenye soka kutokana na jinsi watu wanavyotoa mrejesho kwa yanayotokea, wakiwa na nguvu kubwa kwenye ushabiki na kufurahia kile kinachotokea uwanjani na kwamba ugonjwa huu umewaathiri sana washabiki ambao hawajaamini bado kwamba hawataweza kuingia viwanjani kushuhudia mechi.
Comments
Loading…