Danny Welbeck ambaye alikuwa anarejea kwenye dimba la Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na Arsenal msimu huu, amegeuka kuwa shujaa wa mchezo wa leo baada ya kufunga bao la ushindi kwa upande wa Arsenal kutokana na makosa ya walinzi wa kati wa Manchester United.
Manchester United katika mchezo huo, walionekana imara sana hasa katika mashambulizi ambapo Angel Di Maria na Ashley Young ndiyo waliokuwa chanzo cha mashambulizi hayo kwa mipira yao ya krosi.
Kocha wa Manchester United, Loius Van Gaal alimuanzisha kwenye safu ya ulinzi Chriss Smalling, Marcos Rojo, Luke Shaw pamoja na Antonio Valencia lakini baada ya mapumziko, alimuingiza Michael Carrick ambaye alichukuwa nafasi ya Ander Herrera na Phil Jones akachukuwa nafasi ya Luke Shaw.
Arsenal walionekana tishio sana hasa kutokana na kasi ya Alexies Sanchez na Alex Oxlade Chamberline na kufanikiwa kupata bao la kuongoza Dk 25 kupitia kwa Nacho Monreal lakini mnamo dakika ya 29, Wayne Rooney alisawzisha kwa kichwa kutokana na krosi ya Angel Di Maria.
Phil Jones na Antonio Valencia walishindwa kuelewana na mnano dk 61 wakajikuta Valencia alirudisha pasi kwa Golikipa, David De Gea ambayo ilikuwa fupi na hapo ndipo Welbeck alipotumia makosa hayo kwa kuunasa mpira kisha kumpiga chenga De Gea kabla ya kufunga bao la pili na la ushindi.
Arsenal walionekana kuwa bora zaidi kwenye kiungo ambako Francis Cocquline, Mesut Ozil na Sant Carzola walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Pamoja na kuwa United ndiyo waliomiliki mpira kwa asimilia kubwa (58), bado pasi za uhakika kutoka kwa viungo hao kupeleka kwa mawinga wao ilionekana kuwa mwiba mchungu kwa Man United.
Baada ya beki wa pembeni wa Arsenal, Hector Bellerin kuonekana kuchoka lakini pia akiwa na kadi ya njano, Kocha Arsene Wenger aliamua kumpumzisha na kumuingiza Calum Chambers huku Aaron Ramsey akingia baada ya Chamberlain kuumia. Wenger pia alimuingiza Olivier Giroud kuchukuwa nafasi ya Danny Welbeck na kukamilisha idadi ya mabadiliko ya wachezaji wake.
Mchezo huo pia ulishuhudia madhambi yakifanyika mara 33 kwa pande zote mbili, huku United wakifanya mara 22 na Arsenal mara 11 kwa mujibu wa bbc.com. Hali hiyo ilipelekea kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kiungo mshambuliaji wa United, Angel Di Maria zikiwa zimesalia Dk 13 mchezo kumalizika.
Matokeo hayo yanawapeleka Arsenal kwenye hatua ya nusu Fainali ya kombe la FA ambapo wao ndiyo mabingwa watetezi na sasa watakutana na ama Bradford au Reading kwenye hatua ya nusu fainali. Kwa upande wa Manchester United, wao watajipanga sasa kuhakikisha wanapigana kupata nafasi ya kucheza klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao.
Comments
Loading…