*Savoy kocha mpya wa Gambia
*Al Ahly watimua kocha Garrido
Waziri wa Michezo wa Ivory Coast, Alain Lobognon ametimuliwa kazi huku uchunguzi ukiendelea juu ya kisa cha wachezaji waliotwaa ubingwa wa Afrika kutolipwa bonasi zao.
Lobognon mwenyewe amethibitisha habari hizo, akisema kwamba aliitwa na waziri mkuu wakazungumzia uamuzi kwamba anatakiwa aachie ngazi kwa maelekezo ya Rais Alassane Ouattara.
Lobognon amelazimika kuwajibika, kwani baada ya Ivory Coast kutwaa ubingwa huo mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta, wachezaji waliahidiwa bonasi lakini kumekuwapo urasimu katika kutoa fedha hizo.
Kutotolewa kwa haki hiyo kulisababisha kocha Herve Renard na kiungo Serey Die kuhoji hadharani kulikoni, wakati walikuwa wameahidi kuwawekea wachezaji na maofisa wa timu fedha kwenye akaunti zao.
Kulitokea kurushiana mpira baina ya wizara yenye dhamana ya michezo na Shirikisho la Soka la Ivory Coast, ndipo serikali ikaanzisha uchunguzi wa nani anakwamisha malipo hayo.
Serikali pia imemfukuza kazi meneja wa hazina aliyekuwa akihusika na utoaji wa fedha hizo, Patrick Yapi.
“Nakuhakikishieni kwamba uchunguzi umefanyika na bado unaendelea kubaini kiini cha mambo haya. Matokeo ya awali tayari yametoka na baadhi ya watu wameadhibiwa. Wote waliohusika wataadhibiwa,” Msemaji wa Serikali, Bruno Kone Nabagne anasema.
Timu hiyo ya taifa ya Ivory Coast, The Elephants, walishinda mechi ya fainali kwa kuwafunga Ghana 9-8 kwenye penati.
Rais Ouattara alifurahishwa na ushindi huo, ambapo kila mmoja kwenye kikosi cha watu 23 walipewa nyumba na pauni 34,000.
Viongozi wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast na maofisa wa benchi la ufundi la timu hiyo pia walipata kiasi hicho cha fedha, ambapo kwa ujumla serikali ilitoa pauni milioni mbili kutokana na ushindi huo.
Kabla ya kufukuzwa, Waziri Lobognon aliwatupia lawama wachezaji kwa kushindwa kuopa taarifa ofisi yake juu kwamba hawakuwa wamepata fedha zao.
GAMBIA WAPATA KOCHA MPYA
Gambia wamemteua kocha wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Raoul Savoy, kushika wadhifa huo kuiandaa timu yao kwa mashindano ya kimataifa.
Savoy (41) ataanza kazi yake kwa kuwaongoza The Scorpions katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.
Kocha huyo kutoka Uswisi ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi barani Afrika, ambapo amepata kufundisha Ethiopia na Swaziland.
Amepata pia kufundisha klabu za Morocco, Cameroon, Algeria na kwao Uswisi na ameahidi kuwapaisha Gambia kisoka.
“Napenda kuwahakikishia kwamba nitafanya kila niwezalo kuona kwamba Gambia wanafanya vyema kwenye soka. najua nitapata ushirikiano mzuri kwa sababu watu wa Gambia wanaipenda soka,” anasema Savoy.
Anachukua mikoba ya Peter Bonu Johnson ambaye mkataba wake ulitenguliwa. Gambia wamerejea kwenye mashindano ya Afrika baada ya kutumikia adhabu ya kutoshiriki kutokana na kudanganya umri wa wachezaji.
Kwenye michuano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika, Gambia wapo kundi moja na Afrika Kusini, Cameroon na Mauritania.
Wachezaji walio England, Modou Barrow wa Swansea na Mustapha Carayol wa Middlesbrough wanatarajiwa kuongoza kikosi cha wachezaji 21 pamoja na Pa Dembo Touray anayekipiga Santos ya Afrika Kusini.
The Scorpions wataanza kambi yao jijini Banjul Juni mosi na baadaye watasafiri hadi Kampala, Uganda kwa kambi zaidi na wanatarajia kucheza na Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes mwezi huo.
AL AHLY WATIMUA KOCHA
Mabingwa wa Misri, Al Ahly wamemtimua kocha wao, Juan Carlos Garrido kutokana na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika taarifa yao rasmi, vigogo hao wa Afrika waliotolewa na Moghreb Tetouan wa Morocco majuzi wamesema wanatafuta kocha mwingine.
Gorrido (46) ambaye ni raia wa Hispania amesema kwamba amejulishwa juu ya uamuzi kwamba hatakuwa kocha hapo msimu ujao, akisema amesikitishwa kutopewa muda kukamilisha mpango wake.
Kocha huyo aliajiriwa Julai mwaka jana na aliwaongoza mabingwa hao kutwaa Super Cup la Misri na la Afrika. Hata hivyo, alikuwa chini ya shinikizo kutokana na mwenendo wa timu kwenye ligi, wakiwa nafasi ya tatu, pointi 11 chini ya vinara Zamalek.