WATU WA SOKA KWENDA MAHAKAMANI HAKUEPUKIKI TANZANIA
HAKUNA ubishi kwamba Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) lilipotoa maelekezo kwamba masuala ya soka yasiingiliwe na serikali na yasifikishwe Mahakamani, lilikusudia kufanya soka ibaki soka ikiwa huru kabisa ikiamua mambo yake yenyewe na ikipanga mipango yake yenyewe.
Hakuna ubishi kwamba ukiingiza siasa za nchi kwenye soka, maendeleo ya mchezo huo yanaweza kwenda mwendo wa konokono kwa maana kwamba watu wa soka wanapanga mambo yao hivi, wanasiasa wanaweza kutoa maagizo tofauti kuwarudisha nyuma ingawa si kwa nia mbaya.
Mtu wa soka akikerwa na maamuzi fulani ya kisoka, kama serikali ikiwa na uwezo wa kushughulika na maamuzi ya kisoka, mtu huyu anaweza kuiomba serikali iingilie kati suala lile lililomkera, wakati vyombo vyenyewe vya soka vikishughulikia suala hilo hilo huku mwingine akipeleka suala hilo hilo Mahakamani. Katika mazingira hayo, kila kitu kinakuwa kwenye mkanganyiko na soka haichezwi bali kesi huku na kesi kule.
Kwa upande wa suala la kupeleka soka Mahakamani, kama FIFA ikiachia hali hiyo, kwanza, maamuzi ya soka ambayo mengi huzingatia matukio ya uwanjani, yataamuliwa Mahakamani ambapo sasa soka itakuwa si soka tena. Aidha, maamuzi sahihi ya kiuongozi wa soka yanayozingatia mitazamo ya kisoka yataamuliwa Mahakamani na aghalabu yanaweza kukosewa lakini maamuzi hayo ya Mahakama yatapaswa kuheshimiwa.
Aidha, suala jepesi la kutolewa uamuzi mara moja na vyombo vya soka linaweza kuchukua muda mrefu kuamuliwa na Mahakama huku hakuna mtu mwenye uwezo wa kuishinikiza Mahakama ifanye haraka kuhitimisha suala hilo la soka. FIFA imeyaona yote hayo na kuamua soka kutopelekwa Mahakamani.
Kwa kufanya maelekezo hayo yawe yanatekelezeka, FIFA imeanzisha ngazi tofauti za ndani ya nchi za kimaamuzi kuhusu migogoro na malalamiko ya soka ambapo ngazi ya juu zaidi ni ya kimataifa ambayo ni Court for Arbitration of Sport (CAS) ambayo kwa kifaransa ni Tribunal Arbitral du Sport (TAS)
Mfumo huo umeanzishwa ukizingatia jambo kubwa zaidi la kuhakikisha kwamba maamuzi yote ya ngazi tofauti za kimaamuzi yanakuwa ya haki pasipo chembe ya kuwa maamuzi haya yanambeba nani au yanamuangusha nani kinyume cha haki kwa kuzingatia matashi binafsi.
Kwa Tanzania maamuzi kadhaa ya kisoka hayazingatii haki bali matashi binafsi huku maagizo ya FIFA ya kuzuia soka kwenda Mahakamani na kulazimisha kesi za soka zipite njia maalum za vyombo vya maamuzi ya kisoka hadi CAS yakitumika kama silaha au kinga dhidi ya watoa maamuzi ya kibinafsi.
Vyombo vya maamuzi ya soka vya nchi hii vinatoa maamuzi kadhaa ya uonevu kabisa vikijua wazi kuwa mhusika hawezi kwenda Mahakamani na anapoenda mpaka CAS, jambo analolalamikia, kwa mfano haki ya kugombea uongozi, linakuwa limepitwa na wakati kwa maana kwamba kwa mfano uchaguzi unaolalamikiwa unakuwa umeshafanyika huku kesi huko CAS ikiwa haijaamuliwa.
Hii kwa Tanzania haishangazi kwani ni utamaduni hata kutoka miongoni mwa watu wanaostahili kuheshimiwa sana. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, mgombea wa chama cha upinzani jimbo la Shinyanga mjini alishinda kwa tofauti kubwa na matokeo kutangazwa, wafusi wake wakishangilia ushindi. Ghafla, ikitangazwa kura kuhesabiwa tena na mgombea wa chama tawala akatangazwa mshindi kwa tofauti ya kura moja, yaani moja kama hii (1)! Chama tawala kikashangilia ushindi ambao ni wazi ulikuwa wa kulazimisha ikithibitishwa na kutoweka mara moja kwa aliyetangaza matokeo hayo ya kulazimisha!
Kule Nzega nako katika uchaguzi wa mwaka huo huo, kwenye kura za maoni ndani ya chama tawala, aliyepata kura nyingi alikuwa mtanzania aliyezaliwa hapa na wazazi wa kisomali. Hakuwahi kuukana uraia wake wa Tanzania wa kuzaliwa lakini aliposhinda kura hizo za maoni akatangazwa si raia wa Tanzania bali Msomali! Yule wa pili, ambaye angestahili kupata nafasi hiyo baada ya chama tawala (si Uhamiaji) kumtangaza mgombea wa kwanza kuwa Msomali, hakuteuliwa na akapewa nafasi huyo wa mwisho. Baada ya kila kitu kumalizika na huyo aliyeshindwa kuwa ndiye mgombea ubunge, Mtanzania aliyepewa usomali akatangazwa kuwa raia halali wa Tanzania!
Kama chama kinachounda serikali kinacheza rafu kama hizo na nyingine nyingi tu, nani atashangaa TFF kufanya maamuzi ya rafu kwa matashi binafsi? Hata kama serikali ingekuwa na uwezo kikanuni kukemea rafu hizi za TFF, serikali gani ya kufanya hivyo wakati chama kilichoiunda kinaishi hivyo hivyo kwa rafu rafu?
Katika uchaguzi mkuu wa TFF ujao, wagombea wawili wa urais wa TFF wa kumrithi Leodgar Tenga, Mohammed Mkwarulo na Jamal Malinzi, wameondolewa kwa nyakati tofauti kwa sababu za kuungaunga na kumuacha mgombea mmoja, Athumani Nyamlani, apigiwe kura za “ndiyo” na “hapana”. Hoja za kuwatupa nje wagombea hao, hasa Malinzi aliyepotezewa kwenye ngazi ya rufani, ni hoja nyepesi mno na zisizo na msingi. Anaambiwa hana uzoefu wa miaka mitano kwenye uongozi wa soka wakati tangu mwaka 2001 alikuwa Mkurugenzi mmojawapo wa Yanga na baadaye katibu mkuu wa klabu hiyo kubwa ya soka ya Tanzania.
Mdau huyu wa soka ameondolewa pia kwa kuhoji uhalali wa katiba mpya ya TFF iliyopitishwa mpaka kusajili kwa msajili bila kupitishwa na mkutano mkuu wa TFF. Kuhoji kwake huko kumechukuliwa kama kupinga maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF. Mwenyewe anasema aliyehoji si yeye bali chama cha soka cha mkoa wa Kagera anachoongoza kama Mwenyekiti. Lakini hata kama yangekuwa mawazo yake, ni sheria gani duniani inayolazimisha watu kufikiri kama wanavyofikiri wengine? Au tunataka tuwe na TFF ya “yes men”, wasio na mawazo yanayojitegemea?
Mdau huyu anayeambiwa hana uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, aligombea wadhifa huu mwaka 2008 kwa kuonekana mzoefu lakini leo, miaka mitano baadaye, uzoefu umemtoweka!
Yote haya yamefanyika kwa sababu kamati iliyofanya maamuzi hayo ni ya mwisho na anayekerwa aende CAS huku uchaguzi ukifanyika chini ya siku 10 baadaye! Pia hayo yamefanyika kwa sababu anayekerwa na maamuzi hayo hawezi kwenda Mahakamani, FIFA imezuia.
Kwenye maonezi kama haya watu wa soka kwenda Mahakamani Tanzania hakuepukiki kwani ni huko tu haki itatendeka. Jamani, aliyezuia mambo ya soka kwenda Mahakamani alizingatia kuwa vyombo vya soka vingetenda haki na hakukusudia kutoa ngao au silaha kwa maamuzi tata ya kibinafsi. Watanzania tubadilike.
Comments
Loading…