Awa mchambuzi wa soka
Kocha wa Arsenal amejitumbukiza katika uchambuzi kwenye kituo cha televisheni cha Ufaransa akiwa Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Baadhi ya washabiki wa Arsenal wameingiwa hofu kwamba muda mwingi anaotumia katika kazi hiyo ya pembeni utamchepua katika kusajili wachezaji muhimu.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, kazi hiyo inaweza kumpa fursa ya kuzama kuangalia wachezaji mahiri na pia kuwanasa kuanzia huko.
Mfaransa huyo anachambua mechi hizo kupitia Kituo cha TF1 cha nchini mwake.
Ikiwa Wenger na Washika Bunduki wa London wamepania kumwaga fedha katika usajili kwa ajili ya msimu ujao, hakuna kitakachowazuia hata kama Wenger angekuwa nyumbani kwao.
Inaelezwa kwamba Wenger amepewa ruhusa kutafuta wachezaji bora hata kama watavunja rekodi ya Mesut Ozil ya zaidi ya pauni milioni 40 alipochukuliwa toka Real Madrid msimu uliopita.
Arsenal sasa wamepata mikataba mipya ya wadhamini ambapo wanaingiza mamilioni ya pauni, hivyo hawana sababu ya kutosajili nyota.
Wenger ana nafasi ya kutazama moja kwa moja wachezaji chipukizi na wakongwe wanavyocheza kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, maana lazima anayo orodha ya majina tangu mapema.
Bado inaelezwa kwamba macho yake yapo kwa mshambuliaji wa AC Milan na Timu ya Taifa ya Italia, Mario Balotelli aliyefunga bao la ushindi dhidi ya England wiki iliyopita.
Comments
Loading…